Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, Azungumza na Balozi wa Indonesia Ikulu Zanzibar. Dk

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Balozi wa Indinonesia Tanzania Balozi Ratlan Pardede, alipofika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo leo. 5/2/2018. 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amepongeza azma ya Indonesia ya kukuza uhusiano na ushirikiano kati yake na Zanzibar katika sekta ya utalii, biashara kupitia zao la karafuu pamoja na kilimo cha zao la mwani.

Rais Dk. Shein ametoa pongezi hizo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Balozi wa Indonesia katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ratlan Pardede, Ikulu mjini Zanzibar ambapo Balozi huyo alieleza azma ya nchi yake kushirikiana na Zanzibar katika sekta hizo.

Katika maelezo yake Dk. Shein alimueleza Balozi Pardede kuwa uwamuzi huo wa Indonesia wa kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo ni uwamuzi sahihi ambao utaimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo baina ya pande mbili hizo.

Dk. Shein alisema kuwa kwa upande wa Sekta ya utalii, Zanzibar kwa upande wake tayari imeshaweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha sekta hiyo inaimarika na inaendelea kuchangia pato la Taifa.

Hivyo, alieleza kuwa mashirikiano kati ya Zanzibar na Indonesia katika sekta hiyo yatasaidia kwa kiasi kikubwa hasa ikizingatiwa kuwa Indonesia tayari imeimarika katika sekta ya utalii kupitia teknolojia ya kisasa pamoja na masuala ya uongozi na usimamizi kwenye sekta hiyo sambamba na mafunzo na utaalamu.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alisisitiza haja ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa pamoja kati ya Zanzibar na Indonesia kupitia kisiwa chake cha kitalii cha Bali ambacho ni maarufu duniani kwa utalii nchini Indonesia.

Dk. Shein alitoa rai ya kuanzisha uhusiano maalum baina ya Zanzibar na Kisiwa cha Bali katika kuendeleza utalii hatua ambayo itazisaidia sana pande zote mbili hasa ikizingatiwa kwamba mazingira ya kijiografia ya Bali yanafanana na Zanzibar.

Aliongeza kuwa uhusiano huo vile vile utaiwezesha Zanzibar kujifunza mbinu bora katika uendeshaji wa sekta ya utalii kutokana na uzoefu wa kisiwa hicho katika kuendeleza sekta ya utalii.

Aidha, kwa upande wa sekta ya biashara ambapo Indonesia imeahidi kuiunga mkono Zanzibar hasa katika zao la karafuu, Dk. Shein alieleza kuwa hiyo ni habari njema ambayo italifanya zao la karafuu lizidi kuimarika katika soko la kimataifa pamoja na kuzidi kulipandisha thamani na kupelekea kukuza uchumi wa Zanzibar.

Kwa upande wa zao la mwani, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikichukua juhudi za makusudi katika kuhakikisha wakulima wa zao hilo wananufaika na kilimo hicho lakini kinachowarejesha nyuma ni bei ya zao hilo inayotolewa na makampuni zinazonunua mwani hapa nchini kwani hununua kwa bei ya chini na kuwafanya wakulima kuvunjika moyo.

Hivyo, Rais Dk. Shein alieleza kuwa azma ya Indonesia kuiunga mkono Zanzibar kwenye zao hilo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuiamrisha kipato cha wakulima wa zao hilo, utaalamu wa kilimo hicho sambamba na kuimarisha sekta ya kilimo na biashara hapa Zanzibar.

Pia, katika mazungumzo hayo, viongozi hao, walizungumzia haja ya kuendeleza uhusiano katika sekta nyengine za maendeleo ikiwemo sekta ya viwanda ambapo Indonesia imepiga hatua kubwa na kwa upande wa Zanzibar nayo hivi sasa imejikita katika kuhakikisha sekta ya viwanda inaimarika.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alimueleza Balozi huyo juu ya mazungumzo aliyoyafanya na Makamo wa Rais wa Indonesia Muhammad Jusuf Kalla huko mjini Jakata Indonesia mnamo mwezi Machi mwaka jana ambapo katika mazungumzo hayo walisisitiza ushirikiana katika sekta za maendeleo ikiwemo utalii, afya, biashara na viwanda, uwekezaji, kilimo, usafiri na usafirishaji, uvuvi, pamoja na sekta nyenginezo.

Viongozi hao ambao walifanya mazungumzo katika ukumbi wa Mkutano wa Balai Sidang mjini Jakata, Indonesia ulipofanyika Mkutano wa Kwanza wa Wakuu wa nchi na Serikali wa Jumuiya ya nchi zinazopakana na Bahari ya Hindi (IORA) ambapo Dk. Shein alihudhuria, sambamba na kushiriki utiaji saini Mkataba unaoainisha mikakati, mipango na maazimio yanayolenga kuongeza kasi ya maendeleo ya Jumuiya hiyo.

Nae Balozi wa Indonesia katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ratlan Pardede alimueleza Dk. Shein azma ya Serikali ya Indonesia ilivyodhamiria katika kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta za aendeleo ikiwemo utalii, kilimo kupitia zao la mwani na biashara kwa zao la karafuu.

Alimueleza Dk. Shein kuwa Indonesia iko tayari kushirikiana na Zanzibar katika kuimarisha sekta ya utalii katika nyanja zote za kukuza sekta hiyo ikiwemo mafunzo, uongozi na usimamizi katika sekta hiyo sambamba na kubadilishana watalii kwa kuwepo usafiri wa moja kwa moja kati ya Indonesia na Zanzibar pamoja na mambo mengineyo.

Aidha, Balozi huyo alimueleza Dk. Shein kuwa nchi yake hivi sasa milango yake iko wazi katika kushirikina na Zanzibar kwenye zao la karafuu kwa kuahidi kusaidia kulipa thamani zaidi zao la karafuu ya Zanzibar pamoja na kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuimarisha soko la karafuu ya Zanzibar.

Kwa uapnde wa zao la mwani nchi hiyo imeahidi kutoa ushirikiano wake katika kuhakikisha mwani wa Zanzibar utapata soko zuri ndani na nje ya nchi hiyo pamoja na kulipa thamani na kutoa mafunzo kwa wakulima wa zao hilo hapa nchini.

Sambamba na hayo, Balozi huyo alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa nchi yake itaendeleza uhusiano na ushirikiano uliopo kati yake na Zanzibar pamoja na kuunga mkono vipaumbele vilivyowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta zake za kiuchumi na kijamii.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.