Habari za Punde

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’ ametuma salamu za rambi rambi kwa familia ya mtumishi wa Chama hicho Zanzibar Marehemu Bi. Nakia Khamis Abdalla aliyefariki leo Januari 25,2018.

Bi. Nakia amefariki dunia akiwa nyumbani kwake mtaa wa Sogea Zanzibar baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Katika Salamu zake  Dk. Mabodi amesema  CCM Zanzibar  imepokea taarifa ya kifo cha mtumishi huyo  kwa Mshutuko, Majonzi na Simanzi kubwa, kwani Marehemu enzi za uhai wake alikuwa Mwadilifu aliyefanya kazi kwa bidii na ubunifu wa hali ya juu katika utumishi wake.

Pamoja na hayo alitoa pole kwa familia Wanachama, Viongozi na Watendaji Wote wa CCM, Marafiki pamoja na Jamaa wa karibu walioguswa na msiba huo, na   kuwaomba waendelee kuwa na uvumilivu katika kipindi chote cha msiba huo.

“ Marehemu alikuwa ni mfano wa kuigwa enzi za uhai wake hasa kwa kujitolea na kukipigania Chama cha Mapinduzi muda wote wa uhai wake, hivyo  tumepoteza mtu muhimu sana ndani ya Chama na Taifa kwa ujumla.

Pia nawaomba watumishi na wanachama na Familia ya Marehemu kuwa na Subra katika kipindi hiki kigumu cha Msiba huo, na tuendelee kumuombea dua mwenzetu ili Mwenyezi Mungu amuweke pahala pema peponi Amin.”, alieleza Dk. Mabodi.

Marehemu Bi. Nakia Khamis Abdalla amefariki leo Tarehe 25/1/2018 Nyumbani kwake Mtaa wa Sogea Zanzibar baada ya kusumbuliwa na maradhi kwa muda mrefu, amezaliwa Januari 6,1965 katika Kijiji cha Ndagaa Wilaya ya Kati Unguja.

Alipata elimu yake ya Sekondari ya Kidato cha Tatu katika Shule ya Ben-Bella Mjini Zanzibar.

Enzi za uhai wake Marehemu Bi. Nakia amehudumu katika Afisi Kuu ya CCM Zanzibar kwa  nafasi mbali mbali zikiwemo Ukarani wa Simu (Telephone Operator), Ulinzi pamoja na nyinginezo.

Marehemu ameolewa na ameacha Mume na Watoto Wawili. Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu pahala Pema Peponi Amin.
                                             Imetolewa.
“KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI’’
Mohamed Sijamini Mohamed
Kny: Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar.
ZANZIBAR.
25 Januari, 2018.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.