Habari za Punde

Wizara ya Afya Zanzibar yaendesha mafunzo ya huduma ya kwanza kwa madereva wa gari za kubeba wagonjwa

 Mkuu wa Usafiri Wizara ya Afya Zanzibar Ali Nassor Juma  akitoa maelezo ya mafunzo ya huduma ya kwanza waliyopewa madereva wa magari ya Ambulance yaliyosimamiwa na Chama cha Msalaba Mwekundu (Red Crooss) katika sherehe za kuyafunga mafunzo hayo yaliyochukua wiki moja yaliyofanyika Karakana kuu ya Wizara ya Afya Mombasa, Mjini Zanzibar
 Madereva wa gari za Ambulance wakitoa huduma ya kwanza  wa majeruhi alievunjika mguu katika sherehe za kukabidhiwa vyeti baada ya kumaliza mafunzo yao yaliyofanyika Karakana kuu ya Wizara ya Afya, Mombasa Mjini Zanzibar.(anaetoa maelekezo) ni Afisa mafunzo kutoka Red Cross Ali Haji Khamis

 Madereva waliopatiwa mafunzo wakionyesha njia bora za kumbeba mgonjwa kwa kutumia kiti cha kawaida katika sherehe za kumaliza mafunzo yao na hatimae kukabidhiwa vyeti.
 Madereva walioshiriki mafunzo ya huduma ya kwanza wakimsikiliza mgeni rasmi Mkurugenzi Uendeshaji na Utumishi wa Wizara ya Afya Ramadhani Khamis Juma (hayupo pichani)
Mkurugenzi Uendeshaji na Utumishi wa Wizara ya Afya Ramadhani Khamis Juma akimkabidhi cheti cha kumaliza mafunzo ya huduma ya kwanza dereva Salum Abdall Salum katika sherehe zilizofanyika Mombasa Mjini Zanzibar

Picha na Makame Mshenga.

Na Ramadhani Ali – Maelezo                                         

Wizara ya Afya Zanzibar imeanza utaratibu wa kuwapatia mafunzo ya huduma ya kwanza madereva wake 43 wa magari ya kuchukulia wagonjwa (Ambulance) yenye lengo la kuwawezesha kusaidia matibabu ya awali kabla ya mgonjwa kumfikisha kwa daktari.

Akizungumza katika sherehe za kuwapa vyeti madereva 12 wa  awamu ya kwanza waliomaliza mafunzo  yao yaliyofanyika Karakana kuu ya Wizara ya Afya iliyopo Mombasa, chini ya usimamizi wa Red Cross, Mkuu wa Usafiri wa Wizara hiyo Nd. Ali Nassor alisema awamu ya pili ya madereva 11 wa Unguja wataanza mafunzo wiki ijayo na madereva 20 wa Pemba wataanza kupatiwa mafunzo ya huduma ya kwanza tarehe 18 hadi 29 mwezi huu.

Ali Nassor alisema mafunzo hayo yanayosimamiwa na Chama cha Msalaba Mwekundu (Red Cross) yameanza kuonyesha mafanikio makubwa na ameishauri Wizara ya Afya kuyafanya kuwa endelevu.

 Aliitaka Wizara kutenga fungu maalumu katika bajeti yake ya kila mwaka kwa ajili ya mafunzo ya madereva na wafanyakazi wa kanda nyengine ambazo hazipewi nafasi kubwa katika suala la mafunzo.

Alisema utaratibu huo utasaidia kuongeza ushirikishwaji wa moja kwa moja wa huduma za afya kwa wafanyakazi wengine wa Wizara hiyo na wananchi wengine katika hatua za awali na hivyo kupunguza ulemavu ambao sio wa lazima kutokea.

Mkurugenzi Uendeshaji na Utumishi katika Wizara ya Afya Ramadhani Khamis Juma ambae alikuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo alisema suala la mafunzo kwa wafanyakazi wa kada mbali mbali ni muhimu na Wizara itaendelea kutilia mkazo.

Aliwashauri madereva waliopatiwa mafunzo hayo kuyatumia kikamilifu na kuwataka kuwa na tahadhari  wanapokuwa wanasafirisha wagonjwa ili isitokee gari lenye mgonjwa linapata ajali.

Mkurugenzi Ali Nassor aliwakumbusha madereva wa Ambulance kuyatumia magari hayo kwa kazi iliyokusudiwa ya kuchukulia wagonjwa na kuwa na kitabu cha safari  (Log book) ili kuwa na kumbukumbu sahihi za safari walizokwenda, muda waliotumia na mafuta yaliyotumika.

Madereva hao walionyesha mbinu mbali mbali walizofundishwa za kuwasaidia wagonjwa na majeruhi wakati wa kuwasafirisha kuwapelekea Hospitali na vituo vya afya.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.