Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balizi Seif Ali Iddi Akabidhi Msaada wa Masine ya Boti Kwa Kikundi cha Hamasisha

Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi Kushoto akimkabidhi Mashine ya Boti Katibu wa Kikundi cha Hamasisha cha Jimbo la Mahonda Bibi  Mwanapatima Othman Salum kwa ajili ya shughuli za Uvuvi za Kikundi hicho.Kati kati yao ni Mkuu wa Nidhamu wa Kikundi cha Hamasa Bwana Kichamu Haji Abdullah.
Mke wa Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Mama Asha Sul;eiman Iddi akitoa nasaha kwa Wanachama wa Kikundi cha Hamasa mara baada ya kukabidhiwa Mashine ya Boti hapo nyumbani kwae Kama.
Mkuu wa Nidhamu wa Kikundi cha Hamasa Bwana Kichamu Haji Abdullah kwa niaba ya wana kikundi wenzake akitoa shukrani kwa Mwakilishi na Mbunge wa Jimbo la Mahonda  kwa uamuzi wao wa kuwapatia  Boti pamoja na Mashine yake kwa ajili ya shughuli za Uvuvi.
(Picha na Hassan Issa OMPR)

Na.Othman Khamis OMPR.
Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Viongozi wa Jimbo hilo wataendelea kuwaunga mkono  Wananchi wao hasa Vijana na Akina Mama walioamua kujituma katika muelekeo wa kujitafutia Maendeleo ili kujenga hatma njema ya maisha yao.
Alisema misaada ya kuyawezesha Makundi hayo katika kuyapatia vifaa, mtaji sambamba na  maarifa itakuwa ikiendelea kila wakati kulingana na mahitaji halisi ya Wananchi ikilenga zaidi katika Vikundi vya Ushirika.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akikabidhi msaada wa  Mashine iliyoitanguliwa  na  Boti ya kuvulia Samaki  aliyoitoa kwa Kushirikiana na Mbunge wa Jimbo hilo Mh. Bahati Abeid Nassir kwa ajili ya Vijana wa  Kikundi cha Hamasa cha Jimbo la Mahonda chenye Mastakimu yake Kijiji cha Fujoni hafla iliyofanyika Nyumbani kwake Kama Kaskazini kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Alisema hakuna Tajiri au Kikundi cha Jamii kilichopata utajiri wa kushtukia  bila ya kufanya kazi za ziada katika kujitafutia riziki ambazo Wanakikundi hao watalazimika kufanya jitihada zitakazowawezesha kujikwamua kutoka  katika mazingira magumu ya maisha.
Balozi Seif  aliwatahadharisha Wanachama wa Kikundi hicho cha Hamasa kwamba msaada huo wa Boti na Mshine yake  usije geuka kuwa chanzo cha  kuleta mifarakano baina yao.
Aliwataka Wanakikundi hao wapatao 50 walio jinsia mbili tofauti  wafanye kazi kwa juhudi zao zote ili vifaa vya msaada waliopatiwa  viwezeshe kuzaa vyengine kwa lengo la kutanua mradi wao unaopaswa kuwa wa kudumu.
Aliwakumbusha  wana Hamasa hao kuzingatia uadilifu baina yao katika mfumo wa matumizi ya Fedha na kuepuka majungu yanayoweza kuwa chanzo cha mizozo inayoweza kuchipuka kutokana na faida itakayozalishwa.
Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameelezea faraja yake  kutokana na muelekeo wa Vijana walioacha dawa za kulevya  wa Kijiji cha  Fujoni na kupatiwa msaada wa Bot na Mashine kwa shughuli za Kiuchumi bado wanaendelea na  maisha yao kwa matumaini makubwa kwenye mradi wao wa Uvuvi.
Mapema Mke wa Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda  Mama Asha Suleiman Iddi  alikiahidi Kikundi hicho cha Hamasa kwa upande wa Akina Mama kufikiria kuwapatia Vifaa kwa ajili ya ukaushaji wa Dagaa litalokuwa likivuliwa na Vijana wa Kiume wa Kikundi hicho.
Mama Asha alisema  hatua hiyo itawajengea msingi imara utakaowawezesha kujitahidi kuwa nao ni miongoni mwa Wanakikundi hicho badala ya kusubiri kuletewa kila kitu nyumbani mfumo ambao umepitwa na wakati katika kanre ya sasa na mihangaiko ya Sayansi na Teknolojia.
Akitoa shukrani  kwa Niaba ya Vijana hao  Mkuu wa Nidhamu wa Kikundi hicho cha Hamasa  Bwana Kichamu Haji Abdullah  alisema kitega uchumi walichopatiwa  kitakuwa ni chanzo na fursa adhimu kwao itakayowasababishia kuacha tegemezi katika mazingira yao ya uwajibikaji wa kila siku.
Kichamu alisema yapo mambo yanayowakabili katika kazi zao za Kimaisha ikiwemo harakati za Kisiasa zikihitaji  nguvu za uwezeshaji kifedha ambayo kwa sasa itakuwa nadra kuwafuata Viongozi wao kwa vile wameshajengewa mazingira ya kuwajibika wao binafsi.
Mashine hiyo pamoja na Boti yake vilivyotolewa na Mwakilishi na Mbunge wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi na Mh. Bahati Abeid Nassir  vimegharimu jumla ya shilingi za Kitanzania Milioni 13,800,000/-.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.