Habari za Punde

NEC yateua Madiwani 8 wanawake viti maalum



Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeteua madiwani nane (8) wanawake wa viti maalum  kujaza nafasi wazi  za madiwani katika halmashauri nane (8) za Tanzania bara.
Taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa NEC, Jaji wa Mahama ya Rufaa, Semistocles Kaijage Jijini Dar es Salaam leo imesema kwamba uteuzi huo umefanywa kwenye kikao cha Tume cha tarehe 19 Julai, mwaka huu.
“Uteuzi huu umefanyika baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa, ambaye kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, alitaarifu Tume ya Taifa ya Uchaguzi uwepo wa nafasi hizo wazi za Madiwani wanawake wa Viti Maalum, kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), baada ya walioteuliwa awali kufariki dunia au kujiuzulu,” amesema Jaji Kaijage.
Amewataja madiwani hao kuwa ni pamoja na, Ndugu Ajira Rajabu Kalinga(CCM-Halmashauri ya Wilaya ya Songea), Ndugu Mary Kazindogo Mbilinyi (CCM-Halmashauri ya Wilaya ya Makete), Ndugu Zainab Abdi Mabrouk (CCM-Halmashauri ya Manispaa ya Kongwa).
Wengine ni Ndugu Restuta Aloyce Gardian (CCM-Halmashauri ya Wilaya ya Muleba), Ndugu Siglinda Sylvesta Ngwega (CCM-Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro), Ndugu Zena Saadi Luzwilo (CCM-Halmashauri ya Mji Kahama), Ndugu Neema Michael Massawe (CHADEMA-Halmashauri ya Wilaya ya Monduli) na Ndugu Teodola Myula Kalungwana (CHADEMA-Halmashauri ya Manispaa ya Iringa).
Mwisho

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.