Habari za Punde

WANANCHI WATAKIWA KUJITOKEZA KWA WINGI KATIKA WIKI YA ELIMU KWA MLIPAKODI


Na: Veronica Kazimoto,Dar es Salaam,4 Machi, 2018.
Wito umetolewa kwa wafanyabiashara na wananchi wote kwa ujumla kujitokeza kwa wingi katika vituo ambavyo vimepangwa rasmi kwa ajili ya wiki ya elimu kwa mlipakodi itakayofanyika kuanzia kesho tarehe 5 hadi 9 Machi, mwaka huu katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi Richard Kayombo kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), alisema maandalizi yamekamilika katika vituo vyote nchi nzima hivyo wananchi watumie fursa hii kujifunza masuala mbalimbali yanayohusu kodi.

"Maandalizi ya wiki ya elimu kwa mlipakodi yamekamilika kwa kiasi kikubwa, niwaombe tu wafanyabiashara na wananchi wote wajitokeze kwa wingi katika vituo vilivyotengwa rasmi katika kila mkoa nchi nzima kwa ajili ya kupata uelewa zaidi juu ya masuala ya kodi, kutoa malalamiko, mirejesho, changamoto pamoja na  maoni mbalimbali," alisema Kayombo.

Kayombo alifafanua kuwa katika wiki hiyo  mada mbalimbali zitafundishwa kama vile ulipaji wa Kodi ya Majengo kwa njia ya kieletroniki, Mkataba wa Huduma kwa Mlipakodi ambao umeainisha haki na wajibu wa mlipakodi na viwango vya huduma wanavyopaswa kupata kutoka TRA pamoja na umuhimu wa kutoa na kudai risiti ikiwa ni pamoja na kikagua kabla ya kuondoka nayo.

"Watalaam wetu wamejipanga vizuri kutoa elimu katika kila mkoa kwenye wiki hii ya elimu kwa mlipakodi. Mada mbalimbali zitafundishwa ikiwa ni pamoja na  kuwakumbusha wananchi kulipa kodi inavyostahili ndani ya muda utaotakiwa," alisisitiza Kayombo. 

Kayombo alisema kuwa, katika wiki hiyo kutakuwa na usajili wa walipakodi wapya hivyo wafanyabiashara ambao hawajasajiliwa wajitokeze kwa wingi kwa ajili ya kupata huduma hiyo.

Wiki ya elimu kwa mlipakodi itakuwa inafanyika kila baada ya miezi mitatu ikiwa na lengo la kuelimisha, kusikiliza malalamiko, changamoto, kupokea mrejesho pamoja na maoni mbalimbali kutoka kwa walipakodi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.