Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Shein Afurahishwa na Utendaji wa Wizara Hiyo Kwa Utendaji Kazi Wake.

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
  Zanzibar                                                                                                               03.11.2017
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameipongeza Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora na kueleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi ili kuutekeleza Utawala Bora kwa vitendo.

Dk. Shein aliyasema hayo leo, Ikulu mjini Zanzibar alipokutana na uongozi wa Ofisi ya Rais,  Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora  ilipowasilisha utekelezaji wa Mpango Kazi wake kwa  Mwaka 2016/2017, Mpango Kazi wa Utekelezaji kwa mwaka 2017/2018 na Utekelezaji wake kwa  kipindi cha robo ya kwanza ya Julai hadi Septemba, 2017.

Alieleza kuwa  furaha yake kwa kuonesha mafanikio makubwa yaliopatikana katika utendaji wa kazi uliowasilishwa na Ofisi hiyo na kueleza kuwa Ofisi hiyo ambayo inashugulikia Katiba, Sheria na Utawala Bora ina changamoto nyingi lakini hata hivyo ni vyema zikapatiwa ufumbuzi.

Aliongeza kuwa mbali ya kuwa na Utawala Bora lakini lengo la Serikali ni kutoa huduma bora na zenye kiwango kizuri ili wananchi wasinungunike na kuitaka Ofisi hiyo kuendelea kufanya vizuri zaidi katika kuwatumikia wananchi na kuwapa huduma zilizo bora.

Alileza kuwa katika nchi za Afrika Zanzibar ni miongoni mwa nchi za mwanzo zilizoanzisha Wizara ya Utawala Bora ambapo kwa hivi sasa Wizara hiyo imepata mafanikio makubwa sana hivyo, ni vyema ikaimarisha ubora na weledi wake.

Dk. Shein aliueleza uongozi huo kuwa pale wanaposikia malalamiko ya wananchi ni vyema wakayafanyia kazi na kuitaka Ofisi hiyo kuwasikiliza wananchi mawazo yao kwani ni njia moja wapo ya kufuata Utawala Bora.

Pia, alisisitiza suala zima la uwajibikaji sambamba na kuimarisha na kuendeleza ushirikiano na umoja miongoni mwa viongozi hao na watendaji wa Ofisi hiyo na kuitaka kuendelea kufanya kazi kwa kasi ili tija iweze kupatikana.

Nae Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd aliipongeza Ofisi hiyo kwa mafaniko iliyoyapata huku akisisitiza haja ya kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya suala zima la kupambana na vitendo vya rushwa na uhujumu wa uchumi.

Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliupongeza uongozi wa Ofisi hiyo kwa uwasilishaji mzuri wa Mpangokazi wake na kusifu mashirikiano mazuri anayoyapata kutoka Wizara hiyo ambayo yanamsaida katika utendaji wake wa kazi.

Waziri wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman alitoa shukurani kwa Dk. Shein kwa uongozi wake thabiti na shupavu unaowafanya wasaidizi aliowateua kwa imani kubwa kusimamia na kutekeleza majukumu yao kwa mujibu na sheria na taratibu zilizopo.

Alieleza kuwa utaratibu aliouanzisha wa Bangokitita ambao huwakutanisha na watendaji wakuu wa Wizara mbali mbali ni mzuri na unastahiki kupigiwa mfano kwa sababu unajenga kivitendo misingi ya Utawala Bora ambayo inahimiza masuala mazima ya uwazi na uwajibikaji.

Aidha, Waziri Haroun alisema kuwa  Mfumo wa kisasa wa usimamizi wa kesi kwa njia ya kielektroniki umewekwa katika Mahkama Kuu Vuga kwa maajiribio na utawekwa katika Mahkama nyengine zote Unguja na Pemba  kufikia mwaka 2020.

Katika kusimamia maadili yaa viongozi Waziri Haroun alaileza kuwa katika kusimamia maadili ya viongozi wa Umma elimu imetolewa kwa viongozi wa Umma kuhusu umuhimu wa maadili ya viongozi wa Umma, sheria ya Maadili ya Umma na utaratibu wa kujaza fomu za tamko la mali na madeni.

Aliongeza kuwa katika kuzuia vitendo vya rushwa  na uhujumu wa uchumi mikutano iliyolenga kukuza uelewa wa jamii kuhusu majukumu ya Mamlaka na umuhimu wa kuepuka vitendo vya rushwa ilifanyika kwa taasisi za Serikali Unguja na Pemba.

Nao uongozi huo ulipongeza hatua hizo za Rais za kukutana na viongozi na kujadili Mipangokazi ya Mawizara na kueleza kuwa mfumo huo umeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa na kupelekea baadhi ya nchi jirani kuufuatilia na kuanza kuuiga mfumo huo ambao Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar umeuanza kwa miaka sita hivi sasa.

Wakati huo huo, Dk. Shein alikutana na uongozi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais ambapo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mohamed Aboud Mohamed alimpongeza Rais Dk. Shein kwa namna anavyoiongoza Zanzibar ambapo kila mmoja anashuhudia mageuzi makubwa ya utendaji wa kazi kwa watumishi hasa katika sekta ya umma.

Aliongeza kuwa mageuzi hayo yamechochea kwa kiasi kikubwa maendeleo ya nchi katika sekta zote ambapo wasaidizi wake wote wanazingatia sana miongozo na maelekezo yake katika kutekeleza majukumu yao ya kusimamia shughuli za Srrikali katika maeneo yao.

Nae Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuipongeza Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais kwa mafanikio iliyoyapata pamoja na kuwasilisha vyema Mpangokazi wake.


Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.