Habari za Punde

MPINA AWATAKA WAWEKEZAJI WA VIWANDA VYA PUNDA KUONGEZA BEI



Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina(mwenye miwani) akikagua kiwanda cha kuchinja Punda cha Hua Cheng Limited kilichopo nje kidogo ya mji wa Dodoma alichokifungua hivi karibuni leo. (Picha na Jumanne Mnyau)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina(mwenye miwani) akipokea maelezo ya usindikaji wa nyama Punda kutoka kwa mfanyakazi wa wa kiwanda cha kuchinja Punda cha Hua Cheng Limited Elizabeth Peter.(Picha na Jumanne Mnyau)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi,Luhaga Mpina(mwenye miwani) akitembezwa katika kiwanda cha  kuchinja  Punda  cha Hua Cheng Limited kilichopo nje kidogo ya mji wa Dodoma  alichokifungua  hivi karibuni na Meneja Mkuu wa kiwanda hicho bwana Xun Long Go .(Picha na Jumanne Mnyau)
Na John Mapepele, Dodoma

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amewataka wawekezaji wa viwanda vya kuchinja Punda nchini kupandisha bei ya kununua wanyama hao badala ya shilingi laki mbili ya sasa kwa punda mmoja ili kudhibiti utoroshaji wa mifugo nje ya nchi ambapo inakadiriwa kuwa zaidi ya mifugo elfu kumi inatoroshwa mipakani kwa siku kwenda nje ya nchi inakonunuliwa kwa bei ya juu.

Akizungumza leo baada ya kufanya ziara ya kushitukiza katika Kiwanda cha Punda cha Hua Cheng Limited kilichopo nje kidogo ya mji wa Dodoma alichokifungua hivi karibuni, Waziri Mpina alisema bei hiyo haiendani na gharama halisi ya ufugaji wa Punda hali inayowafanya wafugaji kuwatorosha mifugo na kulikosesha taifa mapato makubwa.

Alisema ili punda aweze kufikia hatua ya kuchinjwa inachukua kiasi cha miaka miwili ambapo gharama zake za ufugaji zinakuwa juu ukilinganisha na bei ya shilingi laki mbili anayouzwa kwa wenye viwanda vya punda nchini.

Aidha alisema kumekuwa na utoroshaji mkubwa wa mifugo wanaokadiriwa kufikia takribani 1,614,035 kwa mwaka unaofanyika kwenye mipaka ya nchi yetu ambapo takribani shilingi bilioni 32.28 zinapotea kama ushuru na takribani shilingi bilioni 24.21 zinapotea kutokana na kodi ya mapato ambayo ingelipwa kwa nyama ambayo ingeuzwa hapo nchini.

Aidha Mpina ameunda tume ya wataalam kutoka Wizarani kwa ajili ya kuja kufanya tathmini kama kiwanda hicho kimetimiza masharti yote yaliyotolewa na Serikali baada ya kukifungua Februari mosi mwaka huu ambapo alisema ikibainika kuwa kiwanda hakijakidhi masharti yaliyotolewa na Serikali kitachukuliwa hatua kali zaidi za kisheria ikiwa ni pamoja na kukifungia kufanya kazi zake.

Aliyataja baadhi ya masharti yaliyotolewa na Serikali wakati wa kukifunga kiwanda hicho Julai 2017 kuwa ni pamoja na kuwa na ranchi za punda, kuboresha kosaafu za Punda nchini, kuunda na kuingia mikataba na vikundi vya wafugaji wa Punda na kuwa na Punda wasiopungua mia tatu katika eneo la kuhifadhia mifugo kabla ya kuchinjwa ili kuwa kuhakikisha kwamba mifugo wanaangaliwa kwa wiki mbili kabla ya kuchinjwa ili wawe katika ubora wa kimataifa.

Waziri Mpina alisema uwekezaji wa aina hiyo wa kuongeza thamani ya mazao ya mifugo ni moja ya vipaumbele vya wizara yake kwa sasa ili kuchochea kwa kasi kufanikisha azma ya Tanzania ya viwanda.

Aidha aliwahakikishia wawekezaji wa kiwanda hicho kuwa endapo watakuwa wamekamilisha masharti atawapa kibali cha kudumu ambapo pia atawaongezea idadi ya kuchinja Punda kutoka punda 20 wa sasa ili vijana wengi wapate ajira na kiwanda kiweze kuchangia zaidi katika mapato ya Serikali.

Mpina aliwahimiza wawekezaji hao kuhakikisha wanawasaidia wafugaji katika kuongeza uzalishaji, kupambana na maradhi, upatikanaji wa maji na malisho kwa mifugo.

Alisema idadi ya punda waliopo nchini ni 520,000 tu hivyo juhudi za makusudi zinahitajika kuongeza uzalishaji.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda hicho Xun Long Go alimshukuru Waziri Mpina kwa kufungua kiwanda hicho ambapo amesema hadi sasa kiwanda kimezalisha na kuuza tani 224 za nyama ya Punda kwenda nchini China na Vietinam ambapo pia tani 52 za ngozi ya Punda ilizalishwa na kuuzwa kuanzi mwezi Februari, 2018.

Alisema kiwanda hicho kimeajiri watanzania 55 ambapo hadi sasa kina punda 88 katika maeneo ya Chalinze na Zuzu mkoani Dodoma.

Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji Mifugo na Masoko wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Lucia Chacha aliutaka uongozi wa kiwanda hicho kwa kubuni mbinu za kuwasaidia wafugaji kwa kuwapatia elimu bora zaidi ya ufufaji wa punda ili waweze kuwazalisha kwa wingi zaidi kuliko ilivyo sasa

Hivi sasa Tanzania ina viwanda viwili tu vya kuchinja na kuuza nyama ya punda ambavyo ni kiwanda cha Punda cha Huacheng Limited kilichopo nje kidogo ya mji wa Dodoma na Kiwanda cha Fang Hua kilichopo Shinyanga ambavyo vyote vimepewa kibali cha kuchinja Punda 20 kwa siku kila kimoja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.