Habari za Punde

Balozi Seif awapongeza watendaji walio chini ya Wizara yake

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Uongozi wa Ofisi yake kuwapongeza kwa kazi kubwa ya kukamilisha Uandishi wa Hotuba ya SMZ ya Utekeleza wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Kushoto ya Balozi Seif  ni Naibu Waziri Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mihayo Juma N’hunga na Katibu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Bibi Raya Issa Mselem.

Kulia ya Balozi Seif ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Dr. Idriss Muslim Hijja, Naibu Wake Nd. Ahmad Kassim,  Mkurugenzi Utumishi Bibi Halima Ramadhan Taufiq na Mkurugenzi wa Uchapaji Nd. Mohamed Suleiman Khatib.
Naibu Waziri Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Mihayo Juma N’hunga aliyesimama akitoa shukrani kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.

Picha na – OMPR – ZNZ

Na Othman Khamis Ame

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kazi kubwa iliyofanywa na Taasisi za Serikali kupitia Idara ya Uratibu wa shughuli za Serikali chini ya usimamizi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ndio iliyofanikisha vyema uandaaji wa Taarifa ya SMZ ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM  kwa Mwaka 2015 – 2017.

Alisema Chama cha Mapinduzi kupitia Mkutano wake Maalum  uliofanyika hivi karibuni Mjini Dodoma  chini ya Mwenyekiti wake Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli umeridhia Taarifa hiyo.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo alipokuwa akiwasilisha salamu rasmi kutoka kwa Uongozi wa Chama cha Mapinduzi  wakati  akizungumza na Uongozi wa  Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Alisema jukumu la utekelezaji wa Ilani ya Chama kilichoshika Madaraka hutekelezwa na Watendaji wote wa Umma wakielewa kwamba kazi iliyo mbele yao kwa sasa  ni kufuatilia utekelezaji wa Ilani kuanzia hatua kwa hatua ili ifikapo Mwaka 2020 iwe rahisi kuwasilisha Utekelezaji huo kwa Mwaka 2017 – 2020.

Balozi Seif  aliwahimiza Viongozi wa Taasisi za Umma kutoa  kipaumbele umuhimu wa kuwa karibu na vyombo vya Habari kwa lengo la kuelezea vyema utendaji wa Taasisi zao katika kila kipindi ili Wananchi walio wengi wafahamu kinachoendelea ndani ya Taasisi hizo.

Aliutaka  Uongozi wa kila Taasisi kuandika Taarifa ya ilichokifanya katika kipindi cha Mwaka 2016/2017 na baadae ijumuishwe pamoja ndani ya Uongozi  mzima wa Wizara ili iwasilishwe kwa Wananchi kupitia vyombo vya Habari.

Akizungumzia maadhimisho ya kusherehekea Miaka 54 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar Balozi Seif  ambae pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa alisema Sherehe za Mwaka huu zimekwenda sambamba na muda uliopangwa jambo ambalo Wazanzibari wanastahiki kujipongeza wenyewe.

Alisema ipo haja kwa Uongozi wa Sekriterieti ya Halmashauri ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa kufanya tathmini ya kina kuangalia mafanikio hayo na baadae kupendekeza   mambo yatakayoweza kusaidia zaidi kunogesha sherehe za Mapinduzi katika Miaka mengine ya mbele  ijayo.

Aliupongeza Uongozi wa Halmashauri ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar sambamba na Taasisi nyengine za Umma na zile Binafsi kwa kuratibu  vyema zoezi zima la sherehe za Mapinduzi kutimia Miaka  54.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Uongozi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Taasisi zake Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mheshimiwa Mihayo Juma N’hunga alisema bado Wananchi walio wengi wanafurahia kuona Maadhimisho ya  ya sherehe za Mapinduzi yanazingatia Historia yake.

Mh. N’hunga alisema  yapo mambo ambayo Wananchi hupendelea kuyaona wakati wa Kilele cha Maadhimisho  ya sherehe za Mapinduzi  yakiwakumbusha  sababu nyingi zilizopelekea kufanyika kwa Mapinduzi hayo ya Zanzibar ya Mwaka 1964.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimueleza Balozi Seif  kwamba pongezi alizozitoa  katika mafanikio ya sherehe za Mapinduzi Mwaka huu zitawafikia Wananchi pamoja na Watendaji wote wa Taasisi za Umma na zile za kiraia kupitia Viongozi wao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.