Balozi wa
Kuwait nchini Tanzania Mhe. Jassem Al Najem akikabidhi kompyuta za mkononi kwa
walimu wakuu wa baadhi ya shule zilizoko katika jimbo a Tunguu Wilaya ya Kati
Unguja. Katikati ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mmanga Mjengo
Mjawiri, akifuatiwa na Mwakilishi wa jimbo hilo Simai Mohammed Said.
Balozi wa
Kuwait nchini Tanzania Mhe. Jassem Al Najem akikabidhi kompyuta za mkononi kwa
walimu wakuu wa baadhi ya shule zilizoko katika jimbo a Tunguu Wilaya ya Kati
Unguja. Katikati ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mmanga Mjengo
Mjawiri, akifuatiwa na Mwakilishi wa jimbo hilo Simai Mohammed Said. (Picha na
Salum Vuai, MAELEZO ZANZIBAR).
Na
Salum Vuai, MAELEZO
UBALOZI
wa Kuwait nchini Tanzania, umezizawadia skuli mbalimbali zilizomo katika jimbo
la Tunguu kompyuta 20 za mkononi (Laptops) na printa kumi ili kuwaongezea maarifa
ya kielimu walimu na wanafunzi.
Makabidhiano
ya kompyuta hizo yalifanyika Disemba 14, 2017 katika kituo cha walimu Dunga
Wilaya ya Kati, ambapo Balozi wa Kuwait Jassem Al Najem akishirikiana na
Mwakilishi wa jimbo la Tunguu Simai Mohammed Said.
Aidha
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mmanga Mjengo Mjawiri, alihudhuria
hafla hiyo akiwa mgeni rasmi, pamoja na Mbunge wa jimbo hilo Khalifa Salum
Suleiman, maofisa kadhaa wa elimu pamoja na masheha.
Akizungumza
na washiriki wa hafla hiyo, Mjawiri alitaka vifaa hivyo vitumike katika njia
sahihi ya kuendeleza elimu badala ya matumizi yaliyo kinyume na maadili
na silka za Mzanzibari.
Alisema
kompyuta hizo zitakapofika katika skuli zilizokusudiwa, zitumike kutafuta mambo
ya kielimu yatakayorahisisha usomeshaji kwa walimu na usomaji kwa wanafunzi.
“Hatutaki
zitumike kama pambo bali zifanye kazi iliyokusudiwa ya kutafuta elimu. Ni
matarajio yetu baada ya mwaka mmoja tutaona mabadiliko katika maendeleo ya
elimu jimboni humu, nasi Wizara ya Elimu tutakuwa tukifuatilia kuona tafauti
kati ya sasa na baadae,” alieleza Naibu Waziri huyo.
Aidha
alisema Wizara yake itaendelea kutimiza wajibu wake pale hali itakaporuhusu
kusambaza na kuongeza vifaa kama hivyo katika skuli mbalimbali za Unguja na
Pemba.
Mjawiri
alimpongeza Mwakilishi wa jimbo hilo kwa juhudi anazochukua kwa kutafuta
vianzio mbalimbali vya maendeleo, akisema anaamini baada ya miaka mitano Tunguu
itakuwa mfano mzuri kwa majimbo mengine kujifunza kutokana na ufanisi wake.
Naibu
Waziri huyo wa Elimu hakuacha kuwakumbusha wazazi na walezi, umuhimu wa kuwa
karibu na watoto wao ili kuhakikisha hawadhuriwi na vitendo vya udhalilishaji
na ubakaji kwa wanawake na watoto vilivyoshamiri nchini kwa sasa.
Aidha
alimshukuru Balozi wa Kuwait Jassem Al Najem kwa msaada huo muhimu,
akisema umeonesha mapenzi makubwa aliyonayo kwa wanafunzi na wananchi wa
Zanzibar.
Kwa
upande wake, Balozi Al Najem alisema vifaa hivyo vyenye thamani ya shilingi
25,000,000, si msaada bali ni zawadi kutoka kwa wananchi wa Kuwait kwa ndugu
zao wa Zanzibar ili viwasaidie katika kuchimba hazina ya elimu.
Aidha
alieleza kufurahishwa na mapokezi aliyopata kutoka kwa wananchi wa jimbo hilo,
na kuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na
jimbo hilo kwa kupeleka aina tafauti za miradi jimboni humo ikiwemo pia sekta
ya michezo.
Alieleza
kuwa utoaji wa vifaa hivyo ni katika kuunga mkono mradi ulioanzishwa na ubalozi
wa nchi yake uliopewa jina la ‘KUELEKEA ELIMU BORA ZAIDI’.
Alitumia
fursa hiyo kuwapa pole familia, serikali, Jeshi la Wananchi wa Tanzania na
wananchi wote kwa msiba mkubwa wa kuuwawa kwa wanajeshi huko Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo Disemba 7, 2017.
Mwakilishi
wa Tunguu Simai Mohammed Said akimshukuru balozi huyo, alisema anaamini vifaa
hivyo vitasaidia kukuza vipawa vya elimu kwa walimu na wanafunzi, ili waendane
na kasi ya mabadiliko ya teknolojia duniani.
Alisema
kwa kushirikiana na viongozi wengine wa jimbo wakiwemo madiwani na taasisi za
serikali, wataendelea kuzitafutia ufumbuzi hatua kwa hatua changamoto
mbalimbali za jimbo hilo ili kuliletea maendeleo zaidi na kuinua ustawi wa watu
wake.
No comments:
Post a Comment