RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameupongeza uongozi na wafanyakazi
wote wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa utendaji mzuri
wa kazi zao zinazopelekea kujenga taswira nzuri ya Ofisi hiyo kwa jamii.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo, Ikulu mjini Zanzibar alipokutana na uongozi wa Ofisi ya Rais na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi wakati ulipowasilisha Utekelezaji wa Mpango
Kazi wa Mwaka 2017/2018, na Mpango Kazi wa Utekelezaji kwa mwaka 2018/2019,
Ofisi ambayo imefunga dimba mikutano ya kukutana na Wizara zote za SMZ
iliyoanza Juni 25 mwaka huu.
Rais Dk. Shein alitoa pongezi za dhati kutoka
ndani ya nafsi yake kwa uongozi na wafanyakazi wote wa Ofisi ya Rais na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa mashirikiano yao na utendaji mzuri wa
kazi zao hatua inayompelekea kuendelea kufanya kazi zake vyema za kuwatumikia
wananchi kwa ufanisi.
Alieleza kuwa uwasilishwaji mzuri wa Mpango Kazi
wa Ofisi hiyo umetokana na uzoefu wa muda mrefu uliopatikana tokea kuanza kwa
zoezi hilo la Bango Kitita ambalo lilianza mara tu alipoingia madarakani na
kuendelea hadi hivi leo na kuipongeza Ofisi hiyo kwa kutekeleza vyema Mpango
Kazi wake huo.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumpongeza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa Ussi Haji Gavu kwa kumsaidia katika
shughuli mbali mbali za kazi na kumpongeza Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa
Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee kwa utendaji wake mzuri wa kazi
sambamba na mashirikiano mazuri anayompa.
Aidha, Dk. Shein aliwashukuru na kuwapongeza
Washauri wake wote kwa kuendelea kumshauri mambo mbali mbali ya msingi na kutoa
nasaha kwa uongozi wa Ofisi hiyo huku akiwataka kuwa wasikilizaji wa wananchi
ikiwa ni pamoja na kuwasikiliza wale wote wanaowaongoza pamoja na wananchi
wengine katika jamii.
“Nimeshuhudia uwezo mkubwa mlionao wafanyakazi wa
Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na nimethibitisha hili kwa
kufuata ule msemo usemao ukitaka kuwajua
wafanya kazi wa Ikulu wape kazi”,alisema Rais Dk. Shein.
Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuzipongeza Wizara nyengine zote zilizowasilisha Mpango
kazi wao kwa kufanya vizuri kazi hiyo na kuonesha mafanikio makubwa jambo
ambalo limeendelea kumpa moyo katika kuhakikisha malengo yaliokusudiwa
yanafikiwa.
Dk. Shein aliueleza uongozi wa Ofisi hiyo ya Rais
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kuwa katika kuongoza ni lazima kuwepo na
mashirikiano ili ufanisi uweze kupatikana hivyo ni vyema wakaimarisha
mashirikiano waliyonayo kwa lengo la kupata ufanisi huo.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alisisitiza haja ya viongozi
kusimamia vyema majukumu yao na kuwajibika ili kutela ufanisi zaidi huku akieleza
umuhimu wa kufanya utafiti jambo ambalo ni muhimu katika utendaji wa kazi huku
akisisitiza haja ya kiongozi kuwa mbunifu.
Aidha, Dk. Shein alieleza haja ya kuwepo mpango wa
masomo kwa muda mrefu na muda mfupi kwa
watendaji wa Ofisi hiyo na kusisitiza kuwapangia nafasi za kazi walizozisomea
mara baada ya kuhitimu masomo yao huku akieleza umuhimu wa kuwepo kwa Kamati ya
Mafunzo ndani ya Wizara ili kurahisisha shughuli hizo.
Kwa upande wa Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi
yaani Diaspora, Rais Dk. Shein alieleza kuwa hatua kubwa zimefikiwa katika
kutekeleza dhamira hiyo kwa upande wa Zanzibar.
Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliupongeza uwasilishaji Mpango Kazi na
utekelezaji mzuri uliowasilishwa na Ofisi hiyo huku akieleza lengo kuu la zoezi
hilo ni kupanga kwa ajili ya kuona mbele na kutoa wito kwa kila kiongozi kujua
wajibu na majukumu yake.
Dk. Mzee aliwapongeza watendaji wa Ofisi hiyo kwa
kufanya kazi kwa kasi na ari kubwa na kuwataka kuendelea kuwa mfano mzuri na kuwa
kioo kwa jamii pamoja na kwa watendaji wengine wa Serikali huku akimpongeza Dk.
Shein kwa niaba ya Wafanyakazi wote wa Ofisi hiyo kutokana na kujifunza mambo
mengi kutoka kwake.
Mapema Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa Ussi Haji Gavu akisoma utangulizia wa
Mpango kazi wa Ofisi hiyo alitoa shukurani za dhati kwa Rais Dk. Shein kwa
kuendeleza utaratibu wa kukutana na watendaji wa Mawizara ili kuwasilisha kwake
taarifa za utekelezaji wa Mpango Kazi.
Waziri Gavu alielezea kuwa uwasilishaji huo wa
taarifa ya utekelezaji wa Mpango Kazi umekuwa dira katika kuonyesha na
kuelekeza njia bora zaidi za utekelezaji wa majukumu ya kila siku.
Alieleza kuwa katika programu ya kusimamia huduma
na shughuli za Rais na kuimarisha Mawasiliano Ikulu, shughuli za Rais zimefanyika vizuri na
wananchi wameeleweshwa juu ya shughuli kadhaa za Serikali zikiwemo maendeleo ya
kiuchumi na kijamii.
Aliongeza kuwa kupitia ziara anazofanya Rais
katika Mikoa yote ya Zanzibar, wananchi hupata fursa ya kuelezea changamoto zinazowakabili
ambazo hutolewa ufafanuzi na Mawaziri wanaofuatana naye katika ziara hizo.
Vile vile, alieleza kuwa jarida la Ikulu pamoja na
vipindi mbali mbali vya Redio na Televisheni vilitayarishwa na kurushwa hewani
ambapo pia, mitandao ya kijamii na magazeti yalitumika katika kuwapatia taarifa
wananchi na watu mbali mbali.
Pamoja na hayo, Waziri Gavu alieleza kuwa kupitia
Programu ya Kuratibu Ushirikiano wa Kikanda, Mashirika ya Kimataifa na
Wazanzibari Wanaoishi Nje ya Nchi, ushiriki wa Zanzibar umekuwa ni wenye tija
katika Jumuiya za Mtangamano wa Kikanda za SADC, EAC,IORA na Jumuiya ya Utatu (EAC-SADC-COMESA).
Aidha, alieleza kuwa mahusiano mazuri yameimarika
zaidi baina ya Serikali na Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi yaani Diaspora
ambapo Serikali imeendeleza dhamira yake ya kuwashajiisha Wanadiaspora
kushiriki katika kuiletea Zanzibar maendeleo ya kiuchumi na kijamii kupitia
Kongamano la Nne la Wanadiaspora.
Nao
Washauri wa Rais wa Zanzibar walimpongeza Rais Dk. Shein kwa juhudi kubwa
alizozifanya katika kuipaisha Zanzibar kimaendeleo ikiwa ni pamoja na
kutekeleza vyema Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 kwa vitendo.
Walieleza kuwa Zanzibar imeweza kupiga hatua kubwa
katika kukuza uchumi wake sambamba na kupunguza umasikini.
Walimpongeza kwa kasi nzuri ya kuongoza nchi
pamoja na juhudi zake za kusisitiza na
kuazisha suala zima la utafiti katika taasisi za Serikali huku wakieleza
umuhimu wa watendaji wa Serikali kupelekwa katika vyuo vyenye sifa na vinavyotambulikana.
Mshauri wa Rais Ushirikiano wa Kimataifa na Uchumi
Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa alieleza
kuwepo kwa Kitengo cha kufuatilia maagizo na maelekezo ya Serikali ambacho
tayari kimeshaanza kazi na kutoa wito
kwa uongozi wa Ofisi hiyo kumsaidia Waziri ili aweze kufanikisha malengo
yaliokusudiwa na Kitengo hicho.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment