Habari za Punde

Trump ataka wahamiaji haramu watimuliwe haraka Marekani

Rais wa Marekani Donald Trump ametoa wito wa kuharakishwa kwa shughuli ya kuwatimua wahamiaji haramu nchini humo bila hata kufuata utaratibu wa mahakama.
Amefanya hivyo kupitia msururu wa ujumbe kwenye Twitter.
"Mtu anapoingia ndani, ni lazima mara moja, bila majaji na kesi mahakamani, tuwarejeshe walikotoka," Trump ameandika.
Amesema hayo siku chache baada yake kubatilisha sera ya kuwatenganisha watoto wa wahamiaji na wazazi wao baada ya sera hiyo kushutumiwa vikali Marekani na nje ya nchi hiyo.
Takwimu zinaonesha watoto 2,300 walikuwa wametenganishwa na wazazi wao kati ya Mei na Juni mwaka huu.
Kuanzia mwezi Mei, wahamiaji wanaovuka mpaka wa Marekani na kuingia nchini humo kinyume cha sheria wanakabiliwa na hatari ya kufunguliwa mashtaka ya jinai chini ya sera ya Trump ya kutowavumilia wahamiaji.
Rais Trump hajatofautisha kati ya wahamiaji wa kiuchumi na wale wanaotafuta hifadhi kutokana na mateso na kudhalilishwa mataifa yao.
Rais huyo amekuwa akishutumiwa hata na viongozi wa chama chake cha Republican kwa lugha kali aliyoitumia kwenye Twitter.
Aliposema awali kwamba wahamiaji wanatishia "kufurika na kuiambukiza nchi yetu, mbunge mwanamke wa chama cha Republican Ileana Ros-Lehtinen alimjibu kwenye Twitter akisema tamko lake halina msingi, "linakera" na linadunisha wale wanaotafuta maisha mazuri.
Maafisa wa uhamiaji Marekani wanasema watoto 2,342 walitenganishwa na wazazi 2,206 kati ya 5 Mei na 9 Juni.
Mnamo 20 Juni, Trump aililegeza msimamo wake wa kuunga mkono sera hiyo kali na badala yake akatia saini agizo la rais la kusitisha hatua hiyo ya kuzitenganisha familia.
Alisema wakati huo: "Huwa sipendi kuona au kusikia familia zikitenganishwa."
Agizo la Rais Trump linaruhusu kuzuiliwa kwa muda mrefu kwa watoto wa wahamiaji (ingawa wakiwa na watoto wao), jambo ambalo wengi wanasema linaenda kinyume na sheria za taifa ambazo haziruhusu watoto kuzuiliwa kwa zaidi ya siku 20.
Baada ya kuchaguliwa kwa Rais Trump mwaka 2016, idadi ya wahamiaji waliozuiliwa au kuzuiwa kuingia Marekani kwenye mipaka yake ilikuwa imeshuka pakubwa.
Hata hivyo tangu Februari 2018, idadi ya wahamiaji wanaovuka mpaka kinyume cha sheria imeongezeka pakubwa.
Idadi ya waliokamatwa mwezi uliopita ni zaidi ya maradufu ya idadi ya wahamiaji waliokamatwa Mei 2017.
Ingawa huwa vigumu kuhesabu idadi ya wanaoingia nchini humo kinyume cha sheria, idadi ya wanaokamatwa mipakani hutumiwa kama kiashiria cha idadi ya wanaovuka na kuingia Marekani kinyume cha sheria.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.