Habari za Punde

Polisi Kaskazini Pemba kudumisha amani sikukuu ya Pasaka


Na Said Abrahaman, Pemba.

JESHI la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, limesema kuwa litadumisha amani na utulivu katika kipindi hichi sikukuu ya Pasaka.

Akizungumza na Gazeti hili Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Haji Khamis Haji, alisema kuwa jeshi hilo limejipanga vizuri ili kuhakikisha amani iliyopo inadumishwa.

Alieleza wamedhamiria kufanya doria za miguu pamoja na kutumia gari katika maeneo mbali mbali ambayo yatatumika kwa sherehe hizo.

"Tumepanga kufanya doria katika maeneo yote, ambayo yatakuwa yakitumika kwa sherehe hizo hasa katika nyumba za ibada pamoja na fukwe,",alifahamisha Kamanda.

Mbali na hayo lakini pia Kamanda huyo alisisitiza kuweka askari wake barabarani ili kulinda usalama wa barabarani.

Hata hivyo kamanda huyo aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana na jeshi hilo  ili liweze kufanya kazi zake inavyotakiwa.

Wakati huo huo Jeshi hilo linamshikilia kijana, Mohammed Salim Suleiman mkaazi wa Pandani Wete kwa tuhuma za kupatikana ng'ombe anasadikiwa ni wa wizi.

Kamanda Haji, alithibitisha hilo na kusema   kuwa mtuhumiwa huyo alipatikana na tuhuma hizo  usiku wa kuamkia leo huko Pandani.  

"Ni kweli kuna kijana mmoja kwa jina anaitwa Mohammed Salim Suleiman wa Pandani alikamatwa akiwa na ng'ombe watatu wa wizi"alifahamisha Kamanda.

Hata hivyo alisema kuwa kwa sasa mtuhumiwa huyo yuko chini ya ulinzi na upelelezi unaendelea.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.