Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ajumuika Katika Futari na Wananchi wa Jimbo Lake.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  Ali Iddi akiwa katika moja ya shughuli za Kidini Nchini.(Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Balozi Seif Ali Iddi alisema licha ya Serikali Kuu kuruhusu Wananchi kuendelea na mikusanyiko yao ya kawaida katika shghuli za Kijamii lakini bado aliwasisitiza Wananchi umuhimu wa kuendelea kutunza mazingira  safi kwenye maeneo yao.
Alisema Serikali ililazimika kuzuia mikusanyiko hiyo baada ya kubaini mfumko wa maradhi ya kuambukiza kama Kipindupindu katika kipindi kilichopita kulikosababishwa na baadhi ya Watu kudharau kuzingatia elimu ya Afya sambamba na usafi wa mazingira.
Balozi Seif Ali Iddi  ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda alisema hayo wakati akizungumza na baadhi ya Wawakilishi  wa Wananchi wa Vijiji vinavyounganisha Jimbo  la Mahonda baada ya kufutari nao pamoja kwenye Makaazi yake hapo Kama, Kaskazini kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliweka wazi kwamba uzuiaji huo wa Mikusanyiko ya Wananchi hasa katika masuala ya kula kwa pamoja hadharani haikukusudiwa kusumbua Jamii  kama baadhi ya Watu walivyokuwa wakitafsiri bali ilikuwa ni wajibu wake kufanya hivyo katika kuona dhamana ya Afya ya Wananchi iko juu ya Serikali.
Alisema Zanzibar tayari imeshashuhudiwa kukumbwa na maradhi ya Kipindupindu tokea Mwaka 1979 jambo ambalo umefika wakati kwa Wananchi wenyewe kwa kushirikana na Viongozi wao kukabiliana kwa nguvu zao zote miripuko inayotokea ili Zanzibar ibaki kuwa na Ustawi usioshaka.
Balozi Seif aliitahadharisha Jamii kuepuka tabia ya kukimbilia kwa Waganga wakati inapokumbwa na mitihani ya maradhi tofauti na badala yake waende moja kwa moja Hospitali na katika Vituo vya Afya ili kupata tiba na ushauri ulio sahihi.
Akizungumzia Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani unaoendelea Nchini huku Kumi la Pili la kuomba maghfira likimalizia Balozi Seif aliwaomba Waumini kuendelea kusameheana kwa makosa na hitilafu zilizoleta migongano miongoni mwao kwa lengo la kuelekea kwenye sifa za ucha Mungu.
Alisema tabia na mwenendo huo mwema unaoridhiwa ndani ya Uislamu Mwenyezi Muungu, Muumba wa vyote viivyomo Ardhini na Mbinguni  huwasamehe waja wake waliokubali kuondoa tofauti zao na kurejea katika kamba iliyonyooka.
Waumini wa Dini ya Kiislamu bado wanaendelea na Ibada ya Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramdhani wakilikaribia Kumi la Tatu la Kuachwa huru na moto likiambatana na Usiku wenye chezo pamoja na kushushwa na Kitabu Kitukufu cha Quran.
Funga ni Moja miongoni mwa Nguzo Tano za Kiislamu zinazomuwajibikia kila Muumini wa Dini ya Kiislamu aliyefikia umri wa Baleghe na akili timamu kuitekeleza vilivyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.