Habari za Punde

Hutuba ya Bajeti ya Matumizi na Mapato ya Wizara ya Afya Zanzibar.

Khadija.Khamis.Maelezo.
Waziri wa Afya Mhe.Hamad Rashid Mohamed amesema Wizara yake imejipanga  kuhakikisha maradhi ya malaria yanamalizika hasa katika maeneo ambayo bado maambukizo ya ugonjwa huu yameripotiwa.
Hayo aliyasema wakati akisoma Hotuba ya  Bajeti ya Wizara ya Afya kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo ya mwaka 2018 hadi 2019 huko katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi chukwani .
Alisema katika kuhakikisha huduma za kinga zinapatikana wizara imekusudia kuhamasisha jamii juu ya usafi wa mazingira ili kujikinga na maradhi mbalimbali yakiwemo malaria,  maradhi ya kuharisha na kipindupindu .
Aidha alisema Wizara imekusudia kuhamasisha jamii juu ya masuala ya Afya kwa  kuendesha programu ya Afya maskulini pamoja na  kufuatilia mienendo ya maradhi ili kuweza kubaini mapema uwepo wa maradhi na kushukuwa tahadhari zinazostahiki.
Alifafanua wizara imekusudia kuimarisha huduma za kinga kwa maradhi mbalimbali yanayoambukiza na yasiyoambukiza na kuendeleza kudhibiti maambukizo ya maradhi ya ukosefu wa kinga mwilini ( VVU).
Alifahamisha katika jitihada hizo zinatarajiwa kuimarisha  huduma za afya ya  mama na mtoto ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vya watoto wachanga kwa kuengeza kiwango cha chanjo kwa watoto walio chini ya umri wa  miaka miwili kufikia zaidi ya asilimia 90 na kutoa chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi kwa watoto wa kike wenye umri wa miaka tisa hadi 14
Waziri huyo alieleza kuwa wizara imekusudia kutekeleza mkakati  wa kitaifa wa kudhibiti maradhi unaoitwa International Health Regulation (IHR) pamoja na kuipa kipaombele kauli mbiu iliyowekwa MATIBABU BURE NI HAKI YA KILA MTU .
Aidha alisema katika kutekeleza mipango mbalimbali ya wizara hiyo imeomba kuidhinishiwa matumizi ya shilling 93,253,000,000 kwa  matumizi ya kawaida, matumizi ya maendeleo na mapato  ya wizara ya afya .
MWISHO
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.