Habari za Punde

Mkuu wa zamani wa TBC Tido Mhando afikishwa mahakamani Dar es Salaam



Aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Tanzania TBC, Tido Mhando amefikishwa mahakamani leo jijini Dar es Salaam kwa mashtaka ya matumizi mabaya ya Madaraka.

Tido Mhando, ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Azam Media alifikishwa katika mahakama ya Kisutu mapema leo Ijumaa, na kusomewa dhidi mashtaka yake.

Wakili wa Taasisi ya Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) Leonard Swai aliambia hakimu mkazi mkuu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Victoria Nongwa kuwa Mhando anatuhumiwa kwa mashtaka matano.

Anadaiwa kutenda makosa hayo mwaka 2008 alipokuwa Mkurugenzi Mkuu wa TBC.

Anatuhumiwa kwa matumizi mabaya ya madaraka, wakati alipokuwa akilitumikia shirika hilo la Utangazaji la Serikali TBC, pamoja na kulitia hasara ya shilingi 897 milioni za Tanzania.

Amekana mashtaka yote na kuachiwa kwa dhamana.

Kesi imeahirishwa hadi Februari 23, 2018 kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali.

Sheria nchini Tanzania haiwaruhusu washtakiwa, mawakili au watu wengine kuzungumzia kesi nje ya mahakama.

Mhando ni miongoni mwa waandishi wa habari na watangazaji wakongwe wa Tanzania.
Aliwahi kufanya kazi Shirika la Utangazaji Uingereza (BBC) kama Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili kabla ya kuwa Mkurugenzi Mkuu wa TBC.

Pia amewahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) inayochapisha magazeti ya Mwananchi, Mwanspoti na The Citizen.

Aliwahi pia kufanyia kasi Sauti ya Ujerumani (Deutsche Welle), Sauti ya Amerika, na Shirika la Utangazaji la Kenya (KBC) lilipokuwa linafahamika kama Sauti ya Kenya (VoK).

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.