Habari za Punde

Naibu Waziri ashuhudia maendeleo makubwa sekta ya Nyumba Fumba, Zanzibar

 Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa Angeline Mabulla (kushoto) akikaribishwa na Naibu Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira kwa upande wa Zanzibar Mheshimiwa Khamis Juma Maalim katika ofisi za Wizara hiyo, Unguja kisiwani Zanzibar.
 Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa Angeline Mabulla (Kulia) akiongozwa na Naibu Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira kwa upande wa Zanzibar Mheshimiwa Khamis Juma Maalim wakati wa ukaguzi wa Ujenzi wa mji wa kisasa wa nyumba za kimaendeleo katika eneo la Fumba, Unguja kisiwani Zanzibar.
 Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa Angeline Mabulla akiwa ameketi ndani ya moja ya nyumba za kisasa zinanzojengwa katika katika eneo la Fumba, Unguja kisiwani Zanzibar.
 Meneja Masoko wa Mradi wa ujenzi wa Mji wa maendeleo wa Fumba Bibi Fatma Musa (T-Shirt Nyekundu), akimuonesha baadhi ya nyumba zilizo kamilika ujenzi wake Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa Angeline Mabulla.
Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya CPS-Lives LTD Sebastian Dietzold (mwenye suti nyeusi) akimuonesha ukubwa eneo la mradi wa nyumba zinazojengwa na kampuni hiyo Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa Angeline Mabulla.(picha Na. Hassan Mabuye, Wizara ya Ardhi)

Na Hassan Mabuye, Wizara ya Ardhi
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa Angeline Mabulla amefanya ziara katika kisiwa cha Zanzibar na kujionea Ujenzi wa mji wa kisasa wa nyumba za kimaendeleo katika eneo la Fumba wakati wa kukabidhi nyumba 60 kwa wanunuzi wa awali.

Ujenzi wa miji huu wa kisasa wa nyumba za kimaendeleo ni mafanikio makubwa ya ujenzi wa nyumba zilizo bora, zinazozingatia mahitaji muhimu ya familia pamoja na kuzijenga kwa mpangilio maalum.

Mradi wa nyumba za Fumba ni mojawapo wa miradi mikubwa iliyoidhinishwa ambao utakuwa na nyumba 1,400 ambazo zinajengwa katika mfumo wa nyumba za chini na nyumba za ghorofa moja hadi sita ambazo utekelezaji wake utakuwa katika awamu 4, na bei ya kuanzia kwa nyumba itakuwa shilingi milioni 37 tu.

Akiongeza wakati wa ziara hiyo Mhe. Mabulla amewashauri wasimamizi wa mradi huo wa Mji wa Fumba unaotekelezwa na Kampuni ya CPS Live Company Ltd kutenga maeneo ya umma ambayo yatatumiwa na wakazi wa mji huo kwa ajili ya kupumzikia, viwanja vya michezo na maeneo ya maegesho ya magari na fukwe kwa ajili ya kupunga upepo hasa ikizingatiwa Zanzibar ina mazingira mazuri ya fukwe.

Katika ziara hii Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa Angeline Mabulla aliongozwa na Naibu Waziri wa ardhi, Maji, Nishati na Mazingira kwa upande wa Zanzibar Mheshimiwa Khamis Juma Maalim ambaye amemueleza kwamba kwa sasa Zanzibar imechukua juhudi za makusudi katika kuhakikisha suala la makaazi linaimarika kwa kasi na kuweza kukuza uchumi kama ilivyoimarika kwa nchi nyingi duniani na kueleza kuwa miji mengine 14 midogo itajengwa hapa Zanzibar.

Eneo la Fumba lenye Hekta 3000 lilitangazwa rasmi na Mamlaka ya Kukuza Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) kuwa Maeneo Huru ya Kiuchumi mnamo mwaka 1992 sambamba na eneo la hekta 808 lililopo Micheweni Pemba.

Mradi huo unamilikiwa na Raia watatu wa Ujerumani na mmoja wa Ubelgiji ambapo kwa upande wa Raia wa Ujerumani ni Bwana Sebastian Dietsold anayemiliki kwa asilimia 40, Bi Katrin Dietsold asilimia 40 na Bwana Tobias Dietsold asilimia 18 na asilimia 2 zilizobaki ndio zinamilikiwa na Raia wa Ubelgiji Johan Aberebe.

Mradi unatarajiwa kuwekeza jumla ya Dola za Kimarekani Milioni 250 kwa awamu nne ambapo utakuwa na nyumba 1400. Awamu ya kwanza ya mradi huo inakusudia kujenga nyumba 720, nyumba za kawaida 237 na mbele ya bahari nyumba 34 na hivyo kufanya jumla ya nyumba zinazojengwa katika awamu hiyo zinatarajiwa kukamilika katika mwishoni mwa mwaka 2019 kufikia nyumba 991.

Mradi huo unatumia teknolojia ya ujenzi inayotumia rasilimali kidogo ya mchanga bila ya kuathiri ubora wa nyumba hizo na kwa kuzingatia mahitaji maalum ya nchi kama Zanzibar yenye joto na vipindi vya mvua ambapo mradi umewekeza katika kiwanda cha kujenga kuta maalum za nyumba za mbao na tayari kiwanda kinafanya kazi hiyo.


Nae Sebastian Dietsold ambaye ndie mkuu wa mradi huo alieleza hatua zilizofikiwa katika Mradi huo na kuahidi kuwa mradi huo utaendelea kuwa wa aina yake hapa Zanzibar na kueleza jinsi walivyokusudia mradi huo kuwasaidia na wananchi wenye kipato cha chini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.