Habari za Punde

Ukataji miti unavyoathiri mazingira kisiwani Pemba


 VIONGOZI wa Jumuiya ya Sanaa Elimu ya Ukimwi na Mazingira Kisiwa Pemba, wakiwawaonyesha waandishi wa habari eneo ambalo liko wazi na wanakusudia kulipanda miti ya mikoko 400,000 ili kurudisha asili ya eneo hilo(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)

BAADHI ya wananchi wa Kisiwa Panza wakipanda miti ya mikoko katika maeneo ya wazi, yaliyoathiriwa kufuatia ukataji wa miti na kupelekea kuwa jangwa.(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)
 MITI ya mikandaa au Mikoko ikiwa imenawiri vizuri, katika moja ya maeneo yaliyomo ndani ya kisiwa Panza, miti hiyo imepandwa kwa nguvu za wananchi kwa lengo la kukinusuru kisiwa chao(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)

NA ABDI SULEIMAN, PEMBA.

PEMBA ni miongoni mwa visiwa vilivyozungukwa na bahari, nacho kikiwa kimezungukwa na visiwa vidogo vidogo vikiwemo Fundo, Njau, Funzi, Panzi, Misali, Makoongwe, Kisiwa Panza na Kojani.

Kwa mujibu wa Matokeo ya Sensa ya watu na makaazi Tanzania 2012, Zanzibar inaidadi ya watu 1,303,568, Unguja ina watu 896,720, Kisiwa cha Pemba kina Wakaazi 406,848 na eneo lenye ukubwa wa 980KM2, katika ramani ya dunia, pemba ipo baina ya Latitudo 40 80’na 50 30’ s, Longitudo 3900 35’ na 3900 50’E, pia ina urefu wa Mail 40 kutoka kaskazini hadi kusini.

Suala la uharibifu wa mazingira, juu ya ukataji wa miti ya mikandaa na miti ya juu, kwa shuhuli za ujenzi, kuni na upigaji wa tanu ya mkaa, zimeshababisha maji ya bahari kupanda katika mashamba.

Uharibufu wa mazingira kwa kiasi kikubwa ndio unaosababisha mabadiliko ya tabianchi, Kisiwa Panza kipo Chokochoko Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba, kikiwa kwa kiasi kikubwa kimeathirika kutokana na ukataji wa miti.

Mwaka 1994 makaburi yanayosadikiwa kuwepo tokea mwaka 1880 Yalifukuka na kupatikana kwa mabaki yake, baada ya kunyesha mvua kubwa na maji ya bahari kupanda juu. Hali hii ilitokea baada ya wananchi kujisahau na kukata miti bila ya mpangilio na maji ya bahari kuvamia maeneo ya kilimo.

Mwandishi wa makala hii alilazimika kufunga safari ya saa moja na nusu, kwa kutumia usafiri wa daladala ya abira kutoka Chake Chake hadi ChokoCho, baada ya kufika chokocho likoni ndipo muda wa dakika 5 zikatumika kwa usafiri wa mashua kwenda Kisiwa Panza.

“Ufahamu wangu mimi baba yangu alikuwa analima eneo hili, sahivi tizama mwandishi…………. Wewe si umekuja kuona tulivyoathirika na ukataji wa miti……………hata ufanye nini hapawi kitu hapa”

Mwajuma Ali Hassan (22) anasema suala la ukataji wa miti limewaathiri sana wakulima, kwani kwa sasa mazao kutoka mashambani yamepungua kutokana na mashamba hayo kujaa maji ya bahari.

“Mashamba yamegeuka majangwa baada ya kuingia maji chumvi, kufuatia wananchi kukata miti bila ya kikomo na kusahau kuwa kisiwa kimezungukwa na bahari,” ameleza Mwajuma.

Ukataji wa miti ovyo umepelekea maisha ya wananchi kuwa rehani, baada ya eneo lenye ukubwa wa hekta 200 kuingiwa na maji chumvi.

Ndani ya eneo hilo kuna mashamba, skuli na makaazi ya watu na vyote vimeathirika kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Naye Abdalla Khalfan Khamis (59), ananeleza kuwa kisiwa kilikuwa na miti yakutosha, ardhi iliyojaa rutba na kinachopandwa kinatia, sasa mambo yamekuwa kombo.

“Ukataji na uvunaji wa miti umekuwa mkubwa, miti mikubwa mikubwa imeteketea kwa wingi, upandaji wake umekuwa mdogo kutokana na wananchi kutokuwa tayari kukinusuru kisiwa chao,” anasema Khamis.

Takriban yapata miaka 20 tokea maji ya bahari kuvamia mashamba ya kilimo, kusababisha wananchi kukosa sehemu za kulima na hivyo kuingia katika shughuli za uvuvi  wa kaure, ukulima wa mwani na uvuvi wa Pweza.

Tashdidi Zubeir (75) ambaye kwa asili alikuwa mkulima, anaeleza kuwa chumvi kuvamia maeno ya kilimo, kumesababisha wakulima kuhama katika mashamba yao na kuingia katika shuhuli nyengine za kujitafutia kipato.

“Wakulima walikuwa wanapata  mazao mengi, ya aina mbali mbali, lakini kwasasa hali imekuwa tofauti kutokana na ukataji wa miti, hakuna tena kinachopatikana, ndiyo maana watu wengi wameamua kujishughulisha na uvuvi,” anasema mzee Zuberi.

Anaelezakuwa umaskini umechangia kwa kiasi kikubwa, kwa wananchi kuharibu Mazingira, “Vijana wanakata miti ovyo, wanapiga tanu za chokaa, wanakata kuni na miti ya kujengea kwa madai kuwa wamekosa ajira.”

“Wasiwasi wangu uko katika daraja lililotenganisha Ndooni na Panza, mwandamo wa mwezi maji hufunika daraja na kuzuwia wananchi kupita kwa muda,”alisema.

Wanafunzi nao hawakuwa nyuma kuzungumzia athari ya ukataji wa miti katika kisiwa hicho, Abdullhalim Abdalla Abdalla (20) ni mwanafunzi wa kidato cha tatu katika skuli ya Sekondari Kisiwa Panza, anasema athari kubwa imetokeakwa kuwa maeneo mengi yameingi maji ya bahari, ikiwemo maeneo ya skuli.

“Tulichukua juhudu ya kupanda miti 2,000, katika maeneo ya skuli ikiwemo mikoko, Zamani maji yalikuwa mbali lakini sasa hivi yameanza kuingia katika eneo la skuli, Ingawa serikali imejenga ukuta kwa saruji bado maji yamebuni sehemu nyengine yakuingia”alisema.

Mwanafunzi mwingine, Amina Hamad Makame (17), anaeleza kuwa mabadiliko ya tabia nchi yameathiri sana sehemu za skuli, kwani wakati wa  bamvua kubwa  wanafunzi hushindwa hata kupita darajani kwa ajili ya kwenda skuli.

“Ni vema wananchi waache  tabia ya ukataji miti ovyo, ili kunusuru kisiwa chetu, watoto wanaokuja nao waweze kuona matunda na sio kuwatupia lawama wazazi wao.”

Mwalimu wa mazingira katika skuli ya Kisiwa Panza Msingi, Salti Salim Abdalla (32) amesema inafika miaka mitatu wakuliama wanakosa sehemu za kulima, ameshauri jamii  kupanda miti kwa wingi karibu na eneo la skuli, ili kupunguza athari za kimazingira zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi.

“Sisi tuliweza kupanda miti ya mikoko 3000, mivinje na mikungu, Miti hii imesaidia kupunguza kasi ya maji kupanda juu katika eneo la skuli,”alisema.

“Miaka 10 iliyopita maji yalikuwa umbali wa kati ya mita 150 na 170 kufika eneo la skuli, sasa yapo mita 100, Shughuli za kilimo zimeathiriwa kwa kiasi kikubwa na maji chumvi,” aliongeza.

Akizungumzia athari za mabadiliko ya tabianchi, Shekh Faki Makame Faki(56) ambaye ni imamu wa msiki katika kisiwa Panza, anansema Kisiwa Panza kimeathirika kutokana na ukataji wa miti.

Kuongezeka kwa maji kumepelekea makaburi kufufuka, ikiwa ni athari nyingine ya mabadiliko ya tabianchi, athari nyingine iko upande wa kilimo, ambako hakuna mazao yanayostawi kwani kila kinachopandwa hakioti, baada ya maji ya chumvi kuingia katika mashamba.

“Uharibifu wa mazingira hasa ukataji ovyo wa miti ni tatizo lililokifikisha kisiwa kilipo, Mafuvu ya maiti yanafukuka katika makaburi na  saivi eneo hilo limekuwa jangwa tu,” anaeleza.

Sheikh Faki ameongeza kuwa wakati umefika wa kutumia mazingira kwa umakini na kwa namna endelevu, ili kuwafaa na vizazi vijavyo.

Mratib wa Jumuiko la Mabadiliko ya Tabianchi Zanzibar (ZACCA), Habiba Juma anasema suala la uhifadhi wa mazingira ni jukumu la kila mtu na sio taasisi moja tu, amewataka wananchi kuendelea kupanda miti kwa wingi, ili kuzuwia maji ya bahari kuvamia maeneo ya kilimo.

“Kisiwa cha Pemba kina maeneo mengi ambayo yameathiriwa na uharibifu wa mazingira, Kasi ya kukata miti kwa wingi ni kubwa kuliko juhudi za wananchi kupanada miti mingine,” anaeleza mratib wa ZACCA.

Katika kukabiliana na hali ya uharibifu wa mazingira, ZACCA kwa kushirikiana na wananchi wamepanda miti ya mikandaa 25,565 katika maeneo ya Wambaa, Tumbe na Mgelema.

Katibu wa Jumuiya ya Sanaa Elimu ya Ukimwi na Mazingira, (JSEUMA) Pemba, Juma Ali Mati, anasema mwaka 2015 walielimisha wananchi 200 juu ya suala la mabadiliko ya tabianchi, juu ya ukataji wa Kuni, upigaji wa tanu za chokaa na mkaa, waliopata mafunzo hayo walitoka kijiji cha Kangani, Chokocho, Makoongwe, Kuku na Mwambe.

Katika kipindi hicho miti 6,550 ya mikoko imepandwa kwa hatua ya Kwanza, Katika awamu ya pili miti 6,800 ilipandwa katika kisiwa cha Matumbilini na ufunguni, Mwaka  2016 miti ya juu 22,000 na miti mingine 4,000 imepandwa kisiwa cha matumbilini.

“Miti 16,000 ilipandwa kisiwa cha Ufunguni, ambapo miti mingi eneo hilo jamii wanaitumia vibaya, huku miti 100,000 imepandwa katika maeneo tafauti ya kisiwa Panza,” aliongeza katibu huyo.

Mwaka 2017 mradi wa LDCF umeweza kupanda miti 400,000, baada ya uhamasishaji walipanda 650,000 katika eneo la Mto wa Kae, Madauni, Ufunguni na Bandarini Juu, huku wakitarajiaa kupanda miti ya juu 300,235, kabala yam mwaka huu kumalizika.

“Lengo letu  ni kudhibiti athari zisiendele kuharibu kisiwa chetu, Mradi umejenga kuta mbili kubwa katika eneo lililokuwa linaingia maji chumvi, ambapo kwa miaka 12 mashamba hayo yanayolimwa na kaya 50 hayatumiki kwa kilimo,”alisema Mati.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Mali Zisizorejesheka Zanzibar, Soud Juma Mohamed, alisema kitu cha msingi katika kudhibiti maji chumvi ni kupanda miti ya mikandaa katika maeno ya baharini, ilikuzuwia kasi ya maji kuingia mashambani.

Kwa upande wake mkuu wa idara ya misitu na mali zisizorejesheka Pemba, Said Juma Ali, anasema ni miaka 10 sasa wamejikita katika upandaji wa miti ya mikandaa na miti mengine, ikiwemo kuanzisha misitu ya jamii kwa lengo la kuhifadhi mazingira.

“Athari za mabadiliko ya tabianchi katika Kisiwa Panza ni kubwa, Eneo kubwa lilikuwa na misitu ya mikandaa ambayo ilikuwa inapunguza nguvu ya maji kuja juu, Miti mikubwa iliyokuwa na nguvu imekatwa, nguvu ya maji kuja juu imeongezeka, hususan upande wa kusini kwenye bahari kuu,”alisema.

Kukatwa kwa miti kumepeleka athari kubwa katika upatikanaji wa maji safi na salama, kwani visima vya jamii vimekauka na pia kilimo cha mihogo kimeathirika kutokana na hali hiyo.

Mkuu wa Idara ya mazingira Pemba, Mwalim Khamis Mwalimu, alisema jumla ya Mikoko 412,436 imepandwa na lengo ni kupanda miti 400,000 katika Kisiwa Panza, Maeneo 123 yamevamiwa na maji chumvi katika Kisiwa Panza,  ambayo ni sawa na hekta 200, Matarajio ni kupanda miti ya juu 2000.

Mtaalamu wa uhifadhi wa miti ya mikandaa Pemba, Salum Khamis Haji, anasema kuwa Kisiwa Panza kinavamiwa na watu kutoka maeneo mbali mbali ikiwemo, Nungwi na Mkokotoni ambao wanakata miti ya kujengea kutoka kisiwani hapo.

Katika jitihada za kuhakikisha kisiwa kinaendelea kuwepo, wastaniwa miti 335,000 imepandwa katika hekta 67 hadi sasa, “Suala la upandaji miti na uhifadhi wa mazingira ni jukumu letu sote, hivyo mikakati madhubuti inahitajika kuhakikisha kisiwa cha Pemba, kinaendelea kuwepo katika ramani ya dunia kwa kupanda miti kabla ya kukata mti.”

MWANDISHI WA MAKALA HAYA ANAPATIKANA KWA EMAIL:abdisuleiman33@gmail.com
SIMU:+255718968355.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.