Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, wakimsikiliza Kamishna Mkuu wa Idara ya Uhamiaji Tanzania Dk. Anna Peter Makakala, akitowa maelezo ya Ubora wa Pasipoti hizi mpya zilizotengenezwa kwa utaalamu wa Kieletronikia, Uzinduzi huo umefanyika katika viwanja vya Makao Makuu ya Uhamiaji Kurasini Jijini Dar es Salaam leo, jumatano 31-1-2018.
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dk. John Pombe Joseph Magufuli leo amezindua Pasipoti mpya ya Tanzania
ya Kielektroniki inayoenda sambamba na Mfumo wa Uhamiaji Mtandao na kuipongeza
Idara ya Uhamiaji kwa kwenda na wakati pamoja na kuonesha uzalendo katika
utendaji kazi wao.
Rais
Magufuli aliyasema hayo katika uzinduzi huo uliofanyika katika Makao Makuu ya
Ofisi za Uhamiaji Tanzania yaliopo Kurasini, jijini Dar-es-Salaam ambapo
viongozi mbali mbali walihudhuria akiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, Makamo wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine wa Serikali zote
mbili.
Katika
maelezo yake, Rais Magufuli alieleza kuwa Pasipoti mpya ni haki ya kila
Mtanzania hivyo ni vyema kuitumia fursa hiyo waliyoipata Watanzania na
kuipongeza Idara ya Uhamiaji Tanzania kwa kuonesha mabadiliko makubwa.
Kuendelea
kuchapa kazi, kubadilisha jina, kuwashughulikia wahamiaji wanaoingia Tanzania
na kuwasaka wahamiaji na kueleza jinsi anavyofarajika kuwaona Maafisa wa
Uhamiaji wanavyowashika Wahamiaji.
Alieleza
haja kwa kuchukua hatua kwa wakuu wa Uhamiaji ambao wahamiaji wamekuwa wakipita
kirahisi bila ya kuwakamata na kumtaka wahusika wasiotimiza wajibu wao
awashughulikie ikiwa ni pamoja na kuwapunguza hata vyeo.
Alisema
kuwa Idara yao ni nyeti na muhimu kwa usalama wa Tanzania huku akiwapongeza
sambamba na kuwataka kuzifanyia kazi changamoto zilizopo.
Aliwapongeza
kwa kazi nzuri wanazozifanya ikiwa ni pamoja na kutumia mfumo wa kiielektroniki
katika kukusanya mapato, wito wa serikali kuhamia Dodoma pamoja na mambo
mengine muhimu.
Alisema
kuwa Idara hiyo ni muhimu hasa katika ulinzi na usalama na maendeleo ya
kuiuchumi ya nchi ambayo Idara hiyo inaifanya kuwa ni nyeti na muhimu sana.
Alieleza
kuwa katika miaka ya karibuni Pasipoti ziligawiwa kiholela na kuwapa mianya
wahalifu na kuharibu taswira ya nchi na kufanya baadhi ya Watanzania kupata
tabu katika baadhi ya nchi.
Alieleza
kuwa kuna raia wengi wa kigeni walipata vibali vya ukaazi ambao si raia,
wengine hawana sifa, ukusanyaji wa mapato ya viza haukuridhisha na mengineyo
hatua ambayo iliifaya Idara hiyo ionekane haikuwa sawa na ndio alipoamua
kufanya mabadiliko na kumteua Dk. Makakala ambaye ameanza vizuri na kumtaka
kuyaondoa mapungufu.
Alimpongeza
Balozi wa Ireland Paul Shercockm kwa kusaidia kupatikana Kampuni ya kutengeneza
Pasipoti kwa kiwango kidogo cha fedha mbali na Kampuni za awali ambazo zilitaka
fedha nyingi.
Alieleza
kuwa fedha zote za mradi huo zimetolewa na Tanzania, na kusema kuwa bei ya sasa
imezingatia ukubwa na ubora wake ambayo itakuwa na kurasa nyingi na kueleza
haja ya kuikubali kutokana na kuimarishwa kwa usalama wa Pasipoti hiyo.
Aliwataka
Watanzania kuzilinda na kuzitunza Pasipoti mpya na kueleza kuwa anaimani kuwa
hakuna ujanja utakaofanyika katika Pasipoti hizo kama ilivyokuwa ikifanywa na baadhi
ya watu.
Pamoja na
hayo alieleza kuwa lengo nikutaka wananchi na wageni wanapewa huduma bora na
wasicheleweshwe na kueleza kuwa kutokana na kushirikishwa kwa kuwataka wadau
wengi katika mfumo huo kutasaidia kupata Pasipoti na huduma nyengine.
Rais
Magufuli aliahidi kutoa Bilioni 10 nyengine baada ya kuwapa nyumba 103 Idara
hiyo kwa ajili ya kujenga jengo zuri la Makao Makuu ya Idara hiyo mjini mjini
Dodoma na kumtaka Mkuu wa Idara hiyo kutafuta eneo kwa ajili ya ujenzin huo ikiwa
ni shukurani zake kwa Idara hiyo.
Alisisitiza
haja ya kuwepo kwa uadilifu na uaminifu kwa watumishi wa Idara hiyo na kueleza
kuwa kwa wale watumishi wachache wanaoendeleza rushwa katika Idara hiyo
kufanyiwa kazi na vyenginevyo wakigunduliwa wafukuzwe.
Dk.
Magufuli aliwahakikishia kuwa iwapo wataendelea na mwendo wao huo wa kubadilika
na changamoto zitabadilika na kuwataka kutembea kifua mbele na kuwataka wajue kuwa
wana jukumu kubwa katika nchi hii.
Pamoja na
hayo, Rais Magufuli aliwahakikishia wakaazi wa Dar-es-Salaam kuzitatua
changamoto walizonazo ikiwa ni kuimarisha miundombinu ya barabara, reli, huduma
za kijamii kama maji, afya, elimu na kuwataka wananchi waendelee kuiunga mkono
Serikali sambamba na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi Dk. Mwigulu Nchemba, alimpongeza Rais Magufuli kwa
kuipeleka Tanzania katika hatua moja muhimu na ya kihistoria na kuwa nchi moja
ya mfano kwa nchi za Afrika Mashariki na Kusini mwa Jangwa la Sahara pamoja na mambo mbali mbali aliyoanza
kuyafanya ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa kiasi
kikubwa.
Dk.
Nchemba alisema kuwa hatua hiyo ni muhimu sana katika mapambano ya uhalifu kwa
kutumia teknlolojia hiyo sambamba na kusaidia kufuta makosa yaliojitokeza hapo
siku za nyuma huku akisema kuwa gharama ya Pasipoti hiyo ni TZS 150,000 ambayo
itatumika kwa miaka kumi.
Nae
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dk. Anna Peter
Makakala, alieleza kuwa Uhamiaji Mtandao ni muunganiko wa Mifumo mbali
mbali ambayo imesanifiwa kufanya kazi kwa pamoja na kutoa taarifa kwa watumiaji
na wadau wa huduma za kiuhamiaji ambao mchakato wake ulianza mwaka 2013 na
kuanza tena 2017 mwezi Juni.
Alieleza
kuwa lengo kuu la Uhamiaji Mtandao ni kuimarisha Ulinzi na Usalama wananchi,
kudhibiti ukusanyaji wa maduhuli ya serikali na kuimarisha utoaji wa huduma za kiuhamiaji
kwa raia na wageni wanaoingia na kuishi hapa nchini kwa madhumuni mbali mbali.
Aliongeza
kuwa Mfumo wa Uhamiaji Mtandao utawezesha Idara ya Uhamiaji kutoa viza
kielektroniki (e-Visa) ambapo mgeni ataweza kuwasilisha ombi lake na kupata
majibu kwa njia ya kielektroniki, mfumo ambao utasaidia Serikali kupata taarifa
sahihi za malipo ya viza na hivyo kuchangia ukuaji wa sekta ya utalii nchini.
Dk. Makakala
alisema kuwa mfumo huo utasaidia udhibiti na usimamizi wa mipaka kielektroniki
ambao utasaidia kudhibiti na kuwezesha uingiaji na utokaji wa raia wa Tanzania na
wageni nchini sambamba na kuchuja wageni wasiotakiwa kuingia nchini, Pia
utasaidia kuimarisha usimamizi wa utoaji vibali.
Pamoja na
hayo alieleza kuwa mfumo huo ambao ndio wa kwanza katika utekelezaji wa Mradi
wa Uhamiaji Mtandao, utawezesha waombaji wa huduma ya Pasipoti kuwasilisha
maombi yao kwa njia ya kielektroniki kutoka mahali popote walipo na kuweza
kufuatilia maombi yao kielektroniki ambayo pia itakuwa imara.
Alitoa
pongezi kwa kupewa nyumba 103 za watumishi wa Idara hiyo na Rais Magufuli na
kueleza kuwa Idara yake imeanza kutekeleza Sera ya Uhamiaji, na kusisitiza kuwa kutokana na kuzinduliwa kwa
Pasipoti hizo mpya Pasipoti za Kawaida mwisho wake itakuwa ni Januari mwaka
2020 na baada ya hapo zitaondolewa katika matumizi na Pasipoti ya Afrika Mashariki haitotolewa
tena.
Sambamba
na hayo, alieleza kuwa Mradi huo unatekelezwa kwa awamu nne ambazo ni mfumo wa
pasipoti za kielektroniki, mfumo wa kielektroniki wa visa, mfumo wa kielektroniki
wa vibali vya ukaazi na pasi pamoja na mfumo wa kielektroniki wa usimamizi na
udhibiti wa mipaka.
Pia, alitoa shukurani kwa Rais kwa kutoa ajira 1510 kwa mwaka
2017 hadi 2018
Katika
hafla hiyo viongozi mbali mbali walikabidhiwa Pasipoti zao akiwemo Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, Makamo wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassa, Makamo wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Rais mstaafu wa Zanzibar Amani Abeid
Karume na baadhi ya viongozi wengineo huku ikielezwa kuwa kwa upande wa
viongozi wa Zanzibar zitaendelea kutolewa Zanzibar.
Balozi wa
Ireland Paul Shercock alitoa pongezi kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa kuanza Mradi huo ambao utaipelekea Tanzania kuimarika katika
uchumi wake na kuwa salama.
Mwakilishi
wa Kampuni ya HID Robert Haskan alieleza jinsi hatua zilizochukuliwa katika
kuhakikisha mfumo huo unaimarika na kuwa wa uhakika na ina sifa za pasi yenye
taarifa za kielektroniki sambamba na kupunguza muda na gharama.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment