Habari za Punde

Serikali ya Kuwait yatoa msaada wa Matrekta na vifaa vya afya

Balozi wa Kuwait Nchini Tanzania, Bwana Jasem Ibrahim Al – Najem akitoa salamu wakati akikabidhi msaada wa Matrekta Matatu kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutoka Serikali ya Kuwait.
  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akipokea hati ya makabidhiano ya msaada wa Matrekta Matatu kutoka kwa Serikali ya Kuwait iliyowasilishwa na Balozi wa Nchi hiyo Nchini Tanzania Bwana Jasem Ibrahim Al – Najem
 Balozi Seif  akilipasha moto Moja ya Matrekta yaliyotolewa  msaada na Serikali ya Kuweit huku  akishuhudiwa na Balozi wa Kuwait Nchini Bwana Jasem.
Wa kwanza chini upande wa Kushoto ni Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mheshimiwa Ayoub Mohamed  Mahmoud.
 Balozi Seif akipokea zawadi mbali mbali kutoka kwa Balozi wa Kuwait Nchini Tanzania Bwana Jasem Ibrahim Al – Najem wakati wa hafla ya kumaliza makabidhiano ya vifaa vya Hospitali na zana za kilimo hapo katika Majengo mpya ya Haospitali Kuu ya Mnazi Mmoja.
  Balozi Seif na baadhi ya Watendaji wa Wizara ya  Afya wakiangalia baadhi ya Vifaa vya masuala ya uchangiaji Damu vilivyofungwa katika chumba maalum Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja.
Meneja wa Kitengo cha Huduma za Damu Salama Dr. Mwanakheir akimueleza Balozi Seif baadhi ya vifaa vilivyofungwa ndani ya chamba Maalum kitakachotoa huduma kwa Watu watakaokwenda kuchangia Damu hapo Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein ameipongeza na kuishukuru Serikali ya Kuwait kupitia Taasisi ya Hilal Nyekundu { Rec Cresent} na Balozi wa Nchi hiyo Nchini Tanzania kwa uamuzi wake wa kuendelea kuisaidia Zanzibar katika Sekya za Afya na Kilimo.
Alisema msaada huo uliotolewa na Kuwait wa Vifaa vya Afya vilivyolenga zaidi huduma za uchangiaji damu salama pamoja na Zana za Kilimo { Matrekta} umelenga kuunga mkono jitihada za SMZ  katika kuimarisha sekta ya Afya na Kilimo.
Dr. Ali Mohamed Shein alitoa shukrani hizo zilizotolewa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akipokea Msaada wa Matrekta Matatu hapo kiwanda cha Matrekta Mbweni pamoja na Vifaa vya Afya katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja.
Vifaa vyote hivyo ambavyo ni zawadi Maalum kutoka kwa Serikali na Wananchi wa Kuweit kwa Ndugu zao wa Zanzibar vimegharimu jumla ya Dola za Kimarekani Laki 270,000.
Rais wa Zanzibar alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Wananchi wote wanafurahia pia dhamira nyengine njema ya Serikali ya Kuwait ya kutoa Mkopo wenye masharti nafuu wa Dola za Kimarekani Milioni 13.6 kwa ajili ya kuifanyia matengenezo makubwa Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja.
Dr. Shein  alisema vifaa hivyo muhimu  ambavyo ni nyenzo imara kwa maendeleo ya Afya na maendeleo ya Taifa vitasaidia kupeleka mbele dhamira ya Seriali ya Mapinduzi ya Zanzibar  katika kuimarisha huduma za afya hapa Nchini.
Alieleza katika kufikia lengo la kuimarisha sekta hiyo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua kwa makusidi kuongeza Bajeti ya Wizara ya Afya kufikia Shilingi Bilioni 93.2 katika mwaka wa fedha  wa 2018/2019 kutoka shilingi Bilioni 72.9 mwaka 2017/2018.
“ Bajeti ya kununulia dawa na vifaa vyengine vya utibabu nayo imeongezwa na kufikia shilingi Bilioni 12.7 mwaka 2018/2019 kutoka shilingi Bilioni 7.0 mwaka uliopita wa fedha wa 2017/2018”. Alisema Dr. Shein.
Rais wa Zanzibar alisema ongezeko hilo la Bajeti kwa Wizara ya Afya litazidi kuimarisha ubora wa huduma za Afya zinazotolewa pamoja na kupunguza changamoto zinazowakabili Wananchi wakati wanapofuata huduma za Afya kwenye Hospitali na Vituo vya Afya hapa Nchini.
Alisema wakati Serikali Kuu  imedhamiria kuifanya Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja kuwa ya rufaa, imeazimia kuimarisha upatikanaji wa huduma zote muhimu zikiwemo zile za Benki ya Damu kwa nia ya kuwasaidia wagonjwa wa dharura.
Alieleza kwa mantiki hiyo Hospitali ya Rufaa lazima iwe na huduma bora zenye kuaminika za kukusanya, kuhifadhi na kuwapatia wagonjwa damu safi kwa kadri ya mahitaji  ya huduma hiyo kwa wagonjwa wa maradhi tofauti.
Rais wa Zanzibar alitoa pongezi maalum kwa wananchi, Vikundi vya Jamii pamoja na Taasisi za Zanzibar zilizohamasika kuchangia Damu kwa ajili ya kuweka hakiba kwa matukio ya dharura pale yanapotokea.
Alisema kwa vile uchangiaji damu ni ishara ya imani, Mapenzi na Uzalendo inayolenga kuokoa maisha ya wanaohitaji aliwataka washirika hao kuendelea kuchangia pale inapohitajika kufanya hivyo na Serikali itajitahidi kuona kuwa huduma za kitengo cha Damu zinazidi kuimarika.
Dr. Shein alitoa wito kwa Uongozi wa Wizara ya Afya, Watendaji wa Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja na kitengo cha huduma za Damu cha Hospitali hiyo wanafanya jitihada kubwa ya kuvitunza vifaa hivyo ili vifikie lengo la kuletwa kwake.
“ Wananchi wanapata matumaini makubwa kuona jinsi Serikali yao inavyopiga hatua kama hizi za maendeleo na kuungwa mkono na washirika wetu wa maendeleo”. Alisisitiza Dr. Shein.
Akizungumzia upande wa zana za Kilimo zilizotolewa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein alisema kutokana na msaada huo Serikali itaongeza uwezo wa kutoa huduma za Matrekta hasa kwa wakulima wa Zao la Mpunga.
Alieleza kwamba  hapana shaka maendeleo ya sekta ya kilimo yatasaidia kuongeza mazao yanayolimwa na wakulima wengi hasazao la mpunga na kufikia lengo la kulima mpunga wa kutosha ili kupunguza kiwango cha mchele unaoagizwa nje ya Nchi na kuwa na lishe bora na ya uhakika.
Dr. Shein alifahamisha kwamba dalili za mafanikio ya jitihada za Wakulima Nchini zimeanza kuonekana kutokana naWakulima wengi Mwaka uliopita kupata mavuno mazuri ya Mpunga yaliyofikia Tani 39,683 kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa kwa kipindi cha miaka Mitano iliyopita.
Akitoa pongezi kwa wakulima kwa kufikia kiwango hicho Rais wa Zanzibar alitoa wito kwa Uongozi wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi kuendelea kuwa karibu na wakulima hao Nchini ili kutambua changamoto wanazokabiliana nazo.
Dr. Ali Mohamed Shein alisisitiza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuchukuwa hatua za kuimarisha Sekta ya Kilimo ili ifikie azma yake ya kuleta Mapinduzi ya Kilimo Nchini.
Akitoa salamu za Serikali ya Kuweit Balozi wa Nchi hiyo Nchini Tanzania Bwana Jasem Ibrahim Al – Najem alisema Wananchi wa Kuweit kupitia Taasisi mbali mbali za Nchi hiyo wataendelea kuunga mkono harakati za Maendeleo za Ndugu zao wa Zanzibar katika nia ya kufikia maisha bora zaidi.
Balozi Jasem alisema uungaji mkono huo umekuja kutokana na uhusiano wa muda mrefu wa kihistori uliopo kati ya Kuweit na Wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Alisema Taasisi mbali mbali za Kuweit bado zitaendelea kuangalia maeneo ambayo wanaweza kuendelea kusaidia zaidi katika azma ya kudumisha uhusiano huo unaofungamana na baadhi ya Tamaduni zinazofanana.
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Bibi Maryam Abdulla Saadala akitoa shukrani kwa Serikali ya Kuweit kutokana na msaada huo mkubwa uliolenga Sekta ya Afya na Kilimo alisema muelekeo wa Zanzibar hivi sasa ni kutoka katika uchumi tegemezi.
Bibi Maryam alisema msaada wa vifaa hivyo vya Afya na zana za kilimo utaongeza chachu ya matumaini ya muelekeo huo unaokusudiwa Zanzibar kuwa na uchumi wa Viwanda ifikapo Mwaka 2020  ili iweze kujikimu yenyewe badala ya kutegemea misaada na nguvu za wahisani.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.