Habari za Punde

Balozi Seif Azungumza na Kamati ya Michezo ya Watu Wenye Ulemavu wa Akili Kitaifa Tanzania.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kulia akiwa pamoja na Ujumbe wa Viongozi wa Kamati ya maandalizi ya Mashindano ya Kitaifa Tanzania ya Watu wenye Ulemavu  uliofika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kumtaarifu uwepo wa mashindano hayo Mwezi Disemba 2017 Visiwani Zanzibar.Kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh,. Mohamed Aboud Mohamed.
Msaidizi Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya Mashindano ya Kitaifa Tanzania ya Watu wenye Ulemavu  Maalim Mohamed  Mwinyi Ramadhan  aliyenyanyua Mikono, akitoa Taarifa ya uwepo wa mashindano ya michezo ya Watu wenye ulemavu Zanzibar. Wa kwanza Kulia ni Balozi Seif akichukua dondoo za maelezo na Msaidizi Mwenyekiti huyo wa Kamati ya maandalizi ya Mashindano ya Kitaifa Tanzania ya Watu wenye Ulemavu  Maalim Mohamed  Mwinyi Ramadhan.
Kulia ya Maalim Mohamed ni Katibu wa Kamati hiyo Mustafa  Nahoda, Bibi Salha Moh’d  Ali na Haidar Hasham Madeweya Wajumbe wa Kamati hiyo.(Picha na  - OMPR – ZNZ.

Na. Othman Khamis OMPR.                                                                                           
Zanzibar  imebahatika kuteuliwa Kitaifa kuwa  Mwenyeji wa Mashindano ya Michezo ya Watu wenye Ulemavu wa Akili Kitaifa Tanzania inayotarajiwa kufanyika  Mwishoni  mwa Wiki ya kwanza ya Mwezi ujao wa Desemba  Mwaka huu wa 2017.
Mashindano hayo yatafanyika kwa lengo la kufanya mchujo wa kuwapata Wanamichezo bora wa kuiwakilisha Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye michezo ya Dunia ya Olimpiki ya Watu wenye ulemavu inayotarajiwa kufanyika  Mwaka 2019 huko Abu dhabi.
Msaidizi Mwenyekiti wa  Kamati ya maandalizi ya Mashindano ya Kitaifa ya Watu wenye Ulemavu Maalim Mohamed  Mwinyi Ramadhan alieleza hayo wakati Wajumbe wa Kamati hiyo walipokutana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kumtaarifu uwepo wa mashindano hayo.
Maalim Mohamed alisema vugu vugu la maandalizi ya mashindano ya Michezo hiyo iliyoasisiwa  mwanzoni mwa Miaka ya 80 limeanza rasmi tokea mwanzoni mwa Mwaka huu, huku Zanzibar  ikiwa katika harakati za kupokea Wanamichezo 525 kutoka Tanzania Bara kati ya wanamichezo wote 700 watakaoshiriki mashindano hayo ya Kitaifa.
Alisema Zanzibar kwa vile imekuwa na uzoefu mkubwa wa kuibua wanamichezo bora imelenga  kutoa wachezaji wengi zaidi watakaojumuika kuunda Timu ya Taifa  ya Tanzania itakayoshiriki Mashindao hayo ya Abu dhabi.
Msaidizi Mwenyekiti  huyo wa Kamati ya maandalizi ya Mashindano ya Kitaifa ya Watu wenye Ulemavu alimueleza Balozi Seif aliyeambatana na Baadhi ya Mawaziri wanaohusika na sekta za Michezo, Elimu na Watu wenye mahitaji Maalum katika Kikao hicho kwamba jukumu la Zanzibar katika michezo hiyo ni kushughulikia  masuala ya usafiri pamoja na Malazi.
Hata hivyo Maalim Mohamed alisema bado Kamati yake  inaendelea kukumbwa na changamoto kubwa  ya upatikanaji wa fedha zitakazokidhi mahitaji ya gharama za Maandalizi hayo pamoja na Kambi ya Vijana walioteuliwa kujiandaa na mashindano hayo.
Wakitoa Mawazo yao Baadhi ya Mawaziri walioshiriki Kikao hicho waliishauri Kamati ya Maandalizi hayo kuzingatia tarehe halisi ya ufunguzi wa Mashindano hayo ambayo inaingiliana na sherehe za Uhuru wa Tanzania Bara zinazofikia kilele chake Tarehe Tisa Disemba.
Mawaziri hao walisema Viongozi wengi wa Kitaifa wakiwemo wale wanaotarajiwa kuteuliwa kuwa Wageni rasmi katika Mashindano hayo wanatarajiwa kushiriki Maadhimisho hayo kitendo ambacho kama Kamati hiyo haikuzingatia  mabadiliko  ya Tarehe, ushiriki wa Viongozi hao utakosekana.
Hata hivyo Mawaziri hao walisema kufanyika kwa Mashindano ya Michezo ya Watu Wenye Ulemavu Visiwani Zanzibar  ni muhimu kutokana na vugu vugu lake linalotoa taswira ya uwepo wageni wengi ambao kwa upande mwengine  husaidia kuimarika kwa Sekta ya Utalii.
Akitoa nasaha zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alivipongeza Vyama vinavyosimamia michezo mbali mbali hasa kile cha Watu wenye ulemavu kwa juhudi vinavyochukuwa katika kusaidia uimarishaji wa Sekta ya Michezo Nchini.
Balozi Seif alisema juhudi hizo kwa kiasi Fulani zimeonyesha mwanga wa kuunga mkono jitihada za Serikali kupitia Wizara inayosimamia Michezo za kurejesha vugu vugu la Michezo Visiwani Zanzibar katika azma yake ya kuirejeshea hadhi yake ya Kimataifa iliyofifia kwa miaka mingi iliyopita.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.