Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzin Dk. Shein, Ahudhuria Hafla ya Hitma ya Marehemu Mzee Abeid Amani Karume Afisi Kuu ya CCM Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akiweka shada la Maua katika kaburi la Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, baada ya kumaliza dua na hitma ya kumuombea iliofanyika katika jengo la Afisi Kuu Kisiwandui Zanzibar leo.7/4/2018.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein leo ameongoza hitma ya kumuombea dua Rais wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, iliyofanyika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui mjini Zanzibar.

Hitma hiyo, ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa, Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Awamu ya Pili Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Sita, Mhe. Amani Abeid Karume na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd.

Viongozi wengine walihudhuria katika hitma hiyo ni  Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabhi, Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakary Zubeir, Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji, viongozi wa Serikali zote mbili, Viongozi wastaafu, Viongozi wa vyama vya siasa, Masheikh kutoka Zanzibar na Tanzania Bara, Wabunge,Wawakilishi, Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama, wananchi kutoka maeneo mbali mbali pamoja na Mabalozi wadogo waliopo hapa Zanzibar.

Hitma hiyo ya kumuombea dua Marehemu Mzee Abeid Amani Karume  ambayo ni miongoni mwa Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa Zanzibar (Karume Day) ilitanguliwa na Qur-an tukufu, iliyosomwa na Ustadh Sharif Abdulrahman Muhidin kutoka Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana na kuongozwa na Sheikh Jafar Abdallah kutoka Masjid Noor Muhammad.

Mara baada ya hitma hiyo, Sheikh Khamis Gharib kutoka Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana alitoa tafsiri ya Suratul Fussilat iliyosomwa na Ustadh Sharif Abdulrahman Muhidin kuanzia aya ya 30 mpaka aya ya 35 ambayo inaenda sambamba na maudhui ya siku hii ya leo.

Akitoa tafsiri hiyo iliyoenda sambamba na mawaidha yenye mnasaba na kumbukumbu ya Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, Sheikh Khamis Gharib alieleza kuwa kuna kila sababu ya kumuombea dua kiongozi huyo pamoja na mashujaa wenzake ili MwenyeziMungu awafanyie wepesi na awarudhuku pepo ya juu ya Firdaus kutokana na mema waliyoyafanya.

Baada ya kisomo hicho cha hitma ambacho hufanyika kila mwaka inapofika tarehe 7, Aprili, viongozi hao na wananchi waliohudhuria katika hitma hiyo walimuombea dua, marehemu mzee Karume katika kaburi lake lililopo pembezoni mwa Afisi hiyo ya CCM Kisiwandui iliyoongozwa na viongozi wa dini akiwemo Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabhi kwa upande wa dini ya Kiislamu, Padri Stanley Lichinga kutoka Kanisa la Anglikana  Zanzibar na Kashap Pandra aliyesoma kwa niaba ya Wahindu.

Viongozi na wanafamilia waliweka mashada ya maua katika kaburi la Marehemu Mzee Karume akiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, aliyeweka shada la maua kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia, ni Amiri Jeshi Mkuu Dk. John Pombe Magufuli na Mzee Abdallah Rashid Abdallah aliweka shada la maua akiwawakilisha wazee.

Wengine walioweka mashada ya maua ni Meja Jenerali Sharif Sheikh Othman aliyeweka kwa niaba ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Tanzania, Balozi Ali Karume aliweka kwa niaba ya familia ya Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume na Balozi mdogo wa Msumbiji anayefanya kazi zake hapa Zanzibar Jorge Augusto  Menezes aliyewawakilisha Mabalozi wenzake waliopo hapa nchini.

Aidha, Mama Mwanamwema Shein aliungana na akina mama wengine katika hitma hiyo iliyofanyika katika Ofisi hiyo Kuu ya CCM Kisiwandui, akiwemo mjane wa marehemu mzee Abeid Karume, Mama Fatma Karume,  Mama Shadya Karume na viongozi wengine wanawake wa kitaifa wakiwemo Mawaziri, Wabunge, Wawakilishi na wananchi kutoka maeneo mbali mbali ya Zanzibar na Tanzania Bara.

Mara baada ya kumalizika kwa tukio hilo muhimu katika eneo hilo la Afisi za CCM Kisiwandui, Rais Dk. Shein alipata fursa ya kufanya mahojiano mafupi na waandishi wa habari na kusisitiza kuwa Marehemu Mzee Karume aliweka misingi ya Utawala Bora katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ataendelea kukumbukwa wka hilo na mengine mengi aliyoyafanya.

Alisema kuwa marehemu mzee Karume amefanya mengi ambalo kubwa ni ukombozi wa Zanzibar ambao ulikuwa wa lazima na Mapinduzi ya Januari 12, 1964 yalikuwa ya halali na yeye alisimama kidete kuingoza ASP na kupanga na wenzake na hatimae kuikomboa Zanzibar na kupelekea Serikali kurudi kwa wananchi wenyewe wa Zanzibar.

Alitumia fursa hiyo kutoa, pongezi kwa viongozi na wananchi waliohudhuria katika dua hiyo, na kusisitiza kuwa Mzee Karume ameweka mfumo mpya wa Serikali ambapo Serikali hiyo imeundwa kwa Dikrii namba sita kati ya Dikrii nyingi zilizotungwa ambapo Serikali ambayo ilikuwa na mfumo wa Kidemokrasi na kusisitiza kuwa  Serikali ya Awamu ya Saba imeendelea kufanya kama zilivyofanya Awamu sita zilizopita kwa nyakati tofauti na uwezo tofauti.

Aidha, alisema kuwa wanaosema kuwa neno Mapinduzi lisiwepo katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni wapinga Mapinduzi na Muungano na si watu wa maendeleo na kusisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ipo na itaendelea kuwepo kwa sababu imetamkwa katika Katiba ya Zanzibar na Katiba ya Jamhuri ya Mmuungano wa Tanzania kwa lengo la kuwatumikia wananchi na ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao ameisimamia kuiunganisha yeye pamoja na mwenziwe Marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

“Na huyo anayoyabeza Mapinduzi  basi ujue kuwa pia, kafaidika nayo, kwani hakuna mwananchi hata mmoja wa Zanzibar ambaye hajafaidika na Mapinduzi yaliyosimamiwa na Mzee Karume...na hakuna hata mmoja asiyemuombea dua Mzee Karume na yule anayefanya hivyo basi ni wale ambao wanayapinga Mapinduzi”, alisema Alhaj Dk. Shein.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alisema kuwa siku hii ni siku adhimu kwani walidhani wataidhoofisha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, walidhani wananchi wa Zanzibar watavunjika moyo na  wao walidhani kuwa wao wanaweza kuitawala Zanzibar mambo ambayo hayakutokea na hayatatokea na kueleza kuwa wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanaikumbuka na wanaithamini sana siku hii.

April 7, 1972 ndiyo siku aliyouawa Rais wa Kwanza wa Zanzibar marehemu Mzee Abeid Amani Karume na wapinga maendeleo nchini ambapo hivi leo imetimia miaka 46 tokea utokee msiba huo.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.