Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) alipokuwa akizungumza na Waziri wa Mamlaka ya Saudi Arabia anayeshuhulikia Mambo ya Kiislamu,Daawa,Misaada na MiongozoMhe,Dk.Sheikh Saleh bin Abdul Aziz bin Muhammad bin Ibrahim Al Sheikh,(kushoto)alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo akifuatana na Ujumbe wake,(katikati) Mkalimani wa lugha) Sheikh Khalid Mohammed Mrisho
STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 30.05.2018

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa ziara ya Waziri wa Mamlaka ya
Saudi Arabia anayeshughulikia Mambo ya Kiislamu, Daawa, Misaada na Miongozo,
hapa Zanzibar ni muhimu kwa maendeleo ya
Zanzibar na Saud Arabia.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo katika mazungumzo kati yake na Waziri huyo wa Mamlaka
ya Saudi Arabia anayeshughulikia Mambo ya Kiislamu, Daawa, Misaada na Miongozo aliyefika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya mazungumzo na Rais.
Katika maelezo yake,
Rais Dk. Shein alieleza kuwa Saud Arabia na Zanzibar zina historia kubwa ya
mashirikiano na mahusiano kati ya pande mbili hizo huku akisisitiza kuwa historia
ya Uislamu inaonesha jinsi Uislamu ulivyoingia Zanzibar ambapo jamii nzima ya
Kiislamu duniani inaelewa suala hilo.
Dk. Shein alieleza
kuwa ziara hiyo ya kiongozi huyo pia, itaimarisha umoja na udugu wa muda mrefu
uliopo kati ya Zanzibar na Saudi Arabia na kueleza kuwa Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar pamoja na wananchi wake watauendeleza umoja huo.
Aidha, Rais Dk. Shein
alieleza kuwa historia ya elimu hasa elimu ya dini ya Kiislamu hapa Zanzibar haiwezi
kutolewa bila ya kuhusishwa Saudi Arabia kwani ni nchi ambayo Mashekhe na
Maulamaa wa Zanzibar walipata elimu hiyo nchini humo hasa katika mji wa Madina.
Dk. Shein alieleza
kuwa mnamo miaka ya sabini Mashekhe na Maulamaa wengi wa Zanzibar walipata
fursa hiyo ya kupata elimu ya dini ya Kiislamu nchini humo na kuifanya Zanzibar
kuwa na hazina kubwa ya viongozi hao wa dini ya Kiislamu.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein alieleza kuwa mbali ya sekta ya elimu Saudi Arabia imesaidia kuiunga
mkono Zanzibar katika kuimarisha miradi ya maendeleo ukiwemo ujenzi wa
miundombinu mbali mbali kama vile jengo la Baraza la Wawakilishi la Zanzibar,
Msikiti wa Mwembeshauri pamoja na mradi wa ujenzi wa barabara huko kisiwani
Pemba kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (BADEA).
Pia, Rais Dk. Shein
alieleza kuwa hivi karibuni kuna msaada mkubwa wa ujenzi wa Hospitali ya
MnaziMmoja kutoka nchini humo kwa mashirikiano ya BADEA na Kuwait.
Rais Dk. Shein pia,
aliipongeza azma ya Saudi Arabia kutaka kujenga Chuo Kikuu cha Kiislamu hapa
Zanzibar ambapo pia, Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuiomba Saudi Arabia
kufungua Ubalozi wake mdogo hapa Zanzibar kama ilivyo kwa baadhi ya nchi kama
vile China, India, Misri, Msumbuji ambazo zina ubalozi mdogo hapa Zanzibar.
Pamoja na hayo, Rais
Dk. Shein alipokea salamu za pongezi kutoka kwa Mfalme wa Saudi Arabia, Salmani
bin Abdulzaziz al Saud pamoja na pongezi kutoka nchi hiyo kutokana mwenendo
mzuri wa Mahujaji wa Zanzibar wanaokwenda kufanya Ibada ya Hijja nchini Saudi
Arabia.
Nae Dk. Sheikh Saleh bin
Abdul Aziz bin Muhammad bin Ibrahim Al Sheikh, Waziri wa Mamlaka ya Saudi
Arabia anayeshughulikia Mambo ya Kiislamu, Daawa na Miongozo alimueleza Dk.
Shein kuwa ziara hiyo imefungua mahusiano mazuri kati ya nchi hiyo na Zanzibar
kupitia Wizara yake ya Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na
Utawala Bora pamoja na Ofisi ya Mufti Mkuu ya Zanzibar.
Waziri Dk. Sheikh Saleh
alitumia fursa hiyo kutoa salamu za Mfalme Salman kwa Dk. Shein pamoja na
kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutokana na miongozo mizuri
inayotoa kwa Mahujaji wake wanaokwenda kuhiji nchini humo.
Alieleza kuwa Mahujaji
wa Zanzibar wamekuwa wakifanya Hijja zao vyema na kufuata taratibu na miongozo
yote muhimu pamoja na kuonesha tabia njema wakati wakifanya ibada yao hiyo
nchini humo.
Aidha, Waziri huyo
alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa vipaumbele vyote vilivyoelezwa na Zanzibar kwa
Saud Arabia atavifanyia kazi kwa kufikisha kwa Mfalme Salman pamoja na Msaidizi
wake ili kufanyiwa kazi.
Kiongozi huyo
alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa ziara yake hiyo haitokuwa ya mwanzo wala ya
mwisho kwani amependezewa na mazingira mazuri ya Zanzibar kutokana na vivutio
kadhaa vilivyopo huku akiahidi kuwa Saudi Arabia itaendelea kuiunga mkono
Zanzibar katika kuimarisha na kuendeleza miradi ya maendeleo.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment