Habari za Punde

Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mhe. Mohammed Raza Darams Akabidhi Vifaa kwa Ajili ya Skuli ya Sekondari Uzini

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi akikabidhiwa Printa na Fedha kutoka kwa Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Zanzibar Mhe.Mohammed Darams Raza Hassanali, kwa ajili ya Skuli ya Sekondari ya Uzini Wilaya ya Kati Unguja,wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Tawi la Chama cha Mapinduzi Mpapa Mkoa wa Kusini Unguja.(Picha na OMPR) 
Na. Othman Khamis OMPR.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi alisema Wana CCM wana dhima kubwa ya kuhakikisha ushindi wa Chama hicho ni lazima kwenye Chaguzi zote katika muelekeo wa kuiona Tanzania inaendelea kubakia kuwa Kisiwa cha Amani Duniani.
Alisema Katiba na Ilani ya CCM imeweka wazi kipengele hicho cha ushindi kinacholinda Heshima ya Wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania kwa Ujumla ili kuepuka Taifa kurejea tena katika madhila ya kutawaliwa yaliyowapata Wazee wakati wa harakati za kuikomboa Nchi hii.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Viongozi na Wanachama wa CCM wa Jimbo la Uzini, Wilaya ya Kati pamoja na Mkoa wa Kusini Unguja mara baada ya kulizindua Rasmi Jengo Jipya la Tawi la CCM Mpapa lililojengwa na Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mh. Moh’d  Raza Hassanali.
Alisema ushindi wa Chama cha Mapinduzi umo ndani ya mikono ya Wanachama wenyewe pamoja na nguvu za Wananchi wanaoendelea kuzikuibali Sera na Ilani za Chama hicho kuanzia Mashina hadi Taifa.
Balozi Seif  alisema katika kuimarisha Uhai na nguvu za Chama kupitia ngazi zote aliwakumbusha Wanachama kuacha tabia ya kufanya vikao kwa nadra jambo ambalo hupelekea baadhi ya Matawi kufungwa kwa muda mrefu kitendo ambacho ni kinyume na Katiba ya Chama hicho.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM alisema Vikao vya Chama lazima vifanyike ndani ya Ofisi na Matawi ya Chama ili kuwapa fursa na haki Wanachama kutoa mawazo yao kwa mujibu wa Katiba, kinyume chake ni kukaribisha fitna na majungu.
Alisema nia ya kuimarisha Chama kwa wakati huu inakwenda sambamba na ujenzi wa Majengo yake yenye hadhi inayokubalika na chama chenyewe ambacho kwa sasa hakina muda kwa Wanachama wake kufanya Mikutano na Vikao chini ya Miti.
Balozi Seif alimpongeza Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mh. Moha’d Raza kwa uamuzi wake wa Kizalendo wa kujenga Matawi ya Kisasa ya Chama ndani ya Jimbo analoliongoza akiwapa Faraja Wanachama hao wa Chama cha Mapinduzi wakati wanapoendesha Vikao vyao kwa utulivu na raha.
Alifahamisha kwamba Mheshimiwa Raza amekuwa mfano wa kutekeleza Sera na Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2015/2020 sambamba na ahadi alizozitoa wakati wa Kampeni ya kuomba kuwatumikia Wananchi wa Jimbo la Uzini.
Akigusia tabia ya baadhi ya Wanachama hasa Vijana ya kuamua  kutishia Viongozi kurejesha Kadi za Chama kwa kigezo cha kutaka kutatuliwa haraka changamoto zao Balozi Seif alisema ni vyema kitendo hicho kikapigwa vita na kuachwa mara moja kwa vile kinaitoa thamani Kadi ya Chama.
Alisema Mwanachama ye yote anayekiamini Chama chake kamwe hawezi kufanya kitendo hicho kinachoonyesha kutopevuka kimaadili kwa baadhi ya Watu wakati kipindi kilichopita  nyuma Mwanachama lazima aingie darasani Miezi Mitatu kabla ya kupewa Kadi ya Chama.
“ Tunapotaka  kukitia thamani Chama chetu  wanachama Wapya lazima waache tabia ya kununuliwa Kadi jambo ambalo watakuwa wameuza na kununuliwa Utu wao”. Alisema Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa.
Alisisitiza kwamba CCM ni Chama Kikubwa na Kikongwe chenye hadhi na Heshima yake kamili ndani na nje ya mipaka ya Tanzania. Hivyo Wanachama wake wasingependa kuharibiwa Taasisi yao ya Kisiasa na Watu wachache kwa kuendekeza tamaa zao binafsi.
Balozi Seif amewatahadharisha Wananchi hasa Vijana kuepuka kununuliwa Kadi za Chama na Baadhi ya Wanachama wenzao wenye nia ya kugombea nafasi mbali mbali za Uongozi ambapo hatma yake wahusika wa tabia hizo hujenga jeuri na kiuburi na kufikia hatua ya kutoa kauli chafu kwamba fedha zao ndizo zilizowaweka madarakani.
Akisoma Risala ya Wanachama  na Viongozi wa Tawi la CCM Mpapa Kiongozi wa Tawi hilo ambae pia ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Kati  Ndugu Othman Ali Maulid alisema Uongozi wa Tawi umeshapanga Programu tofauti za kuimarisha  kazi za Chama Tawini hapo.
Nd. Othman alisema nguvu ya Chama ni kutambua changamoto za Vijana ambapo kwa namna ya pekee Viongozi wa Tawi na Jimbo la Uzini wameamua kuwakusanya katika Vikundi vya ujasiri amali ili wapate Taaluma itakayowasaidia kuendesha maisha na Familia zao kwa ujumla.
Mapema Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mheshimiwa Moh’d  Raza Hassanali akitoa Taarifa ya Ujenzi huo alisema Jengo hilo Jipya la Ofisi ya CCM Tawi la Mpapa  uliogharimu shilingi Milioni 61,000,000/- na kufanywa ndani ya kipindi cha  Miezi Mitatu mnamo Mwaka 2016 ni utekelezaji wa Ahadi alizozitoa wakati wa Kampeni ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015.
Mh. Raza alisema ushirikiano wa karibu uliyoonyeshwa kati ya Viongozi , Wanachama wote wa CCM pamoja na Wananchi wengi ndio uliofanikisha kukamilika kwa haraka malengo ya kuimarisha Chama ndani ya Jimbo hilo likiwemo jengo hilo.
Alitahadharisha kwamba Kiongozi atakayechaguliwa na Wananchi lazima atimize Uzalendo wake kwa kuwatumikia Wananchi waliomchaguwa huku akiwaasa Wananchi hao kuepuka hadaa za baadhi ya watu wanaowashawishi wawachague na hatimae kujaza matumbo yao bila ya kujali Heshima waliyowapa.
Akitoa salamu za Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Kati Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya hiyo Nd. Hassan Mrisho alisema Wanachama wa CCM wanaendelea kupata faraja kuona Viongozi wa Majimbo wanatekeleza Ilani ya Chama kwa asilimia inayoridhisha.
Nd. Hassan alikumbusha kwamba Tawi la Chama cha Mapinduzi la Mpapa  kwa wakati huo likiwa chini ya Uongozi wa Chama cha ASP ni chimbuko la kwanza la hamasa ya kuwajengea ari ya UmojaWananchi iliyosababisha kuzaliwa kwa Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964.
Alisema hilo linathibitishwa na msimamo wa Wanachama wake kitendo cha kulisababishia Jimbo la Uzini kuwa la kwanza kuongoza katika Ushindi wa asilimia Kubwa ikilingankishwa na Majimbo mengi na Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Ndugu Hassan Mrisho alijigamba na kuweka msimamo kwamba Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Kati hakitakuwa tayari kuona sifa hiyo kubwa ya mafanikio ya Jimbo la Uzini inachafuliwa na wadokozi wachache.
Katika Mkutano huo wa Uzinduzi wa Tawi Jipya la Chama cha Mapinduzi la Mpapa Mheshimiwa Raza alimkabidhi Balozi Seif   mchango wa Shilingi Milioni 19 na Laki Tisa  {19,600,000/- } alizozilenga kuwaongezea nguvu Wananchi waliounda Vikundi vya Ushirika.
Jumla ya Vikundi 97  vilivyokwisha sajiliwa kutoka Shehia  17 ndani ya Jimbo la Uzini vitafaidika na mchango huo ambapo kila Kikundi kitapata shilingi Laki 200,000/-  zitakazosaidia kutunisha mifuko yao katika kuendeleza miradi yao waliyojipangia.
Vikundi hivyo vya Ushirika vinatoka katika Shehia za Machui, Koani, Kidimni, Miwani, Ghana, Kiboje Muembe Shauri, Kiboje Mkwajuni, Mgeni Haji, Uzini, Mitakawani, Tunduni, Mchangani, Kijibwe Mtu, Bambi, Mpapa, Pagali pamoja na Umbuji.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.