Habari za Punde

Mke wa Rais wa Mama Mwanamwema Shein Azungumza na Umoja wa Wanawake wa Dubai.

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Dubai                                                                                                                    26.01.2018
---
MKE wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein amekutana na Umoja wa Wanawake wa Dubai (DWE), na kufanya nao mazungumzo ambapo Umoja huo umeahidi kuwaunga mkono akina Mama wa Zanzibar wakiwemo waliojiunga kwenye vikundi ili wazidi kupata maendeleo endelevu sambamba na kujikwamua kiuchumi.

Mama Shein alikutana na Umoja huo wa Wanawake wa Dubai (DWE), mjini Dubai ambao katika maelezo yake Mama Shein aliueleza Umoja huo mafanikio yaliofikiwa na wanawake wa Zanzibar pamoja na changamoto walizonazo.

Katika maelezo yake Mama Shein alisema kuwa juhudi za makusudi zimekuwa zikichukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha wanawake wanapata fursa katika kujiletea maendeleo yao.

Mama Shein alieleza kuwa chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein wanawake wameweza kupewa fursa nzuri katika uongozi Serikalini pamoja na kupewa vipaumbele kwenye masuala mbali mbali ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Alieleza kuwa Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT), kwa upande wake umekuwa ukitoa mashirikiano na kuwasaidia wanawake wenzao sambamba na kuwaunga mkono akina mama walioko mjini na vijijini kwa kuwasaidia katika miradi yao ya maendeleo kupitia vikundi vyao walivyoviunda.

Mama Shein alieleza kuwa kwa upande wa Zanzibar wanawake wengi ambao wameunda vikundi vyao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ikiwa ni pamoja na ukosefu wa mafunzo na utaalamu ambao utawasadia katika kuendeleza miradi yao.

Aidha, Mama Shein alieleza kuwa wanawake wa Zanzibar wamekuwa wakikabiliwa na ukosefu wa soko la kuuzia bidhaa zao wanazozitengeneza pamoja na ukosefu wa vifaa vya kutendea kazi zao katika vikundi vyao walivyoviunda.

Kutokana na Umoja huo kuonesha nia ya kuwasaidia wanawake wa Zanzibar, Mama Shein alieleza haja ya uongozi wa Jumuiya hiyo kuitembelea Zanzibar na kupata fursa ya kuvitembelea vikundi vya wanawake wa Zanzibar ili kujionea wenyewe mafanikio yaliofikiwa sambamba na changamoto wanazozikabili.

Sambamba na hayo, Mama Shein ameeleza haja ya kukuza uhusiano na ushirikiano kati ya Umoja huo na Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT), ikiwa ni pamoja na viongozi wake kutembeleana kwa lengo la kubadilishana uzoefu na utaalamu kati ya pande mbili hizo.

Nao Umoja wa Wanawake wa Dubai (DWE) ulimuahidi Mama Shein kuwa uko tayari kuwaunga mkono akina mama wa Zanzibar sambamba na kushirikiana nao kikamilifu huku ukisisitiza kuwa mara baada ya taratibu za kidiplomasia zitakapokamilika wako tayari kuitembelea Zanzibar kwa lengo la kukutana na akina mama wenzao.

Akina Mama hao walimueleza Mama Shein kuwa Umoja wao una fursa mbali mbali ambazo zinaweza kuwasaidia akina mama wa Zanzibar hasa wale ambao wamejiunga katika vikundi kutokanan na uzoefu na utaratibu walionao wa kuwasaidia katika Nyanja zote.

Walieleza kuwa Umoja wao pia umekuwa ukitoa  fursa mbali mbali ikiwa ni pamoja na ufadhili wa masomo, misaaada ya kifedha na kitaalamu pamoja na vifaa jambo ambalo wako tayari kulifanya kwa akina Mama wa Zanzibar kwani wamevutika na juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa jinsi inavyowaunga mkono wanawake.

Aidha, akina mama hao wa Umoja wa Wanawake wa Dubei (DWE), ambao uko chini ya kiongozi wake Mke wa Mtawala wa Dubai Mama Sheikha Manal Bint Mohammed Bin Rashid Al Maktoum, uliahidi kukuza ushirikiano wake na uhusiano wa karibu uliopo kati ya pande mbili hizo.

Sambamba na hayo, uongozi wa Umoja huo nchini Dubai ulitumiafursa hiyo kumpongeza Mama Shein kwa kuwatembelea pamoja na kupata kujua shughuli zao na kueleza kuwa hatua hiyo ya Mama Shein inaonesha wazi jinsi anavyowajali, anavyowasamini na kuwapenda akina mama wenziwe ambao na wao kwa uoande wao wamemuhakikishia kuwa wataendelea kumpenda na kumthamini na kumuweka katika kumbukumbu zao.

Umoja huo umeundwa mwaka 2006 chini ya Sheria Namba 26 na kutangwazwa rasmi mnamo mwaka 2008, kupitia Mtawala wa Dubai  Sheikh Mohammed Bin Rashid Al Maktom.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.