Habari za Punde

Kongamano la mabaharia

Waziri wa Habari ,Utalii,Utamaduni na Michezo Mhe. Rashid Ali Juma kwa niaba ya Makamu wa Pili wa Rais Mhe.Balozi Seif Ali Iddi akifungua kongamano la kwanza la kihistoria la mabaharia huko ukumbi wa Baraza la Wawakilshi la Zamani
Baadhi ya wanachama wa chama cha Mabaharia wakimsikiliza Waziri wa Habari Utalii,Utamaduni na Michezo kwa niaba ya Makamu wa pili wa Rais katika ufunguzi wa kongamano la kwanza la Mbaharia huko katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la Zamani (Picha na Kijakazi Abdalla Maelezo)

Na Kijakazi Abdalla. - Maelezo, Zanzibar.
MAKAMU wa pili wa Rais Mhe. Balozi Seif Ali Iddi amesema Serikali itasimamia ipasavyo haki za mabaharia ili kuwawezesha kufanya kazi zao kwa uzalendo na kupata mafanikio zaidi.

Akifungua kongamano la kwanza la kihistoria huko katika ukumbi zamani wa baraza la Wawakilishi kwa niaba ya Makamu wa pili Waziri wa Habari, Utalii,Utamaduni na Michezo Mhe.Rashid Ali Juma amesema serikali inatambua umuhimu wa mabaharia katika kukuza uchumi wa Nchi kutokana na jitihada zao.

Alisema kuwa atahakikisha mabaharia wanaekewa mazingira mazuri ambayo yatawezesha kukuza ajira ili kuwawezesha wazanzibari kunufaika na kupunguza tatizo la umasikini

Aidha Mhe. Rashid alisema serikali itachukuwa jitihada mbalimbali za kuimarisha mazingira bora ya mabaharia yatakayosaidia ukuaji wa kazi ya uchumi na kurekebisha kasoro zilizopo katika sekta hiyo ili iweze kuwa na uchumi ambao utaweza kushinda katika soko huria la kimataifa.

Hata hivyo alisema Serikali itafuatilia na kuzingatia utaratibu wa kuweka kima cha chini cha mshahara kwa mabaharia ili kuendana na mkataba wa kazi wa kimataifa kwa mabaharia.

Vilevile  aliwaomba wamiliki wa meli nchini kuhakikisha wanatoa mikataba ya ajira zote za mabaharia melini na kufuatilia maslahi pamoja na suala zima la mishahara .
Aidha aliwataka mabaharia hao kufanya kazi kwa mashirikiano ili lengo la kuwepo  kwa uwezo wa kuleta maendeleo ya haraka ili kupiga vita vitendo ambavyo vyenye kuvunja umoja wao.

Sambamba na hayo alisema kuwa katika suala la ushirikishwaji wa mabaharia katika utoaji wa maamuzi yanayohusu sekta ya bahari lina umuhimu ambao una uwezo wa kuongeza uwajibikaji na utaweza kutoa maamuzi katika masuala yote yanayohusu mabaharia.

Akisoma risala Katibu wa Chama cha Mabaharia Yahaya Alawi ameiomba Serikali kupatiwa ufumbuzi wa matatizo yanayowakabili ikiwemo kupatiwa ajira katika meli zilizosajiliwa na serikali pamoja na kurekebishwa kwa sheria iliyopo ili kuweza kupata haki zao.

Aidha aliitaka Serikali kuwapa kipa umbele katika sula zima la uchimbaji na  utafutaji wa mafuta pamoja na gesi baharini  kwa vile vijana wengi wamekuwa na ujuzi katika sula zima la kazi hizo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.