Habari za Punde

Rais Dk Shein safarini Uingereza
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
  Zanzibar                                                        06.07.2018
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, ameondoka nchini leo kuelekea Uingereza kwa safari maalum ya wiki tatu.

Katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume viongozi mbali mbali wa Serikali, vyama vya siasa  pamoja na wakuu wa vikosi vya ulinzi na usalama wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar walimuaga Rais Dk. Shein.

Dk. Shein katika safari hiyo, amefuatana na Mkewe Mama Mwanamwema Shein pamoja na Watendaji wengine wa Serikali.

Wakati huo huo, Rais Dk. Shein amemtumia salamu za pongezi Rais wa Comoro, Azali Assoumani kwa kutimiza miaka 43 tokea kupata Uhuru kwa Taifa hilo.

Salamu hizo zilieleza kuwa kwa niaba yake Dk. Shein, wananchi pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wanaungana pamoja na ndugu zao wa Comoro katika kusherehekea siku hiyo adhimu ya uhuru wa Taifa hilo.

Aidha, katika salamu hizo, Dk. Shein alimuhakikishia Rais Azali Assoumani kuwa Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano mkubwa uliopo kati yake na nchi hiyo pamoja na wananchi wake sambamba na kuimarisha ustawi wa pande mbili hizo.

Dk. Shein alimtakia kiongozi huyo na familia yake pamoja na wananchi wote wa Comoro kuendeleza amani, upendo na utulivu walionao ili maendeleo yazidi kuimarika. Comoro ilipata uhuru wake Julai 6 mwaka 1975 kutoka kwa koloni la Kifaransa.

 Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.