Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa Ussi Haji Gavu, akizungumza wakati wa kumuaga Afisa Mkuu wa (UNICEF) Zanzibar Bi Francesca Morandini aliyemaliza muda wake wa kazi hapa Zanzibar.Hafla hiyoimefanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Park Hayyt Shangani Zanzibar.
Afisa Mkuu wa (UNICEF) Zanzibar Bi Francesca Morandini aliyemaliza muda wake wa kazi hapa Zanzibar.akitowa neno la shukran kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa Ushirikiano wao wakati wote alipokuwa akifanya kazi zake Zanzibar kupitia Taasisi ya UNICEF, kulia Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Issa Haji Gavu.
Afisa Mkuu wa (UNICEF) Zanzibar Bi Francesca Morandini aliyemaliza muda wake wa kazi hapa Zanzibar.akizungumza na kutowa shukrani wakati wa hafla ya kumuaga iliofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Park Hayyt Shangani Zanzibar.
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imelihakikishia Shirika
la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto duniani (UNICEF) kuwa litaendelea
kuthamini mchango mkubwa wa Shirika hilo katika kuhakikisha watoto wa Zanzibar wanaendelea
kupata haki zao zote za msingi.
Waziri wa Nchi Ofisi
ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa Ussi Haji Gavu aliyasema hayo
huko katika ukumbi wa Hoteli ya Park Hayat, Shangani mjini Zanzibar wakati wa
hafla fupi iliyotayarishwa na Ofisi ya Rais kwa ajili ya kumuaga Afisa Mkuu wa (UNICEF)
Zanzibar Bi Francesca Morandini
aliyemaliza muda wake wa kazi hapa Zanzibar.
Katika maelezo yake
Waziri Gavu alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini sana
mashirikiano makubwa yaliopo kati yake na Shirika hilo huko akitumia fursa hiyo
kumpongeza na kumshukuru Afisa Mkuu huyo kwa mashirikiano yake katika kipindi
chote alichofanya kazi Zanzibar.
Alieleza kuwa katika
muda wake wote wa Kazi hapa Zanzibar, Afisa Mkuu huyo aliweza kutoa mashirikiano
mazuri kwa Wizara na Taasisi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar jambo ambalo
limeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kufikia malengo yaliokusudiwa.
Aidha, Waziri Gavu
alitumia fursa hiyo kumueleza Afisa Mkuu huyo wa UNICEF kuwa Serikali ya
Mapnduzia ya Zanzibar itaendelea kutoa ushirikiano wake kwa Shirika hilo pamoja
na mashirika mengine yote ya Umoja wa Mataifa kwa kutambua umuhimu wake mkubwa
katika maendeleo ya nchi pamoja na wananchi wake.
Nae Afisa Mkuu wa (UNICEF) Zanzibar Bi Francesca Morandini alitoa shukurani na pongezi kwa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi kwa kumuandalia hafla hiyo fupi ya kumuaga na kueleza kuwa tukio hilo
limeonesha wazi kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi inavyothamini juhudi za
Shirika hilo.
Hivyo, aliihakikishia
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa Shirika hilo la (UNICEF) litaendelea
kuiunga mkono Zanzibar katika juhudi zake za kujiletea maendeleo endelevu pamoja
na kuwahakikishia watoto wanapata haki zao zote za msingi.
Sambamba na hayo,
Afisa Mkuu huyo alizipongeza juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inazozichukua
katika kuwahudumia watoto kwa kuweka mikakati madhubuti ambayo imekuwa chachu
katika kuwaenzi, kuwalinda na kuwatunza watoto pamoja na akina mama wa Zanzibar
kwa jumla.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment