Habari za Punde

Balozi Seif: Serikali haitovumilia miradi isiyopata baraka za serikali

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kati kati akiongozwa na Mwakilishi wa Jimbo la Kijini Mh. Juma Makungu Juma  wa kwanza mbele Kushoto kukagua Hoteli ya Sun Rise iliyopo Matemwe Mbuyu Tende inayokusudia kutaka kujenga Kituo cha Upigaji Mbizi { Diving} katika Mwambao wa Matemwe.
Nyuma ya Mh. Juma Makungu Juma ni Mkuu wa Mkoa Kaskazini Unaguja Mh. Vuai Mwinyi na wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Sun Rise Bwana Hussein Munnawar Mohamed.
 Balozi Seif aliyevaa Suti Nyeusi na Kukaa kitini kati kati akimsikiliza  kwa makini Mkurugenzi Uwezeshaji na Miradi ya Maendeleo wa Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar {ZIPA} Nd. Sharif  Ali Sharif akielezea utaratibu wa Muwekezaji anavyotakiwa kuufuata kabla na baada ya kuanzisha mradi wake.
Diwani wa Wadi ya Mwatemwe Ndugu Hassan Mcha Hassan kushoto aliyesimama akiwasilisha salamu za faraja za Wananchi wa Wadi yake kutokana na jitihada za Muwekezaji wa Hoteli ya Sun Rise kuwaunga mkono katika kuwawekeza miundombinu inayorahisisha miradi yao ya Maendeleo na ustawi wa Jamii.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema ushirikishwaji wa Wananchi katika Miradi ya Kiuchumi inayowekezwa  kwenye maeneo yao ndio njia pekee inayosababisha utulivu na kudumu kwa muda mrefu uendeshaji wa miradi inayoanzishwa.
Alisema kinyume na utaratibu huo ambao unastahiki kuendelea kusimamiwa na Taasisi zinazotoa Vibali kwa ajili ya kuendelezwa kwa Miradi ya Kiuchumi, sintofahamu na migogoro isiyokwisha huvukuta baina ya Wananchi na Wawekezaji na hatimae hukosekana usuluhishi.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo baada ya kufanya ziara fupi ya kuangalia eneo linalotarajiwa kutaka kuanzishwa kwa Ujenzi wa Mradi wa Kituo cha Upigaji Mbizi {Diving} katika mwambao wa Matembwe unaosimamiwa na Uongozi wa Hoteli ya Sun Rise.
Alisema ipo baadhi ya miradi ya Uwekezaji inayopata baraka zote za Serikali katika uanzishwaji wake kupitia Taasisi husika lakini kinachojichomoza baadae ni kufifia kwa Miradi hiyo kunakotokana na ujanja wa baadhi ya Watu kutia mikono yao kwa kutaka kuendeleza Ubinafsi.
Balozi Seif alisema tabia hiyo kamwe haitoendelea kuvumiliwa na Serikali Kuu kwani lengo la kuweka milango wazi ya kuanzishwa kwa Miradi ya Kiuchumi ni kuwapa fursa za kupata ajira Wananchi wake ili kuongeza kipato chao na kupunguza umaskini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuagiza Uongozi wa Hoteli ya Sun Rise kusubiri maamuzi ya Serikali Kuu kuhusu uanzishwaji wa Mradi wao wa Kituo cha Upigaji  Mbizi Matemwe ili kutafakari mawazo ya baadhi ya Taasisi.
“ Serikali itakaa tena kuangalia Mradi wa Diving Centre Matemwe huku Muwekezaji wa Mradi huo akalazimika kufanya subra ili kutoa fursa ya kutafakari mawazo ya baadhi ya Taasisi ambapo uamuzi utakaotolewa ulete mafanikio kwa pande zote husika ”. Alisema Balozi Seif.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar isingependa kuona mradi huo muhimu kwa kuchochea Sekta ya Utalii Zanzibar unakumbwa na changamoto zinazoweza kuepukwa mapema likiwemo suala la Kimazingira.
Balozi Seif alisema maombi ya uanzishwaji wa Miradi zaidi ya Mmoja katika eneo dogo yaliyofanywa na Uongozi wa Hoteli ya Sun Rise ndio ulioisukuma Serikali kutaka kufanya utafiti wa kina kwa kuzishirikisha Taasisi zote zinazosimamia Uwekezaji ili ijiridhishe na hatimae kutoa maamuzi sahihi.
Mapema Mkurugenzi Uwezeshaji na Miradi ya Maendeleo wa Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar {ZIPA} Nd. Sharif  Ali Sharif  alisema Taasisi ya Uwekezaji hufikia maamuzi ya kutoa ruhusa ya kuanzishwa kwa Mradi wa Uwekezaji baada ya Mmiliki wa Mradi husika kukamilisha taratibu zote zinazomruhusu kuwekeza Nchini.
Nd. Sharifu alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba miongoni mwa Taratibu hizo ni ushirikishwaji wa Wataalamu wa Taasisi zote zilizopewa jukumu la kusimamia masuala ya miradi na uwekezaji wakiwemo sambamba na Wawakilishi wa Wananchi katika maeneo husika.
Alisema kinachozingatiwa na kupewa kipaumbele zaidi kwa miradi ya kiuchumi ni namna Miradi hiyo inavyoweza kusaidia pato la Taifa kwa asilimia kubwa pamoja na kuunga mkono jitihada za Maendeleo ya Wananchi katika kustawisha maisha yao.
Akiwasilisha salamu za Wananchi wa Ukanda wa Mwambao wa Matemwe, Diwani wa Wadi ya Mwatemwe Ndugu Hassan Mcha Hassan alisema Mradi wa Hoteli ya Sun Rise umeleta mafanikio makubwa kwa Wananchi wake tokea ulipoanzishwa  kwa zaidi ya Miaka Kumi sasa.
Nd. Hassan alisema Wananchi wa Matemwe wamelazimika kumuenga enga Muwekezaji huyo kutokana na juhudi kubwa anazoendelea kuzichukuwa za kuwasogezesha miundombinu katika kuwarahisisha mambo yao ya Maendeleo ya kila siku.
Alisema kitendo cha Uongozi wa Sun Rise cha kupeleka huduma za Umeme Kijijini hapo uliogharimu zaidi ya shilingi Milioni  Mia 128,000,000/-  kimewawezesha Wananchi hao  pamoja na Wanafunzi wa Skuli za Vijiji hivyo kupata huduma za Umeme zilizorahisisha pia upatikanaji wa huduma za Maji safi na salama.
Diwani huyo wa Wadi ya Matemwe alielezea faraja yake kwa niaba ya Wananchi anaowaongoza kwamba Sun Rise hivi sasa imetoa ajira kwa Vijana wazalendo wa Vijiji vya Mwambao wa Matemwe katika Miradi ya Hoteli na kupunguza ukali wa Maisha kwa Wananchi hao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.