Habari za Punde

Wafanyakazi wa umma walilia kifungu cha 58 kutotekelezwa
NA HAJI NASSOR, PEMBA

WAFANYAKAZI wa sekta za umma nchini, wamependekeza kusimamiwa kikamilifu kufanyiwa uchunguuzi wa afya zao kila baada ya muda, kama sheria ya Afya na Usalama Kazini no 8 ya mwaka 2005, ilivyoelekeza kwenye kifungu chake cha 58 cha sheria hiyo.

Walisema muajiri amekuwa makini na kulazimisha kumfanyia uchuguuzi wa kiafya, mtu anaetaka kumuajiri, ambapo hilo limetajwa kwenye sheria ya uajiri, ingawa baada ya ajira sheria ya Afya na Usalama Kazini ya kufanyiwa tena uchunguuzi, haitekelezwi.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti, wafanyakazi hao walisema, wapo baadhi yao wamekuwa wakimaliza muda wa utumishi, bila ya kufanyiwa uchunguuzi wa afya zao.

Walisema wanashangaa kuona sheria halali ipo, inayomlazimisha muajiri, kila baada ya muda kuwafanyia uchunguuzi wa afya, ingawa hilo limebakia kwenye vitabu vya sheria bila ya kutekelezwa.

Mmoja kati ya aliekuwa mfanyakazi wa wizara ya Afya Pemba sehemu ya udereva Suleima Mohamed Suleiman (74), alisema yeye tokea mwaka alioajiriwa mwaka 1977 na hadi alipostaafu miaka 35 baadae, hakumbuki kufanyiwa uchunguzi wa afya yake.

Alisema akiwa ndani ya utumishi, alikumbana na changamoto kadhaa, ikiwemo hata kukukosa likizo, fedha za nje ya wakati wa kazi, pamoja na kukosa kufanyiwa vipimo kila muda.

“Kwanza sijui kama kuna sheria inayomlazimisha muajiri kunichunguuza kiafya, naona nafanya kazi tu, sina likizo na hata ikitokezea naenda hospitali, basi gharama huwa zangu binafsi”,alifafanunua.

Nae aliekuwa dereva Kamisheni ya Utalii Pemba Khamis Sultan Hemed (67), anasema yeye alianza kazi mwaka 1971, lakini uchunguuzi wa afya, anakumbuka mwaka huo wakati anaajiriwa.

Hata hivyo dereva huyo aliestaafu mwaka 2000, alisema hana hakika kuwa waajiri, sheria hiyo ya Afya na Usalama Kazini hasa kifungu cha 58 ikiwa, wanakifahamu.

“Nilitarajia muajiri kifungu hicho akitekeleze, maana iwapo atakipuuza, atakosa mfanyakazi imara na mwenye afya bora, kwenye kutekeleza majukumu yake”,alieleza.

Mohamed Amran Massoud dereva Shirika la Utangaazaji Zabzibar ZBC Pemba, alisema kwenye wizara yake, yeye ameshashiriki zaidi ya mara nne, kufanyiwa uchunguuzi wa afya yake.

Mohamed Juma Rashid ambae ni Afisa Utumishi wa wizara hiyo, alisema kila mwaka wizara hiyo, imekuwa ikiwaleta madaktari, kwa ajili ya kuchunguuza afya za watendaji wake.

“Sisi hatukubali kuwaacha wafanayakazi bila ya kuwachunguuza afya, maana ndani yake tunapata kujua nani anapaswa kupangiwa kazi ngumu na nani hapaswi”,alifafanua.

Afisa Mdhamini wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Pemba Juma Bakari Alawi, alisema yeye tokea ashike nafasi hiyo mwaka wa pili sasa, hajawahi kuwafanyia uchunguzi wa afya wafanyakazi wake.

“Tatizo hasa ni ukosefu wa bajeti kwa ajili ya shughuli hiyo, lakini katika bajeti ijayo ya mwaka 2018/2019, tutaingiza kifungu maalumu, ili kuwafanyia uchunguuzi watendaji wetu”,alifafanua.

Afisa Mdhamini wizara ya Afya Pemba Bakar Ali Bakar, alikiri kuwa hata ofisi yake haijawahi kuwafanyia uchunguzi wa kiafya wafanyakazi wake, kama sheria hiyo inavyoelekeza.

“Kwa upande wa wizara yetu, sio tatizo la bajeti bali ni mifumo ya ndani ya wizara tu bado haijakaa sawa, lakini sasa tumeshajipanga na tutawafanyia”,alifafanua.

Wafanyakazi wa Wizara ya Miundombinu Pemba, Khamis Massoud na Asha Mohamed, walisema wao kila mwaka wamekuwa wakifanyiwa uchunguuzi wa afya zao, na imekuwa ikizaa matunda.

Waziri wa Nchi Afisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe: Haroun Ali Suleiman, alisema wakati sheria ipo, hakuna namna kwa waajiri bali ni kuhakikisha wanaitekeleza.

“Mkazo kwa waajiri wasiuweke tu wakati wanapotaka kuajiri ndio wawafanyie vipimo, bali hata baada ya muda kama sheria ilivyoelekeza wawafanyie uchunguuzi”,alifafanua.

Sheria ya afya na usalama kazini no 8 ya mwaka 2005 ambayo ina vifungu 133 na sehemu  13, kwenye kifungu chake cha 58 kimeeleza kuwa               
baada ya muda wafanyakazi watachunguuzwa afya zao na madaktari wenye sifa, ambao wataidhinishwa na Mkurugenzi”.

Aidha kifungu hicho kimeendelea kueleza kuwa, gharama za uchunguuzi zitalipwa na Muajiri.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.