Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Mhe. Dkt Khalid Salum Mohammed akizingumza na Waandishi wa Habari wa Vyombo Mbalimbali Zanzibar Muelekeo
wa Bajeti ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
..Ndugu Waandishi wa Habari,
Ndugu wananchi mnaotusikiliza
1.
Kwanza kabisa, napenda nianze kwa
kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu mwenye ukarimu alietuwezesha kukutana tena
tukiwa wenye afya njema ili tuweze kuelezana kwa muhtasari kuhusu Mapendekezo
ya Mpango wa Maendeleo na Mwelekeo wa Bajeti kwa mwaka wa fedha 2018/2019.
HALI YA UCHUMI, 2017
2.
Pato la Taifa limeongezeka kutoka
thamani ya shilingi za kitanzania 2,628 bilioni mwaka 2016 hadi kufikia 3,099
bilioni mwaka 2017 kwa kutumia vigezo vya bei ya mwaka husika. Ukuaji halisi wa
uchumi umefikia asilimia 7.5 kwa mwaka 2017 Aidha, kwa ukuaji huo wa uchumi kumejitokeza
ongezeko la wastani wa Pato la Mtu binafsi kwa mwaka 2017 na kufikia Pato la
Kila Mtu la TZS 2,020,000 (USD 907) ikilinganishwa nawastani wa TZS 1,806,000 (USD
830) kwa mwaka 2016.
3.
Sekta ya kilimo imeongoza kwa
ukuaji katika Pato la Taifa na kufikia wastani wa asilimia 8.8 mwaka 2017
kutoka ukuaji wa wastani wa asilimia 6.3 mwaka 2016. Sekta ya Huduma nayo
imekua kwa wastani wa asilimia 8.2 mwaka 2017 kutoka wastani wa asilimia 7.2
mwaka 2016 na Sekta ya Viwanda imekua kwa asilimia 7.9 ikilinganishwa na
asilimia 9.7 mwaka 2016.
MFUMKO WA
BEI
4.
Kasi ya mfumko wa bei za bidhaa na
huduma nchini imeshuka hadi kufikia wastani wa asilimia 5.6 ikilinganishwa na
wastani wa asilimia 6.7 mwaka 2016. Kushuka huko kumesababishwa na kushuka kwa
mfumko wa bei za bidhaa za chakula, kuongezeka kwa uzalishaji wa ndani
kulikotokana na hali nzuri ya hewa pamoja na utulivu wa thamani ya Shilingi ya
Tanzania dhidi ya Dola ya Kimarekani.
MAPATO NA
MATUMIZI YA SERIKALI
5.
Katika mwaka wa fedha 2017/18 tunaoumalizia,
Serikali ilikadiria kukusanya jumla ya TZS 1,087.4 bilioni ikijumuisha, mapato ya
TZS 675.8 bilioni yanayotokana na vyanzo vya ndani. Kati ya fedha hizo, jumla
ya TZS 627.0 bilioni zilipangwa zitokane na makusanyo ya vyanzo vya kodi na TZS
48.8 bilioni zilitarajiwa kutokana na vyanzo visivyo vya kodi
6.
Kwa upande wa misaada kutoka nje,
jumla ya TZS 380.5 bilioni zilitarajiwa kukusanywa katika mwaka 2017/18. Kati
ya Fedha hizo, Ruzuku ilikuwa ni TZS 82.2 bilioni na Mikopo ni TZS 298.3
bilioni. Ili kuziba nakisi iliyojitokeza ya Bajeti Jumla ya TZS 30.0 bilioni
zilitarajiwa kukopwa katika soko la ndani.
UTEKELEZAJI
HALISI KWA MIEZI TISA (JULAI – MACHI,2018)
7.
Kwa kipindi cha miezi tisa mapato
halisi ya ndani yalifikia TZS 506.6 bilioni. Mapato kutokana na kodi yalifikia
TZS 465.2 bilioni na Mapato yasiyokuwa ya kodi yalifikia TZS 41.4 bilioni. Hadi Machi 2018, jumla ya TZS 20.0 bilioni
zimekopwa kupitia Hati Fungani, sawa na asilimia 66.7 ya makadirio ya mwaka.
8.
Katika kipindi cha mapitio (Julai –
Machi 2018), Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepokea Ruzuku na Mikopo kwa
ajili ya Miradi na Programu za Maendeleo iliyofikia TZS 151.0 bilioni.
9.
Kwa upande wa Matumizi, Serikali
ilikadiria kutumia jumla ya TZS 1,087.4 bilioni ikijumuisha, TZS 590.7 bilioni
kwa matumizi ya kazi za kawaida na TZS 496.6 bilioni kwa matumizi ya kazi za
maendeleo. Kati ya fedha hizo za
maendeleo, TZS 116.1 bilioni ni mchango wa Serikali na TZS 380.5 bilioni kutoka
kwa washirika wa maendeleo.
10.
Hadi kufikia Machi 2018, matumizi
halisi yalifikia TZS 681.6 bilioni sawa na asilimia 98 ya makadirio ya kipindi
hicho. Kati ya matumizi hayo TZS 457.1 bilioni zilitumika kwa kazi za kawaida
na TZS 224.5 bilioni kwa kazi za maendeleo.
DENI LA TAIFA
11.
Hadi kufikia Machi 2018, Deni la
Taifa limefikia TZS 519.7 bilioni, likimaanisha ukuaji wa asilimia 37.8 kutoka TZS
377.1 bilioni lililokuwepo mwezi Machi 2017. Katika kiasi hicho, deni la ndani limefikia
TZS 158.3 bilioni na deni la nje limefikia TZS 361.4 bilioni. Deni hilo ni sawa
na asilimia 16.8 kwa Pato la Taifa, hivyo, bado tuna kiwango kidogo cha
kudaiwa, deni letu linahimilika na tuna fursa zaidi ya kukopa tukihitaji, kwa
ajili ya kuharakisha maendeleo yetu
MWELEKEO WA UCHUMI NA BAJETI KWA MWAKA 2018/2019
12.
Kwa mwaka 2018, Pato la Taifa
linatarajiwa kukua kwa kasi ya wastani wa asilimia 7.7. Matarajio ya ukuaji wa
uchumi yatatokana na mambo yafuatayo:
i.
Kuendelea na juhudi za kuongeza uzalishaji wa
mazao ya chakula kwa ununuzi wa matrekta 20 mapya ambayo yatasaidia kuongeza
kasi ya uzalishaji wa ndani.
ii.
Kuongezeka kwa uhamasishaji wa uwekezaji wa
ndani na nje kwa kutekelezwa miradi mipya ikiwemo miradi ya ujenzi wa
miundombinu ya barabara, uwanja wa ndege na makaazi (Kwahani, Chumbuni) pamoja
na miradi binafsi ya uwekezaji katika maeneo ya Nyamanzi, Fumba, Mtoni na
Matemwe.
iii.
Kuongezeka kwa kiwango cha idadi ya watalii
wanaoingia nchini kutokana na kuendelea kuutangaza utalii na kupatikana kwa
masoko mapya.
iv.
Kuendelea kuwepo kwa amani na utulivu.
MAENEO
YA VIPAUMBELE KWA MWAKA 2018/19
13.
Kwa mwaka 2018/19, maeneo
yatakayopewa kipaumbele katika utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ni kama
yafuatayo:-
i.
Kuimarisha Miundombinu ya Maeneo ya Uingiaji
Nchini, Barabara na Nishati;
ii.
Kuendeleza sekta ya Utalii;
iii.
Kuimarisha Viwanda Vidogo Vidogo kwa Kuongeza
Thamani Bidhaa na Ubora wa Vifungashio;
iv.
Kuimarisha Kilimo kwa Kujenga Miundombinu ya
Umwagiliaji Maji, Uvuvi na Mifugo;
v.
Kuimarisha Ubora wa Huduma za Kijamii
zikiwemo Elimu, Afya, Michezo na Upatikanaji wa Maji safi na Salama;
vi.
Kukuza Uwezo wa Watu;
vii.
Utawala Bora,Uimarishaji wa Taasisi na
Uwekaji Mji katika Hali ya Usalama;
viii.
Ajira kwa Vijana;
ix.
Kuendeleza Tafiti.
MWELEKEO WA
MAPATO
14.
Kwa mwaka wa fedha 2018/19,
Serikali inatarajia kukusanya jumla ya TZS 1.315.1 trilioni zikiwemo TZS 807.5
bilioni zitokanazo na vyanzo vya ndani, TZS 464.2 bilioni kutoka kwa washirika
wa maendeleo, TZS 3.4 bilioni Mfuko wa wafadhili na TZS 40 bilioni mikopo ya
ndani.
Mapato ya Nje
15.
Kwa mwaka wa fedha 2018/19,
Serikali inatarajia kupokea jumla ya TZS 463.9 bilioni kutoka kwa washirika wa
maendeleo, zinazojumuisha Ruzuku ya TZS 77.6 bilioni na Mikopo ya TZS 386.3
bilioni.
MWELEKEO WA
MATUMIZI
16.
Serikali inakadiria kutumia jumla
ya TZS 1,315.1 bilioni katika mwaka wa fedha 2018/19 ikiwemo matumizi ya kazi
za kawaida ya TZS 702.2 bilioni na matumizi ya kazi za maendeleo ya TZS 612.9
bilioni.
HITIMISHO
17.
Nachukua fursa hii kuwashukuru kwa
dhati kabisa na kuwapongeza mmoja mmoja Washiriki wote wa Maendeleo kwa
kutimiza wajibu wao wa kutaka kusaidia katika Bajeti yetu. Nasi kwa upande wetu
tutaendelea kutimiza wajibu wetu wa kutekeleza bajeti hiyo ili kufikia malengo
tuliyokubaliana.
18.
Bajeti ya mwaka 2018/19 itaendana na
mambo muhimu matano ambayo yatatoa fursa kubwa ya kukuza uchumi na maendeleo ya
jamii ya Mzanzibari. Matumaini yangu
kuwa wananchi wa Zanzibar wataitumia fursa hiyo muhimu kwa nia ya kuimarisha
amani na kujenga Zanzibar yenye maendeleo makubwa ya kiuchumi na kijamii.
19.
Maeneo hayo ya fursa za kiuchumi ni
pamoja:
a)
Maendeleo ya viwanda (Industrial
Parks), kuendeleza wazalishaji wadogo wadogo pamoja na usarifu wa mazao ya
kilimo
b)
Upatikanaji wa ajira kwa vijana wetu
pamoja na jitihada mbali mbali ambazo Serikali itazichukua kukabiliana na
uchache wa fursa za ajira kwa vijana wetu.
c)
Utafutaji wa mafuta na gesi ambapo
Serikali itaendelea kuchukua hatua kadhaa ili kuendeleza zoaezi hilo pamoja na
kujitayarisha kitaalamu na kiuchumi kukabiliana na matokeo chanya ya zoezi
hilo.
d)
Kuendeleza miundombinu na Huduma za
Jamii ambapo Serikali imetenga kiasi kikubwa cha bajeti yake kuendeleza huduma
za Elimu, Afya, miundombinu na mawasiliano.
e)
Ugatuzi wa madaraka mikoani ambapo
huduma zitasogezwa zaidi kwa wananchi pamoja na kuwapa fursa za kujiendeleza kiuchumi
katika sehemu zao.
20.
Kazi kubwa itakayotukabili ni
uwajibikaji wetu pamoja na mashirikiano mazuri kati ya sekta ya umma na jamii
kwa jumla ili utekelezaji wa bajeti ijayo ufikie lengo lililokusydiwa. Ni
muhimu sana watendaji na wananchi wote kwa pamoja kuzidisha moyo na ari ya
maendeleo ili tufikie katika kiwango kizuri cha utekelezaji wa bajeti na hivyo
kufikia malengo yetu ya ukuaji wa uchumi tulioutarajia pamoja na ustawi wa
jamii kwa jumla.
Inawezekana,
tutimize wajibu wetu.
Ahsanteni
Dr. Khalid
Salum Mohamed
Waziri wa
Fedha na Mipango
Zanzibar
No comments:
Post a Comment