Habari za Punde

Mradi wa Partoma Waimarisha Huduma Katika Wodi za Mama Wajawazito Zanzibar.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya akina Mama na Watoto Zanzibar Dr. Salma Abdi Mahmoud, akizungumza wakati wa hafla ya kutowa shukrani na maelezo kuhusu Mradi wa kuimarisha Uzazi salama wa Mama wajawazito na Watoto katika semina ilofanyika Hotel ya Zanzibar Beach Resort Mjini Zanzibar. 
Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Dr. Jamala Adam Taib akimkabidhi Cheti Mshiriki wa Mafunzo  ya  Mradi unaotolewa na  Partoma Lamlat Hassan Nondo  katika semina iliyofanyika  Hotel ya Zanzibar Beach Resort.
Kiongozi wa Mradi wa Partoma Nanna Maaloe  akikamkabidhi kadi maalumu za kupimia wajawazito Katibu Mkuu Wizara ya Afya  Zanzibar Asha Ali Abdulla katika semina iliyofanyika  Hotel ya Zanzibar Beach Resort.

Baadi ya waalikwa walioshiriki katika Semina ya Mradi unaotolewa na Partoma  iliyofanyika katika Ukumbi wa Hotel ya Zanzibr Beach Resort Resort. Picha Na Abdalla Omar Maelezo- Zaznibar.   

Na Ramadhani Ali – Maelezo. 2.7.2018
Upungufu wa Wafanyakazi na vifaa katika wodi za wazazi pamoja na Idadi kubwa ya akinamama wanaofika kujifungua katika Hospitali Kuu ya Mnazimmoja kunapelekea matatizo kwa mama wajawazito na watoto wachanga wakati wa kujifungua.
Akiwasilisha matokeo ya utafiti uliofanywa kupitia Mradi wa PartoMa Daktari wa Wodi ya Wazazi wa Hospitali hiyo Dkt. Natasha Housseine alisema pamoja na juhudi kubwa zinazochukuliwa na madaktari na wakunga, mapungufu hayo yanasababisha baadhi ya wakati watoto kupoteza maisha muda mfupi baada ya kuzaliwa kwa kukosa uangalizi mzuri.
Dkt. Natasha alisema Hospitali ya Mnazimmoja wastani ya watoto wachanga  12000 huzaliwa kwa mwaka idadi ambayo ni kubwa ukilinganisha na nyenzo na wafanyakazi waliopo ndani ya wodi.
Alieleza kuwa kutokana na tatizo hilo, Mradi wa PartoMa ambao unalenga kufuata taratibu zote za kumuangalia mama mjamzito tokea mwanzo wa kupata uchungu hadi kujifungua umeanzishwa miaka mitatu iliyopita katika Hospitali hiyo.
Alisema Mradi wa PartoMa unaotekelezwa kwa pamoja na Hospitali Kuu ya Mnazimmoja na Chuo Kikuu cha Copenhagen unasaidia kutoa miongozo na mafunzo kwa madaktari na wakunga wachanga ili kuhakikisha usalama wa wazazi wakati wa kujifungua na watoto wachanga baada ya kuzaliwa.
Dkt. Natasha aliongeza kuwa miongozo inayotolewa kwa mama wajawazito kupitia Mradi huo imeanza kuleta mafanikio ikiwa ni pamoja na mama wajawazito kujenga utamaduni wa kupima katika hatua za awali za kujua mwenendo wa afya zao kabla ya kufika hatua ya kujifungua.
Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na watoto wachanga wa Hospitali Kuu ya Mnazimmoja Dkt. Salma Abdi Mahmoud alisema Wizara ya Afya imekuwa ikifanyakazi kwa ushirikiano mkubwa na madaktari wa Zanzibar, kutoka nje ya nchi  na Taasisi za Kimataifa kuhakikisha mama wajawazito na watoto wachanga wanapatiwa huduma bora wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua.
Alisema mahitaji muhimu ya mama wajawazito na watoto wachanga  hivi sasa yamesambazwa katika maeneo yote mijini na vijijini na aliwashauri akinamama  kuzitumia huduma hizo kuimarisha afya zao na watoto wanapozaliwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.