Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akifungua Mkutano wa Warsha ya Kutoa Uelewa Juu ya Mamlaka Itakayosimamia Viwanda Vidogo vidogo na Vya Kati,(SMIDA) iliofanyika katika kumbi wa Zamani wa Baraza la Wawakilishi Kikwajuni Zanzibar,ilioandaliwa na Wizara ya Biashara Viwanda na Masoko Zanzibar.
SERIAKLI ya Mapinduzi ya Zanzibar
imeamua kuanzisha Taasisi ya Wakala wa Serikali wa Kusimamia Maendeleo ya
Viwanda vidogo vidogo na vya kati, Zanzibar (SMIDA) ili sekta ya viwanda iweze
kuimarika, kusimamiwa kwa karibu pamoja na kusaidiwa kwa lengo la kuvilea
viwanda hivyo.
Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema hayo leo
katika uzinduzi wa Warsha ya Utambulisho wa Wakala wa Serikali wa Kusimamia
Maendeleo ya Viwanda vidogo vidogo na vya kati (SMIDA), hafla iliyofanyika
katika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi, Kikwajuni Mjini Unguja.
Katika
maelezo yake, Dk. Shein alisema kuwa mifano ya Taasisi kama hiyo ipo mingi
katika nchi mbali mbali ambapo kwa upande wa Tanzania Bara lipo Shirika la
Maendeleo ya Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO), India kuna Shirika la Taifa la
Viwanda Vidogo Vidogo la India, na Mauritius lipo (SMIDA), kama iliyo kwa
Zanzibar.
Alieleza
kuwa katika nchi nyengine zipo taasisi mahsusi zilizoanzishwa kwa lengo
lamkusaidia na kusimamia uanzishwaji na maendeleo ya miradi midogo midogo ya
Wajasiriamali kama vile nchini Kenya, Pakistani, Malaysia na Bangladesh.
Hivyo,
Dk. Sheijn alieleza kuwa itakuwa ni fursa muhimu ya kujifunza mikakati ya
mafanikio yao na kutambua changamoto zilizowakabili kuweza kubuni mbinu nzuri
za kukabiliana na changamotio za aina hiyo.
Dk. Shein
alitoa wito kuitumia vyema fursa hiyo na nyenginezo kwa kujifunza kutoka nchi
mbali mbali kama hizo ili malengo ya Serikali ya kuanzisha Mamlaka hiyo yaweze
kufikiwa na kuleta manufaa yaliyokusudiwa.
Aliongeza
kuwa katika awamu mbalimbali za uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,
Zanzibar imekuwa ikiandaa mipango na kutekeleza mikakati ya kuimarisha sekta ya
viwanda kwa kutambua umuhimu wake na kusisitiza kuwa Sekta ya viwanda ina umuhimu
wake katika kuchangia uchumi, kuimarisha sekta nyengine za uzalishaji na
biashara, kuimarisha upatikanaji wa bidhaa mbali mbali na kutoa fursa kubwa ya
ajira kwa wananchi.
Alieleza
kuwa mchango wa sekta ya viwanda umeendelea kuimarika nchini na kuchangia pato
la Taifa kutoka TZS bilioni 417.0 mwaka 2015 na kufikia TZS bilioni 487.9 mwaka
2016 ambapo mchango huo umefikia asilimia 18.6 mwaka 2016 kutoka asilimia 18.1
mwaka 2015 katikajumlaya pato la Taifa.
Dk. Shein
alieleza kuwa mchango huo umeimarika zaidi kufuatia kufanya kazi kwa viwanda
vya maji ya chupa, kiwanda cha Azam na kiwanda cha Sukari cha Mahonda ambapo
kwa mujibu wa Dk. Shein Serikali kupitia Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi
(ZIPA) imeshaidhinisha ujenzi wa viwanda vipya vitano katika eneo la Viwanda
Vidogo Vidogo Amani na maeneo ya Maruhubi.
Aidha,
Dk. Shein alieleza kuwa kuanzishwa na kufanya kazi ipasavyo kwa Wakala wa
Serikali wa Kusimamia Maendeleo ya Viwanda uliozinduliwa leo kutapunguza kwa
kiasi kikubwa changamoto zinazoikabili sekta ya biashara kwani miongoni mwa
majukumu yake ni kutoa mafunzo kwa wenye nia ya kuanzisha miradi ya uzalishaji
mali na wale ambao tayari wanayo miradi ya aina hiyo.
Kutokana
na hilo, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwataka Wakuu wote wa Wilaya Zanzibar
kuhakikisha kila Wilaya inakuwa na kiwanda na kutokana na uzoefu wao wa kazi alisisitiza
kuwa ana uhakika hilo linawezekana.
Dk. Shein
alieleza kuwa Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2015-2020 imezielekeza
Serikali zake mbili kuelekea katika uchumi wa Viwanda, ili iwe ni ukombozi
halisi wa kuwapatia fursa zaidi za ajira vijana.
Pia, Dk.
Shein alieleza jinsi alivyolizungumizia suala zima la ajira katika ziara yake
aliyoifanya wiki iliyopita, kuanzia tarehe 20 hai 27 katika Umoja wa nchi za
Falme ya Kiarabu (UAE) wakati alipokutana na viongozi wa Umoja huo akiwemo
Mtawala wa Abu Dhabi, Sheikh Muhammed bin Zayed Al Nahyan.
Nae
Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Balozi Amina Salum Ali alieleza kuwa
Wizara yake katika kumaliza Mpango wa Zanzibar kukuza Uchumi (MKUZA) na katika
kujipanga na mpango mpya wa uchumi wa mwaka 2010 imejipanga kutekeleza mkakati
wa kuendeleza viwanda kwa kupitia upya sera ya Viwanda na kuja na Sera mpya na
Sheria itakayowezesha kwenda kwa kasi mpya katika kujenga viwanda
vitakavyoongeza ajira.
Aliongeza
kuwa Sekta zote zinaendelea kufanyiwa tathmini ili kuona zitawezaje kuwezesha
viwanda vihamie Zanzibar na kutoa mchango mkubwa na kusisitiza kuwa Zanzibar ya viwanda
inawezekana.
Balozi
Amina alieleza kuwa Awamu hii ya Saba, Serikali imefanya mapitio ya Sera ya
Ujasiriamali na kupendekeza uanzishaji wa wakala wa Serikali wa kusimamia
viwanda, ambao madhumuni yake makubwa ni kujenga viwanda vya msingi
vitakavyoweza kuchangia viwanda vikubwa ambavyo vitaendeshwa ili kuongeza
ukuaji wa sekta zote za uchumi ikiwemo utalii, kilimo, uvuvi, bahari, madawa,
teknoloji, mafuta na gesi asilia.
Sambamba
na hayo, Waziri huyo alichukua nafasi hiyo kutoa taarifa rasmi kuwa Sheria ya
Wakala imeshakuwa inafanya kazi baada ya Rais kuitia saini na bajeti ya
uanzishwaji kwa fedha za SMZ zimetengwa huku akieleza kuwa tayari Wizara
imeshaona eneo la kuanzia makao makuu na kuiomba Serikali kuwapatia.
Mapema,
Kaibu Mkuu wa Wizara hiyo Juma Ali Juma alieleza kuwa Wakala hiyo inatarajiwa
kutoa fursa kubwa sana kwa wajasiriamali wa hapa nchini katika kuimarisha
uzalishaji wa bidhaa zao kwa kutumia viwanda.
Alieleza
kuwa kutokana na wingi wa vijana wanaomaliza masomo kila mwaka katika ngazi
mbali mbali, suala la kuajiriwa wote Serikalini limekuwa changamoto kubwa na
ndio maana Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikatilia mkazo suala la
uanzishwaji wa Mifuko ya Uanzishaji wananchi kiuchumi na sasa suala la uanzishaji
wa viwanda vidogo, vidogo na vya kati ili kutoa fursa ya ajira.
Alisema
kuwa suala hilo na uazishaji wa viwanda bado halijafahamika vizuri wananchi wengi na hasa vijana hawana uwelewa
wataanza vipi uzalishaji wa viwanda, bidhaa gani zinaweza kuzalishwa nchini
kutokana na rasiliamali zilizopo, ubora sambamba na uwelewa wa soko.
Hivyo,
Katibu Mkuu huyo, alisisitiza kuwa Warsha hiyo aliyoifungua Rais madhumini yake
ni kutoa uelewa kwa wananchi pamoja na lengo la kuwataka kuelewa kuwa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshatenga Sheria na tayari imeshaanza kufanya kazi
hivyo wakae mkao wa kula kwa kunufaika na malengo yaliokusudiwa.
Alieleza
kuwa wanakusudia kutoa uelewa katika ngazi ya Taifa ambapo leo hii wamezindua
rasmi hadi ngazi za Serikali za Mitaa ambako ndiko waliko wananchi wengi na
ndiko ambako kutaanzishwa maeneo ya uzalishaji wa viwanda.
Sambamba
na hayo, Katibu Mkuu huyo alieleza matumaini makubwa ya kushirikiana na Shirika
la Maendeleo ya Viwanda, Tanzania (SIDO) ambao wana uzoefu mkubwa katika
kuendeleza viwanda vidogo vidogo Tanzania.
Nae
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Viwanda Tanzania (SIDO), Inginia
Profesa Sylvester Mpanduji alitoa pongezi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
kwa kuanzisha Wakala wa Serrikali wa Kusimamia Maendeleo ya Viwanda Vidogo
Vidogo na vya kati (SMIDA) huku akiwataka Watanzania kuzitumia bidhaa za hapa
nchini.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment