Habari za Punde

Tume mpya ya Uchaguzi yatoa ahadi: Hakutokuwa na dosari chaguzi zijazo

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kulia akizungumza na Uongozi Mpya wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar {ZEC} ukiongozwa na Mwenyekiti wake Jaji Mstaafu wa Zanzibar Mh. Hamid Mahmoud Hamid  Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
 Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Jaji Hamid Mahmoud wa Kwanza kutoka Kulia akiwa na Wajumbe wa Tume yake, Kulia yake ni Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo Mh. Mabrouk Jabu Makame.
  Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania Bwana Mohamed Ali Ahmed  wa Pili kutoka Kushoto mwenye Suti rangi ya Maziwa akisisitiza jambo wakati alipofika kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kujitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo.
 Balozi Seif Ali Iddi akielezea dhamira ya Serikali katika kulinda Amani ya Taifa alipokuwa akizungumza na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania Bwana Mohamed Ali Ahmed.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR
Tume ya Uchaguzi Zanzibar umeahidi kwamba hakutakuwa na dosari katika chaguzi zijazo kutokana na Uongozi pamoja na Watendaji wa kujipanga vyema katika kukabiliana na changamoto zozote zinazoweza kujitokeza wakati wa kufanyika kwa  chaguzi hizo.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar {ZEC} Jaji Mstaafu wa Zanzibar  Mh. Hamid Mahmoud Hamid akiiongoza Timu ya Makamishna wa Tume hiyo alisema hayo wakati wakijitambulisha rasmi kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar.
Mwenyekiti na Makamishna hao wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar waliteuliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein hivi karibu na kuwaapisha kushika nyadhifa hizo katika kipindi cha Miaka Mitano ijayo baada ya Tume iliyopita kumaliza muda wake wa Utumishi.
Jaji Hamid Mahmoud Hamid alisema imani iliyoonyeshwa na Viongozi wa Serikali kwa kuwapatia fursa ya uwajibikaji ndani ya Tume hiyo ndio chimbuko  na chachu itakayopelekea kuwapa nguvu za kufanyakazi  zao kwa ueledi, uaminifu na kujiamini.
Alisema kazi mpya itakayoikabili Tume ya Uchaguzi  ya Zanzibar kwa hivi sasa ni maandalizi ya kuendesha Uchaguzi Mdogo wa Jimbo  la Jang’ombe kwa nafasi ya Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Naye kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameupongeza Uongozi Mpya wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar {ZEC} uliopewa jukumu la kuendesha Uchaguzi Visiwani Zanzibar.
Balozi Seif alisema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alikuwa na vigezo vingi vilivyompa ushawishi wa kumteua Mwenyekiti pamoja na Makamishna wa Tume hiyo.
Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwatanabahisha Viongozi wa Taasisi hiyo inayosimamia Uchaguzi Zanzibar kwamba kazi zao zina changamoto ambazo wanapaswa kutumia hekima na busara katika kuzitafuatia ufumbuzi kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Miongozo iliyowekwa ya kusimamia Taasisi hiyo.
Ujumbe huo wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar  ulioongozwa na Mwenyekiti wake  Jaji Mstaafu wa Zanzibar Hamid Mahmoud Hamid umeambatana na Makamu Mwenyekiti wake Mh. Mabrouk Jabu Makame, Kepteni  Feteh Saad Mgeni na Bibi Jokha Khamis Makame.
Wajumbe wengine wa Tume hiyo ni Bwana Makame Juma Pandu, Dr. Kombo Khamis Hassan pamoja na Jaji Khamis Ramadhan Abdulla.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Balozi Seif Ali Iddi alikutana kwa mazungumzo na Naibu Msajili  Mpya wa Vyama vya Siasa Nchini Tanzania Nd. Mohamed Ali Ahmed  aliyefika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kujitambulisha Rasmi baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo.
Katika mazungumzo yao Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania  Nd. Mohamed Ali Ahmed alisema kauli za baadhi ya Viongozi wa Kisiasa bado zinaenda kinyume na dhamira ya uwepo wa Vyama vya siasa iliyomo ndani ya Sheria nambari 2 ya Mwaka 1992.
Alisema licha ya kwamba Vyama vya Siasa vinajengwa na matendo ya Viongozi wa Vyama vya siasa lakini Msajili wa Vyama hivyo hatavumilia kauli za Viongozi wenye muelekeo wa kuleta uchochezi na hatimae kuwavuruga Wananchi.
Nd. Mohamed alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Vyama vyote vya Kisiasa Nchini lazima vizingatie Sheria, Kanuni na taratibu zilizowekwa za kuendesha Vyama vyenyewe  ili ile dhama ya uwepo wa Demokrasia iwafikie Wananchi wote.
Naibu Msajili huyo wa Vyama vya Siasa Tanzania ameelezea faraja yake kutokana na Uongozi wa Chama cha Siasa cha Mapinduzi kuwafuatilia Wanachama wake iliyowapa Uongozi hasa katika Mabaraza ya kutunga Sheria jambo ambalo linapaswa kupongezwa.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema suala la Amani ya Taifa lazima ilindwe kwa nguvu zote jambo ambalo Serikali kamwe haitakuwa tayari kuona lulu hiyo inachezewa.
“Tutamchulia hatua Mtu ye yote hata awe nani bila ya kujali wadhifa wake, Imani ya Dini pamoja na Itikadi ya Kisiasa ”. Alionya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Balozi Seif alifafanua kwamba Serikai Kuu kamwe haichukii kukosolewa kwa vile wasimamizi wake ni Binaadamu, bali kisichoridhiwa na Serikali hiyo ni baadhi ya Kauli zinazotolewa na Watu wakiwemo Viongozi, wanaharakati na hata Waumini wa Dini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.