Habari za Punde

Hotuba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria Utawala Bora na Idara Maalum ya BLW kwa wizara ya OR TMSMIM 2018/2019

Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria Utawala Bora na Idara Maalum Mhe. Machano Othman Akisoma Hutoba ya Maoni ya Kamati Kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakati wa Mkutano wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Zanzibar.

HOTUBA YA MAONI YA KAMATI YA SHERIA, UTAWALA BORA
NA IDARA MAALUM KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA
MATUMIZI YA WIZARA YA NCHI (OR) TAWALA ZA MIKOA,
SERIKALI ZA MITAA NA IDARA MAALUM ZA SMZ KWA
MWAKA WA FEDHA 2018/2019

Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba kutumia nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mwenye wingi wa Rehma, Muumba wa Mbingu na Ardhi na vyote vilivyomo, kwa kutujaalia kukutana kwa mara nyengine tena, asubuhi hii ya leo, katika Mkutano huu wa Kumi wa Baraza la Tisa kwa dhamira ya kujadili Bajeti kuu ya Serikali na Taasisi zake, chini ya Baraza lako Tukufu. Kwani hii ni rehma yake Muumba kwa kutupa pumzi na afya njema ambayo wenzetu wengine amewanyima fursa hii.

Mheshimiwa Spika, pia, napenda kutumia fursa hii adhim kushukuru na kukupongeza wewe binafsi kwa kunipa nafasi hii ya kusimama mbele ya Baraza lako Tukufu, kwa lengo la kuwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Sheria, Utawala Bora na Idara Maalum kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Wizara ya Nchi (OR) Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ kwa mwaka wa fedha 2018/2019 kama sheria na Kanuni za Baraza hili zinavyoelekeza.

Mheshimiwa Spika, aidha nawapongeza na kuwashukuru kwa dhati viongozi wa Wizara hii wakiongozwa na Waziri wao makini Mhe. Haji Omar Kheir, Naibu Waziri, Mhe. Shamata Shaame Khamis, Nd. Katibu Mkuu, Wakuu wa Mikoa pamoja Afisa Mdhamini Pemba, na watendaji wote kwa mashirikiano yao makubwa waliyotuonesha katika Kamati yetu kwa kutekeleza majukumu yetu ipasavyo. Vile vile, shukurani za pekee ziende kwa Wakuu, Maafisa na Wapiganaji wote wa Idara Maalum za SMZ kwa mashirikiano yao waliyotupatia kwa kipindi chote cha utekelezaji wa shughuli za Kamati.

Mheshimiwa Spika, Sambamba na hayo, natumia nafasi hii kuishukuru Wizara ya Nchi (OR) Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ kwa kutumia na kutekeleza vyema ushauri na maagizo ya Kamati pamoja kuisimamia kikamilifu Bajeti yao ya mwaka 2017/2018, jambo hili limewawezesha kujenga ari ya kuwasilisha mbele ya Kamati yetu, pamoja na Baraza lako Tukufu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha, kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 ili ipate baraka za Wajumbe wako na kwa mnasaba huo, tunaomba Baraza lako tukufu liiridhie na liipitishwe Bajeti hii kwa maslahi ya wananchi na Serikali kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, Aidha, naomba kutoa shukrani na pongezi za pekee kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi imara wa Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein, kwa kusimama vyema katika uongozi wake na kuhakikisha maendeleo ya watu na ustawi wa jamii nchini yameimarika pamoja na kusimamia maendeleo ya uchumi kufuatana na misingi na madhumuni yaliyowekwa na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kwa kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora umefanikiwa.

Mheshimiwa Spika, Ni matumaini ya Kamati yangu kuwa mafanikio yanayopatikana katika uimarikaji wa uchumi wetu na huduma za kijamii yanatokana na Utekelezaji mzuri wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015/2020, ambapo utekelezaji wake utaendelea kwa kipindi chote cha Bajeti ya mwaka 2018/2019 na kuhakikisha kuwa hatua kubwa ya maendeleo inafikiwa chini ya misingi bora iliyoainishwa ndani ya Ilani hii ili kuakisi na kuiwezesha jamii kiuchumi na kujikwamua na hali ngumu ya umasikini.

Mheshimiwa Spika, Bajeti hii imekadiriwa kufanya kazi kwa kuzingatia malengo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na inaakisi hali halisi ya uchumi wetu na harakati za kupunguza umasikini ifikapo mwaka 2020 lakini pia kwa kuzingatia malengo ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA III).

Mheshimiwa Spika, pia nachukua nafasi hii kuwashukuru kwa kazi kubwa walioifanya Wajumbe wa Kamati yangu wakati tukiwa tunapitia bajeti hii, kwa kuonesha mashirikiano yao makubwa katika kutekeleza majukumu ya Kamati hii.
Hivyo, kwa ridhaa yako naomba sasa uwatambue Wajumbe wa Kamati hii kama ifuatavyo:
1.     Mhe. Machano Othman Said             Mwenyekiti
2.     Mhe. Mwantatu Mbarak Khamis         Makamo Mwenyekiti
3.     Mhe. Saada Ramadhan Mwendwa       Mjumbe
4.     Mhe. Wanu Hafidh Ameir                 Mjumbe
5.     Mhe. Nadir Abdulatif Yussuf              Mjumbe
6.     Mhe. Ali Khamis Bakar                      Mjumbe
7.     Mhe. Suleiman Makame Ali               Mjumbe
8.     Ndg. Ali Alawy Ali                                       Katibu, na
9.     Ndg. Haji Jecha Salim                        Katibu.
Mheshimiwa Spika, Kamati ya Sheria, Utawala Bora na Iadara Maalum imetumia uweledi wake wa hali ya juu katika kupitia, kuchambua na kujiridhisha katika programu zote zilizokusudiwa kufanyiwa kazi kupitia Fungu la Bajeti la wizara hii kama ilivyoelezwa katika Kanuni ya 96(1) na 106(3) katika jadweli la kwanza la Kanuni za Baraza la Wawakilishi, 2016.

Mheshimiwa Spika, Ni imani ya Kamati hii kwamba kupatikana kwa fedha zilizopangwa katika Wizara hii kutasaidia kwa kiasi kikubwa utekelezaji na ukamilishaji wa malengo yaliyokusudiwa kutekelezwa ikiwa ni pamoja na kukamilisha miradi iliyotengwa kwa mwaka huu wa 2018/2019 na vile vile kuendeleza mradi mkubwa wa Mahanga na nyumba za Askari wa Idara Maalum kisiwani Pemba.

IDARA ZA MAKAO MAKUU (FUNGU D 01)
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza kazi zake kwa mwaka wa fedha 2017/2018 Kamati yangu imefanikiwa kutembelea na kujionea shughuli mbali mbali za kawaida na zile za miradi ya maendeleo ambazo zinasimamiwa na kuratibiwa na wizara hii katika utekelezaji wake, ikiwa zinakabiliwa na changamoto kadhaa, kama vile uchache wa vitendea kazi na visivyokidhi wakati tulionao, uhaba wa vyombo vya usafiri pamoja na upungufu mkubwa wa watendaji katika sekta zilizogatuliwa, ubovu wa barabara za ndani pamoja na uchakavu wa baadhi ya Mahanga na nyumba za Askari wetu wa Idara Maalum, hata hivyo, Kamati inaipongeza sana Serikali kwa kuanza ujenzi wa Mahanga ya Wapiganaji wa Vikosi vyetu kupitia mradi maalum.

Mheshimiwa Spika, Kamati inashauri kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Idara hizi kupatiwa fedha za kutosha na kwa wakati ili kuweza kutatua changamoto ambazo zinawakwaza katika uendeshaji wa shughuli zao, kwa lengo la kuleta ufanisi na kuimarisha sekta zote za maendeleo katika Taasisi hizo.

Mheshimiwa Spika, Kamati inapongeza sana kazi nzuri zinazofanywa na afisi kuu kwa kupitia na kuandaa miradi mbali mbali ya maendeleo ambayo msingi wake ni kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi katika nchi yetu. Hata hivyo, Kamati imebaini, katika bajeti hii wizara imekusudia kujenga barabara za ndani kupitia Halmashauri zake mbali mbali za Unguja na Pemba lakini fedha zilizokusudiwa kujengewa barabara hizo hazionekani katika bajeti hii, jambo ambalo linatia shaka utekelezaji wake, Kamati inashauri Serikali kupitia Mfuko wa Barabara kuwapataia fedha walau asilimia 30% ya makusanyo yao ili Wizara iweze kujenga barabara za ndani.

Mheshimiwa Spika, Kamati inashauri, Wizara inapoweka mipango ya ujenzi wa barabara au mradi wowote uliokusudiwa kutekelezwa na Halmashauri au Manispaa fedha zake zioneshwe mapema katika bajeti ya Wizara katika mwaka husika ili wajumbe wa Baraza hili tukufu watambue mapema kiasi cha fedha zilizotengwa kwa kuendeleza ujenzi huo kama zinakidhi mahitaji au hazikidhi kwa mujibu wa umuhimu wa barabara hizo.
Aidha, Kamati inashauri barabara ambazo zilikusudiwa kujengwa na Halmashauri katika bajeti ya mwaka 2017/2018 na kushindwa kujengwa kwa ukosefu wa fedha, barabara hizo zijengwe katika bajeti hii inayokuja kwa mwaka 2018/2019.
IDARA YA URATIBU WA TAWALA ZA MIKOA NA
SERIKALI ZA MITAA (Fungu D 07 – D 11)

Mheshimiwa Spika, Katika programu ya Uratibu wa Tawala za Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa, kwa ujumla Kamati yangu ya Sheria, Utawala Bora na Idara Maalum imeridhishwa na utekelezaji wa programu mbali mbali zinazosimamiwa na Tawala za Mikoa pamoja Mamlaka ya Serikali za Mitaa zaidi katika ukusanyaji wa mapato kutokana na baadhi ya Halmashauri, Mabaraza na Manispaa kuvuka malengo waliyokusudia. Hii inaonesha wazi kuwa endapo vyanzo vya mapato vitasimamiwa ipasavyo basi hali ya uchumi katika nchi yetu itaimarika na hivyo kuweza kutekeleza vyema Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015/2020.

Mheshimiwa Spika, Kamati imebaini kuwepo kwa changamoto katika utekelezaji wa Sheria ya Tawala za Mikoa, nambari 8 ya mwaka 2014, kifungu cha 30(1) amabacho kinazitaka Kamati za Maendeleo za Mikoa kukutana mara mbili kwa mwaka, Hata hivyo, vikao hivyo havifanyiki na kupelekea Mkoa kushindwa kufanya tathmini nzuri juu ya utekelezaji wa shughuli zake hivyo kupelekea kukosekana kwa maendeleo ya nchi.

Mheshimiwa Spika, kukosekana kufanyika kwa vikao hivi katika Kamati za Maendeleo ya Mkoa kunapelekea malalamiko mbali mbali kwa baadhi ya wajumbe wa Kamati hizi wakiwemo Wabunge ambao huingiziwa fedha zao katika miradi iliyopangwa lakini pia hukosa marejesho ya matumizi ya fedha hizo kwa vile vikao hivi vimekosekana.

Mheshimiwa Spika, Kamati inashauri katika bajeti hii tunayoijadili, Serikali kupitia Wizara hii ya Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ kuhakikisha kuwa vikao hivi vinafanyika na kwa wakati mahususi ili kuendana sambamba na sheria hii pamoja kusaidia kuibua miradi mengine ya kimaendeleo.

Mheshimiwa Spika, Kamati inaipongeza sana Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kusimamia kikamilifu mradi wa Ugatuzi ambao kwa mwaka huu unaoishia Juni 30, 2018 mafanikio kadhaa yamepatikana ikiwa ni pamoja na uelewa wa wananchi juu ya dhana kamili ya Ugatuzi na faida zake kwa jamii. Kwa kuwa hili ni jambo jema kwa nchi yetu na kwa kuwa lengo la Serikali ni kuwashirikisha wananchi katika Serikali yao kama ambavyo Katiba yetu imetuelekeza, basi ni vyema Ugatuzi ukaendelezwa na kusimamiwa. Aidha, Kamati inaiomba Serikali ifikiriekugatua pia sekta ya maji ili kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama ambazo inajitokeza katika Halmashauri mbali mbali hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa dhana ya Ugatuzi ni njema na inaleta ufanisi kwa watendaji, Kamati inapongeza sana juhudi za Serikali katika kusimamia vyema Ugatuzi katika Taasisi zilizogatuliwa na kupelekwa Halmashauri. Aidha, Kamati imeridhishwa na Wizara ambazo zimegatua watumishi wao kikamilifu na kuwapeleka Mamlaka ya Serikali za Mitaa ikiwemo Wizara ya Afya na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali. Hata hivyo, Kamati haikuridhika na mpango wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi kwa kuchelewesha kupeleka Stahiki za watumishi wake walioko Halmashauri na hivyo kushindwa moja kwa moja kuonekana kwa Bajeti yao katika fedha za Matumizi Kutoka Wizarani kwenda katika Halmashauri zao, hadi tunajadili na kupitisha bajeti hii kwenye Kamati, Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi imehamisha mishahara tu bado stahiki nyengine kama vile fedha za likizo, mchango wa ZSSF na matumizi mengine (OC). Hivyo, Kamati inaiomba Wizara ya Fedha na Mipango kuingilia kati ili fedha hizo zipelekwe Wizara ya Nchi (OR) Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ katika mwaka wa fedha 2018/2019.

Aidha, Kamati inashauri Wizara kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali za Mitaa kutoa uelewa juu ya matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo kwa Waheshimiwa Madiwani juu ya namna ya kutumia fedha za miradi kama sheria zinavyoelekeza.

Mheshimiwa Spika, Kamati imebaini katika mwaka huu wa fedha kuwepo kwa changamoto kubwa ya kukosekana kwa Hatimiliki katika baadhi ya maeneo ya uzalishaji pamoja na majengo ya ofisi, jambo linalopelekea maeneo hayo kutotambulika kisheria kwa maeneo hayo na hivyo kupelekea baadhi ya mapato kupotea. Hata hivyo, Kamati imeelezwa kuwepo kwa agizo la Serikali la kupatiwa Hati kwa maeneo yote yanayomilikiwa na Halmashauri za Unguja na Pemba pamoja na kupatiwa Hati za Madiko yaliyomo katika Halmashauri hizo na kuleta taswira njema kwa Serikali yetu ambayo kila siku ipo katika harakati za kuhakikisha suala la ukusanyaji mapato limeimarika.

Mheshimiwa Spika, Kamati inashauri Baraza la Mji Wete pamoja na Halmashauri ya Micheweni kuhakikisha zinaongeza nguvu ya ukusanyaji wa mapato ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa ulipaji kodi na kuwachukulia hatua wale wote wanaokwenda kinyume na agizo la ulipaji kodi na hivyo, kupelekea mapato ya Taasisi hizo kushuka ingawa katika kipindi hiki inaonekana Baraza la Mji Wete likipiga hatua ya ukusanyaji ila juhudi hizo zinahitaji kulindwa na kuimarishwa.

Mheshimiwa Spika, Kamati yangu inaliomba Baraza lako tukufu kuidhinisha kiasi cha fedha zilizotengwa kwa ajili ya uendeshaji wa programu zote zilizopangwa katika Tawala za Mikoa pamoja na Mamlaka ya Serikali za Mitaa ili kusaidia kufikia malengo yaliyokusudiwa.

PROGRAMU ZA IDARA MAALUM ZA SMZ (FUNGU D 02 – D 06)
Mheshimiwa Spika,  Kamati inapongeza sana juhudi zinazofanywa na wapiganaji wetu wa vikosi kwa kazi nzito wanazozifanya za kulinda, kusimamia na kudumisha usalama wa raia na mali zao pamoja na kuhakikisha kuwepo kwa amani na utulivu katika nchi yetu. Sambamba na hayo, Kamati imeridhika kwa kiasi kikubwa hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa Mahanga ya Askari kisiwani Pemba, juhudi hizo za Serikali zinaonekana kutia moyo kwa kuona kuwa Serikali inawajali na kuwathamini vijana wetu na vile vile, Serikali kutekeleza kwa vitendo ahadi zake zilizotolewa katika Ripoti ya Kamati na Bajeti ya mwaka 2017/2018, Kamati pia, inaiomba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ifikirie kuijenga kwa kiwango cha lami Barabara ya kutoka Kama meli kumi hadi Kambi ya KMKM kama ambayo inatarajiwa kujengwa Chuo cha Kijeshi kwa Vikosi vyetu vya SMZ.

Mheshimiwa Spika, Kamati imebaini kuwepo changamoto ya kuwekewa kiwango kikubwa cha Makadirio ya Mapato kwa vikosi vya Idara Maalum ambapo kila kikosi kimetakiwa kukusanya mapato kama inavyoonekana katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Hivyo, Kamati inaitaka Wizara ya Fedha wakati wanapofikiria upangaji na Makadirio ya ukusanyaji wa Mapato kwa Idara Maalum wafikirie na vyanzo vyao vya Mapato na vile vile wazingatie kazi za msingi zinazotekelezwa katika Idara hizi, kwa mfano Kikosi cha Valantia Zanzibar kimekasimiwa kukusanya jumla ya shilingi 60,259,000.00 ambazo zitaenda katika mfuko mkuu wa Serikali hali ambayo ni vigumu kukusanya fedha hizo kutokana na ukoksefu wa vyanzo vya mapato lakini pia uchache wa wataalamu na rasilimali ziliomo katika kikosi hiki zinachangia kutofikiwa kwa malengo.

Mheshimiwa Spika, aidha, Kamati inaishauri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Fedha kupunguza au kuondosha kabisa Makadirio ya Mapato ya shilingi 70,991,000.00/- kwa mwaka wa fedha 2018/2019 kwa Idara ya Chuo cha Mafunzo ambao wakati wote nguvu zao zipo katika ujenzi wa Mahanga ya Askari na Nyumba za Maafisa na vile vile wanaendelea na ujenzi wa gereza la watoto – Hanyegwa Mchana, hivyo hakuna chanzo chengine chochote cha mapato ambacho kitatumika kukusanyia fedha hizo. Pia, Kikosi cha Valantia kimepangiwa kuchangia shilingi 60,259,000/- toka fungu la ada ya ulinzi, hata hivyo, kwa mujibu wa maelezo yao kazi hiyo sasa itafanywa na Wakala wa Ulinzi wa JKU.

Mheshimiwa Spika, Kamati pia haikuridhika na kiwango cha Mapato ambacho Kikosi cha Zimamoto na Uokozi wamepangiwa kukusanya ambacho ni jumla ya shilingi 74,184,000.00 kiwango hicho ni ikubwa na Kikosi hiki hakina uwezo wala vyanzo vya kupata mapato hayo. Kati ya fedha waliopangiwa Kikosi cha Zimamoto, shilingi 25,000,000/- ni ada ya ulinzi na shilingi milioni 3 ni ada ya ujenzi, shughuli ambazo hazipo kwa mwaka huu wa fedha.

Mheshimiwa Spika, Kamati kwa mara nyengine tena imesikitishwa na baadhi ya Taasisi za Serikali kukataa kutekeleza maagizo ya Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt Ali Mohamed Shein la kuwaimarishia Kikosi cha Zimamoto huduma zao katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, ikiwemo ujenzi wa Banda la kuhifadhia gari zao za Zimamoto eneo la Uwanja wa Ndege wa zamani pamoja na kuwapatia maji katika hodhi lao liliopo katika kituo cha kipya uwanjani hapo na kuifanyia matengenezo barabara ambayo inatumiwa na magari ya Zimamoto kiwanjani hapo.

Aidha, Kamati inaishauri Wizara ya Tawala za Mikoa kukaa na Wizara nyengine kuangalia jinsi ambavyo Zimamoto watapata mgao wao kutokana na huduma wanazotoa katika Taasisi mbali mbali hasa uwanja wa Ndege wa Kimataifa, kama ilivyo kwa upande wa Tanzania Bara na nchi nyenginezo Ulimwenguni.

Mheshimiwa Spika, Kamati inapongeza juhudi za kuanzishwa kwa Ofisi ya Wakala wa Ulinzi wa JKU ambapo majukumu ya ofisi hii yameainishwa kwa mujibu wa Sheria namba 2 ya mwaka 2015 na itafanya kazi za ulinzi katika sekta mbali mbali ikiwemo mashirika na watu binafsi, ni imani ya Kamati yangu kuwa ofisi hii itaimarisha ulinzi na usalama wa mali za raia na wageni wanaowekeza katika nchi yetu. Hata hivyo, katika kufikia malengo yake, Kamati inashauri Serikali iangalie uwezekano wa kupatiwa fungu lao la fedha ambalo litawawezesha kujitegemea wenyewe kwa mujibu wa majukuu yao.

Aidha, Kamati inashauri Wajumbe wa Baraza hili tukufu kuridhia na kuidhinisha fedha za ruzuku zilizopangwa kwa ajili ya Ofisi hii ili ipate kwenda sambamba na malengo yaliyokusudiwa.

Mheshimiwa Spika,  kwa nyakati tofauti Kamati imekuwa ikizungumzia suala la Hatimiliki kwa maeneo yanayokaliwa au kutumiwa na vikosi vya Idara Maalum za SMZ kwa shughuli mbali mbali ikiwemo ulinzi na usalama wa raia na mali zao. Kwa kuwa suala hili limekuwa na ukakasi katika utekelezaji wake kwa Bajeti iliyopita lakini pia, na Bajeti hii tuliyonayo; Kamati inashauri Serikali kupitia Idara ya Ardhi kufuta baadhi ya viwanja ambavyo vimetolewa na Serikali kwa makazi ya watu na vipo karibu na maeneo ya Kambi hususan katika Kambi ya Ndugukitu kisiwani Pemba amabapo kwa kiasi kikubwa hupelekea wakaazi wa maeneo hayo kukwaza shaughuli mbali mbali za askari wetu.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kilimo ni uti wa mgongo na kwa kuwa kilimo ndio msingi mkuu wa maendeleo katika nchi yoyote, Kamati inashauri Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi itakapopata miradi ya Kilimo pia iwashirikishe na kuviwezesha kitaalamu na kifedha Vikosi vya JKU na Mafunzo katika kuendesha miradi yao ya Kilimo kwa mashamba yote yaliyochini ya vikosi hivyo yanatumika kwa ajili ya uzalishaji wa chakula na mboga mboga.

WAKALA WA USAJILI WA MATUKIO YA KIJAMII (FUNGU D 12)
                                                                               
Mheshimiwa Spika, Wakala wa Usajili na Matukio ya Kijamii inalo jukumu kubwa la kuimarisha mfumo wa Usajili wa Matukio ya Kijaamii katika nchi yetu na ni Taasisi pekee ambayo tunaitegemea kwa ajili ya kutunza takwimu sahihi za jamii yetu. Katika ziara zilizopita, Kamati imebaini kuwepo kwa changamoto kubwa ya ucheleweshwaji wa kutolewa vyeti vya kuzaliwa katika Wilaya zote za Unguja na Pemba.

Kamati inashauri Serikali kwa Bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali kupitia Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii kuhakikisha kwamba inaweka miundombinu rafiki na mazingira rahisi katika kutoa vyeti vya kuzaliwa katika ofisi za Wilaya zote Unguja na Pemba kwa kuzingatia utaratibu unaofaa.

HITIMISHO
                           
Mheshimiwa Spika, katika Bajeti hii ambayo inatumia mfumo wa PBB (Program Based Budget) ina utaratibu wake mzuri ambao tumeshauzoea Waheshimiwa Wajumbe wote kwa wale wazoefu wa siku nyingi humu Barazani lakini pia na wale wapya wameshauzoea mfumo huu. Kwa maana hiyo lipo tatizo la kubadilisha vipengele vilivyomo ndani ya Mfumo huu kwa kuzingatia programu kuu na programu ndogo jambo ambalo limewakwaza sana Wajumbe wakati wa upitiaji wa Bajeti hii katika Kamati. Kamati inashauri wakati Wizara ya Fedha wanapofanya mabadiliko ndani ya Mfumo huu tuliouzoea katika kupitia Bajeti basi watoe taarifa kwa Wajumbe ili kuzuia hoja zitakazojengwa dhidi ya mabadiliko hayo.

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia, nachukua fursa hii kuiomba jamii katika kipindi hiki cha mvua za masika zinazoendelea kunyesha kuzidi kuweka usafi katika mazingira yetu kwa kuitunza michirizi ya maji ya mvua na kuepuka kutupa taka kiholela katika kila sehemu ndani ya miji yetu, kufanya hivyo kutasaidia kujikinga na maradhi ya mripuko na malaria ambayo ni hatari kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, pia, naomba niwashukuru Makamanda wa Idara Maalum za SMZ, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wilaya, Wakurugenzi, Madiwani, Masheha na watendaji wote wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ kwa utendaji wao, uzalendo wao na mashirikiano yao katika kutekeleza majukumu ya Kamati yetu katika kipindi chote cha maisha ya Kamati hii.

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, Kamati inawaomba Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako Tukufu waichangie Bajeti hii na hatimae waidhinishe Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, makadirio ya fedha zilizopangwa kutumiwa kwa mwaka wa fedha 2018/2019.

Mheshimiwa Spika,        Naomba Kuunga Mkono Hoja.

Ahsante,
 Machano Othman Said,     
Mwenyekiti,
Kamati ya Sheria, Utawala Bora na Idara Maalum,
Baraza la Wawakilishi,

Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.