Habari za Punde

Waziri Mahmoud: Tunawajengea kwa mwendo kasi kituo chenu cha afyaWaziri wa Afya Mh Mahmoud Thabit Kombo akikagua ujenzi wa kituo cha Afya kijiji cha Ngomeni, shehia ya Mgelema  Chakechake, Pemba

NA HAJI NASSOR, PEMBA

WIZARA ya Afya Zanzibar, imewaeleza wananchi wa Ngomeni shehia ya Mgelema wilaya ya Chakechake Pemba, kuwa ujenzi wa kituo chao kipya cha afya unatarajiwa kukamilika si zaidi ya miezi mitatu ijayo, kama mambo walioyapanga yatakwenda vyema.

Kauli hiyo imetolewa na waziri wa Wizara hiyo Mhe: Mahamoud Thabiti Kombo hivi karibuni, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kijijini hapo, ikiwa ni sehemu ya ziara yake alioifanya ghafla kuangalia ujenzi maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo.

Alisema baada ya ujenzi huo sasa kukabidhi wajenzi wa wizara yake, na kama vifaa walivyovipanga watavipata kupitia bajeti yao kuu, miezi mitatu ijayo, wananchi wa kijiji cha Ngomeni, wataanza kupata huduma za kiafya kama walivyowananchi wengine.

Waziri huyo alisema mikakati ya serikali kupitia Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015 hadi 2020 ni kuona wananchi wote wanapata huduma za kitabibu bila ya ubaguzi wa chama wala rangi ya watu.

Alisema ndio maana baada ya Rais wa Zanzibar kutembelea kijiji hicho na kutoa agizo la ujenzi wa kituo cha afya kijijini hapo, wizara yake ilijipanga haraka kutekeleza agizo hilo.

“Sisi kama wizara, kazi yetu ni kuwafikishia wananchi huduma za kiafya popote pale walipo, ingawa baada ya kiongozi wetu mpendwa kutoa agizo lake, na sisi twalitekeleza”,alifafanua.

Katika hatua nyengine Waziri huyo wa Afya, alisema baada ya ujenzi huyo kukamilika, wananchi wasiwe na wasiwasi wa upatikanaji wa dawa na madaktari husika.

Alisema tayari wameshapewa kibali cha kuajiria kati ya madaktari 300 hadi 350, ambapo mongoni mwao watatoa huduma kwa kituo hicho cha cha kijiji cha Ngomeni.

“Hivi karibuni tulishazungumza na mamlaka husika juu ya ajira za madaktari, hivyo kibali kimeshatoka na naamini tukiajiri basi na wananchi wa Ngomeni kupitia kituo chao cha Afya watafika”,alifafanua.’

Kuhusu nyumba ya dakatari kwa ajili ya Kituo hicho cha Afya, alisema baadae wizara itajenga nyumba ambayo itakuwa na uwezo wa kukaliwa na madaktari watatu kwa wakati mmoja.

Kwa upande wake fundi mkuu wa ujenzi wa Kituo hicho cha Afya Omar Maktuba, alisema kikosi kazi alichonacho cha mafundi 10 na vibarua 20, kama akipewa vifaa kwa wakati, hatarajii miezi mitatu ijayo bila ya kukabidhi jengo hilo.

“Ujenzi kwa sasa unaendelea vyema, maana msingi wa mwanzo “foundation” iliojengwa na mkandarasi tuliuvunja na sisi tumeshanza kwa kasi tokea August 17 mwaka huu, na kwa kikosi nilichonacho kazi hii itamalizika kwa muda mfupi ujao”,alisema.

Katika hatua nyengine fundi huyo Mkuu, aliwataka wananchi wa kijiji cha Ngomeni shehia hiyo ya Mgelema, kuwapa kila aina ya ushirikiano ili ujenzi huo ukamilike kwa wakati.


Wazo la kujenga kituo cha afya kijijini hapo, liliasisiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe: dk Ali Mohamed Shein, alipokitembelea kijiji hicho mwishoni mwaka jana.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.