Habari za Punde

Polisi Kaskazini Pemba yakusanya zaidi ya Mil 8

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

JESHI la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, limeingiza jumla ya Tshs, Milion 8,450,000/=baada ya  kukamata makosa 1107 ya usalama barabarani kuanzia Januari hadi April 13 mwaka huu.       

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Haji Khamis Haji, alisema makosa ya magari yalikuwa 714, vespa na pikipiki 346 na baskeli 47.

Alisema   Jeshi hilo limekamata makosa 1107, ikiwemo makosa ya mwendo kasi, kutokuvaa kofia ngumu, kutotii sheria za njia, kuzidisha abiria, kutokuwa na leseni, baskeli na kutumia gari zisivyoruhusiwa. 

“Makosa hayo yalipelekwa mahakamani, ambapo kati ya kesi hizo, wengine walionywa, kesi nyengine kufutwa na nyengine kupatiwa hukumu”, alisema Kamanda huyo.

Kamanda Haji, alisema  wamekuwa wakifanya doria za miguu na vyombo vya moto, ili kuhakikisha wanadhibiti makosa ya usalama barabarani, ambayo yanaweza kusababisha athari mbali mbali kwa watumiaji wa njia kwenye Mkoa huo.

Aliwataka madereva kukata leseni, ili kuweza kuondosha migogoro na kusema kuwa Jeshi hilo litakuwa barabarani wakati wote na kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wanaokaidi kutii sheria zilizowekwa.

“Elimu tunatoa kwa madereva, ili wajue sheria zao lakini wapo baadhi yao wanakaidi, hivyo hatutowaachia madereva wa aina hiyo”, alisema.
Hivyo Kamanda huyo aliwataka madereva kufuata sheria bila ya shuruti, ili kuweza kuepusha changamoto zinazoweza kuepukika, ikiwepo ajali.
                                              

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.