NA ZUHURA JUMA, PEMBA
WAKULIMA wa zao la karafuu Wilaya ya Wete wamesema wana
mashaka na sheria ya karafuu namba 2 ya mwaka 2014 pamoja na kanuni zake,
kutokana na baadhi ya vipengele vya sheria hiyo kumkandamiza mkulima.
Wakizungumza
katika mkutano wa kutathmini zao la karafuu katika Ukumbi wa Baraza la
Wawakilishi Wete, baadhi ya Wakilima walisema kutokana na Serikali kutegemea zao
hilo kwa kiasi kikubwa, ni vyema kuangalia upya sheria hiyo, ili kuweza kumsaidia
mkulima.
Walisema
kuwa, kumekuwa na baadhi vipengele ndani ya sheria hiyo ambavyo vinamkandamiza
mkulima katika kuendesha shughuli zake za kilimo cha zao la karafuu, jambo
ambalo linawasababishia vikwazo vikubwa mbali mbali, ikiwemo kupata hasara.
“Kwa
kweli sheria sio rafiki kwetu hasa hii ya kuhamisha karafuu kutoka sehemu moja
kwenda nyengine inatukwaza wakulima, maana wengine mashamba yetu yako kwenye
Wilaya nyengine na sisi tupo kwengine”, walisema wakulima hao.
Mkulima
Mussa Ali Mussa mkaazi wa Kiuyu Minungwini alisema bado sheria ya zao la karafuu
zinawakwaza wakulima, hivyo ni vyema kwa serikali kupitia shirika hilo kuzirekebisha
ili kuweza kwenda sambamba na wakulima.
“Mimi
nakaa Wilaya ya Wete, lakini shamba langu lipo Wilaya ya Mkoani na huko hakuna
eneo la kuanikia, hivyo ilinisababishia kupata hasara kubwa kutokana na karafuu
zangu kukosa hua”
Nae
mkulima, Bimkubwa OmarAmour mkaazi wa shehia ya Bopwe Wete, aliiomba Serikali
kuwatafutia maeneo rasmi ya kuanikia karafuu zao, ili kuweza kuepusha zao hilo
kuharibika.
“Karafuu
zangu naanika pembeni mwa barabara na wakija Wizara husika wananiambia niziondoshe
na kama sikuziondosha watanitolesha faini, hivi tunaelekea wapi maana tumekuwa
tukihangaika ili tupate karafuu zinazotakiwa lakini kwa hali hii kila siku
karafuu zetu zitaharibika”, alisema mama huyo.
Aliiomba
Serikali kuzitazama upya sheria zinazomkwaza mkulima wa karafuu, ili kuepusha
changamoto wanazozipata wakati wa kuchuma zao hilo.
Mwanasheria
kutoka shirika la ZSTC, Ali Hilal Vuai, alisema kuwa, watachukua juhudi za
kuziangalia upya sheria hizo, ili kuepuka changamoto zilizopo kwenye vifungu
hivyo, ikiwemo ile ya uhamishaji wa karafuu kutoka sehemu moja kwenda nyengine.
Akichangia
mada ya uadilifu katika zao hilo, Jabu Mbwana Said kutoka shehia ya Kinyasini, alisema
kuwa kuna baadhi ya wapimaji wa zao hilo
wamekosa uadilifu wakatika wa kupima karafuu zinazokwenda kuuzwa, jambo mbalo
linawatia huzuni wakulima hao kila wanapofikiria.
“Mimi
binafsi yangu nishakwenda nikaambiwa na sisi tunakata chetu, hivyo inauma sana
kwani mimi ndie niliepata shida ya kulishughulikia zao hili, hivyo shirika
liwape mafunzo ya uadilifu watendaji wao, ili kuepusha kumnyonya mkulima”, alisema mkulima huyo.
Nae
Mkuu wa Wilaya ya Wete, Abeid Juma Ali, alilipongeza Shirika la Biashara la
ZSTC pamoja na wakulima kwa juhudi yao ya kuuzia karafuu zao katika vituo vya
kununulia zao hilo, ambapo kwa msimu huu wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa.
“Juhudi
zenu ndio mafanikio ya zao letu na nchi kwa ujumla, hivyo muendelee, ili kukuza
uchumi wetu”, alisema Mkuu huyo.
Mkutano
huo wa tahmini kwa zao la karafuu kwa msimu wa mwaka 2017/2018 ,kwa wakulima wa
karafuu ulifanyika katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Wete Pemba.
No comments:
Post a Comment