Timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes itakutana na Uganda katika nusu fainali ya Kombe la Cecafa.
Uganda iliyoibuka mshindi katika kundi lake inakabiliana na Zanzibar
iliyoibuka mshindi wa pili baada ya kupoteza mchezo wake wa mwisho na Libya
ambapo wangeweza kuiepuka Uganda na kukabiliana na Burundi ambao wameibuka
waashindi wa pili.
Katika nusu fainali nyengine wenyeji Kenya watavaana na Burundi.
Michezo yote ya nusu fainali itafanyika katika Uwanja wa Kisumu siku ya
Alkhamisi tarehe 14/12/17 wakati fainali itafanyika katika mji wa Machakos siku
ya Jumapili tarehe 17/12/17
Uganda Cranes wamewahi kukutana na Zanzibar Heroes mara 14 ambapo Cranes
wameweza kushinda mara 12 kutoka sare mara moja na kupoteza mara moja.
Timu ya Taifa ya Zanzibar iliwahi kushinda mara moja tu Kombe la Cecafa mwaka 1995 ambapo iliwaondoa Waganda kwa
kuwafunga 1-0 goli lililofungwa na Victor Bambo.
Zanzibar Heroes imeweza kuwashangaza wengi katika mashindano ya Cecafa
mwaka huu huku wakionesha kandanda safi inayotegemea pasi fupi fupi na
wachezaji wenye kujituma wakiwa uwanjani huku wakijua majukumu yao.
Licha ya rekodi kuonesha Uganda Cranes wana rekodi nzuri dhidi ya
Zanzibar Heroes hata hivyo kikosi cha Heroes mwaka huu chini ya Kocha Hemed
Morocco kina uwezo wa kuigeuza historia hii na kuwafurahisha wazanzibari kwa
kuiondoa Uganda na kuingia Fainali.
Katika Soka kila kitu kinawezekana hivyo uwezo wa kuwafunga Uganda tunao
na ninaamini wachezaji ari wanayo na Zanzibar kwa ujumla inaamini hivyo.
Timu ya Zanzibar Heroes imepita katika majaribu ya wachezaji wake
kupimwa mkojo wakidhaniwa kutumia madawa ya kuongeza nguvu hasa ukizingatia
uwezo wao walioweza kuonesha uwanjani kuwashangaza wengi mpaka Cecafa kuamua
kuchagua wachezaji wane wa timu kupimwa mkojo ambapo vipimo vyao vimepelekwa
Afrika Kusini kwa uchunguzi zaidi
Ninaamini Kocha Morocco pamoja na benchi lake la ufundi litawajenga
vijana kisaikolojia waweze kuondokana na kasumba hii na kuwaweka tayari kwa
mechi ya kesho na kufanya kile ambacho taifa la Zanzibar limewatuma kwenda
kukifanya na kuiletea heshima Zanzibar na kutuma ujumbe kwa vitendo CAF na FIFA
kwamba Zanzibar soka lipo na tulipoomba
kujiunga hatukubahatisha.
Wazanzibari kwa pamoja tuwaunge mkono Timu yetu kwa hali na mali kwani
sehemu pekee ambapo wimbo wetu wa Taifa la Zanzibar na bendera ya Taifa la
Zanzibar hutumika nje ya visiwa hivi ni pale vijana wetu wanaposimama kuimba
kwa moyo wa uzalendo wakituwakilisha na kuthibitisha kwamba Zanzibar haitoweza
kufutika katika medani ya Soka.
Kama kawaida blog ya ZanziNews inawatakia Heroes kila la kheri na sote
tuwe pamoja kuiombea dua iibuke na ushindi kuzidi kuwafurahisha Wazanzibari na
kuijengea heshima nchi yetu.
Go Zanzibar Heroes Go!
Kila la kheri Zanzibar Heroes
No comments:
Post a Comment