Habari za Punde

Mawakala wa Forodha na Wafanyabiashara Watakiwa Kwenda na Mabadiliko ya Kimataifa Katika Biashara Zao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi Dkt. Burhan Othman Simai akifungua mkutano wa siku moja wa Mawakala wa Forodha na Wafanayabiashara wa mbali mbali katika Ukumbi wa Kitengo cha Afya ya uzazi wa Mpango Kidongochekundu Zanzibar.
Baadhi  ya washiriki wa mkutano wa Mwakala wa Forodha na wafanyabiashara  wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji alipokuwa akifungua mkutano huo katika ukumbi wa Kitengo cha Afya ya uzazi wa Mpango Kidongochekundu Mjini Zanzibar.
Afisa wa Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi  Nd. Abrahaman Hassan Mussa akieleza utaratibu wa Uingizaji wa Bidhaa za Chakula Dawa na vifaa Tiba katika mkutano  wakala wa Forodha na wafanyabiashara uliofanyika Kitengo cha Afya ya uzazi wa Mpango Kidongochekundu Mjini Zanzibar.
Mwenyekiti wa Mawakala wa Forodha Omar Hussein Mussa akitoa mchango wa mawakala na wafanyabiashara katika mkutano uliowashirikisha wadau wa sekta hiyo katika ukumbi wa Kitengo cha Afya ya uzazi wa Mpango Kidongochekundu Mjini Zanzibar.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi Dkt. Khamis Ali Omar akifunga mkutao wa Mawakala wa Forodha  na Wafanyabiashara uliofanyika Kidongochekundu Mjini Zanzibar.(Picha Abdalla Omar Maelezo Zanzibar)

Na Ramadhani Ali – Maelezo Zanzibar.                                                                                
Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi Dkt. Burhan Othman Simai amesema kutoakana na mabadiliko ya mfumo wa biashara Duniani waagiziaji  na wasafirishaji bidhaa Zanzibar wanapaswa kubadilika na kufanya kazi hiyo  kwa mujibu wa Sheria zinazotumika za kimataifa na kikanda.
Dkt. Burhan ametoa ushauri huo alipokuwa akifungua mkutano wa siku moja wa wa wafanyabiashara wa bidhaa za chakula,dawa , vipodozi na vifaa tiba kupitia vituo vya Forodha uliofanyika ofisi ya kitengo cha afya ya uzazi wa mpango  Kidongochekundu.
Alisema idadi kubwa ya wafanyabiashara wa Zanzibar wamekuwa na tabia ya  wakisafirisha bidhaa  kienyeji bila ya kufuata taratibu kwa kuwa na vibali halali vinavyowaruhusu kufanya biashara hiyo.
“Fanyeni biashara zenu kwa mujibu wa mikataba na  miongozo ya kikanda na Kimataifa kwa usalama wa biashara zenu, ” Dkt. Burhan aliwashauri.
Aliwataka  kujenga ushirikiano wa karibu na Ofisi ya Wakala wa  Chakula Dawa na Vipodozi ili kuhakikisha wanajiepusha na matatizo yanayoweza kutokea na kuingia hasara isiyokuwa ya lazima.
 Alisema Ofisi ya Wakala wa Chakula, Dawa na vipodozi  hivi sasa imeimarisha  udhibiti wa uingizaji na usafirishaji bidhaa kwa lengo la kulinda afya za wananchi.
“Serikali imetupa dhamana ya kulinda afya za wananchi hivyo bidhaa mbovu , zilizpitwa na wakati na zisizokidhi viwango haturuhusu kuingia  Zanzibar, ” alisisitiza Mkurugenzi Mtendaji.
Aliwaeleza wafanyabiashara hao kuwa mwaka uliopita walifanya mchakato wa kubadilisha sheria na kuweka sheria mpya No 3 ya mwaka 2017 ambayo Imeweka misingi ya kuhakikisha  Zanzibar haigeuzwi kuwa jaa la bidhaa mbovu.
Akitoa muhtasari wa kazi za Wakala wa Chakula Dawa na Vipodozi Ndugu Abrahaman Hassan alisema ni asilimia 10 tu ya wafanyabiashara wa Zanzibar wanaofuata taratibu za uingizaji na usafirishaji wa bidhaa Zanzibar.
Alisema kutokana na kasoro hiyo kiasi cha tani 2424.3 za bidhaa mbali mbali zilizoharibika zimeangamizwa na Ofisi hiyo na zaidi ya tani 2824 za bidhaa zilizopitwa na wakati zimerejeshwa zilikotoka na kusababisha hasara kwa wafanyabiashara na kuharibu mazingira wakati wa kuangamizwa.
Kwa upande wao wafanyabiashara hao waliishauri Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi wanapoandaa sheria na taratibu mpya kuwashirikisha wadau wake ili kuifanya iwe rahisi kutekelezeka.
Walisema kutokana na sheria nyingi za biashara zilizowekwa  katika bandari ya Zanzibar, baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wameanza kuhamisha biashara zao na kuzipeleka nchi jirani jambo ambalo ni hasara kwa Zanzibar ambayo inategemea sekta ya biashara katika pato lake.
Mkutano huo ulihudhuriwa na wafanyabiashara wa maduka ya dawa, mawakala wa uingizaji na usafirishaji bidhaa bandarini, maafisa wa Forodha na Maafisa wa Mamlaka  ya Mapato Tanzania.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.