Habari za Punde

Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar awataka wananchi kuchangia damu kwa hiari

 NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Zanzibar, Dk. Abdulla Juma Mabodi akizungumza katika tamasha la uchangiaji wa damu iliyoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mjini na Magharib, katika Mnara wa Kumbukumbu ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar ulioko Kisonge,
 BAADHI ya wananchi walioshiriki tamasha  la uchangiaji damu wakifuatilia matukio mbalimbali yanayoendelea kwenye maeneo ya Kumbukumbu ya Mnara wa miaka 50 ya  Mapinduzi ya Zanzibar ulioko Kisonge.  

BAADHI ya waandaji wa tamasha la uchangiaji damu kutoka Jumuiya ya Maendeleo ya Wanawake na Vijana.
 KATIBU Msaidizi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), MKoa wa Magharibi Suleiman Mzee Suleiman akichangia damu katika tamasha hilo la uchangiaji damu



NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Zanzibar Dk.Abdalla Juma Saadalla ‘Mabodi’ amewataka wananchi wa visiwani humu bila ya kujali tofauti zao za kisiasa, kidini na kikabila kuwa na utamaduni wa kuchangia damu kwa hiari ili kuokoa maisha ya wenzao  husasan wanaopata ajali na akina mama wajawazito wakati wa kujifungua.

Wito huo umetolewa jana katika tamasha la uchangiaji wa damu salama lililofanyika katika Mnara wa Kumbukumbu ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar ulioko Kisonge, ambapo alisema mahitaji ya damu ni ya kila siku na kwamba kuna haja ya wananchi kuwa na uzalendo wa kujitolea kwa ajili ya maisha ya wengine.

Naibu huyo Katibu Mkuu alifafanua kuwa nchi zilizoendelea na zinazoendelea zimekuwa na viwanda vya kutengeneza bidhaa mbalimbali ikiwemo vifaa tiba vya hospitalini, lakini wameshindwa kutengeneza damu ya binadamu kwa ajili ya matumizi ya kitiba

Pia, alisisitiza kuwa lazima wananchi watambue kuwa benki ya damu ni wao wenyewe na hakuna kampuni wala kiwanda kinachoweza kuzalisha damu hiyo.

“Wananchi sisi wenyewe ndio wenye jukumu la kuzalisha damu kwa ajili ya kuiweka katika benki ya damu ili itumike kwa ajili ya mtu yeyote anayehitaji huduma hiyo tena kwa wakati,” alisema Dk.Mabodi.

Akizungumzia faida ya utoaji wa damu kitaalamu alisema kuwa mtu anapotoa damu anapunguza vichocheo vya hasira pia damu inapotoka mwilini inatoa fursa ya kutengeneza damu nyingine mpya inayokuwa na uwezo mkubwa wa kiutendaji katika mzunguko wa damu mwilini.

Hata hivyo, alisema kwamba matukio ya ajali za aina mbalimbali pindi yanapotokea huku wa kina mama wajawazito wanaojifungua wanahitaji damu hiyo na kwamba lazima utamaduni wa kutoa damu upewe kipaumbele.

Naye Ofisa Uhamasishaji kutoka Mpango wa Damu   salama Zanzibar, Omar Said Omar amezipongeza taasisi   zilizoandaa tamasha hilo la kuchangia damu na kwamba  litasaidia kupunguza vifo vinavyotokana na ukosefu wa damu.

 Alisema matarajio ya kitengo hicho ni kupata zaidi ya chupa za damu 1,000 ambazo kwa matumizi yake chupa moja utumika kwa watu watatu ambao wanaohitaji huduma za kimatibabu.

Wakizungumza kwa wakati tofauti baadhi ya wananchi, askari wa majeshi ya ulinzi na Idara maalum za SMZ pamoja na wananchi walioshiriki kuchangia damu  waliahidi kuwa mabalozi wazuri wa kuwahamasisha wananchi wengine kujitokeza kuchangia damu.
Kwa upande wake Koplo Suleiman Ali kutoka kituo cha Jeshi la Polisi la Ng’ambo, aliwashauri askari wwenzake  kuwa mstari wa mbele katika kuchangia damu kwa lengo la kuunga mkono kampeni za uchangiaji wa damu.

Naye Nassor Othman Mkaazi wa Kisauni Unguja, alieleza kuwa amekuwa ni mdau wa kuchangia damu kwa miaka Sita na wakati mmoja kati ya familia yake wanapohitaji damu wanapata huduma hiyo bila tatizo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.