Habari za Punde

Waziri Kiongozi Mstaafu wa Zanzibar Mhe. Shamsi Awataka Masheha Kuwahamasisha Wananchi Kujiunga na Kuanzisha Saccos Kwa Maendeleo Yao.

Na Takdir Ali. Maelezo Zanzibar.
Waziri Kiongozi Mstafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mh.Shamsi Vuai Nahodha amewaagiza Masheha kuwashajiisha wafuasi wao kujiunga na Vikundi vya Ushirika ili waweze kujipatia kipato cha kuwaendesha Maisha yao.
Amesema katika Vikundi kuna fursa nyingi za kimaendeleo lakini bado baadhi ya Masheha hawajachukuwa juhudi za kuwashajiisha Wanajamii kujiunga na kuibua fursa hizo.
Mh.Shamsi ameyasema hayo huko Mbarali meli 4, katika Ofisi ya Meli Saccos alipokuwa akizungumza na Viongozi wa Sacos hiyo mara baada ya kukabidhi sh. Milioni 8 ikiwa ni ahadi aliitoa katika Mkutano mkuu wa Sacos hiyo uliofanyika 1/07/2018.
Amesema Masheha ni sehemu ya Serikali hivyo wanapaswa kusimamia mipango iliowekwa na Serikali ya kuwakwamua Wananchi wake kutokana na tatizo la Umasikini iwemo Mkuza 3.
Mbali na hayo Mh. Shamsi amewawaomba Wanasiasa wenzake kuwekeza zaidi Wananchi wao katika Vikundi vya Ushirika ili waweze kujipatia kipato na kuepukana na hali tegemezi.
“Wanasiasa wenzangu kutoka vyama vyote naomba tuwaingize Wanachama wetu katika Sacos kwani kuna Wananchi wengi hasa ukizingatia kuwa mtaji wa Mabenki ni Fedha lakini mtaji wetu sisi Wanasiasa ni Wananchi hivyo tuwasaidieni Wananchi wetu jamani.”Aliomba Mh.Shamsi.
Hata hivyo  amewaasa Wanasiasa wenye tabia ya kuanzisha utitiri wa Sacos kila inapofika kipindi cha kampeni za Uchaguzi lakini mara baada ya kumalizika Uchaguzi wanaviacha vikisambaratika jambo ambalo linawavunja moyo Wananchi na kupelekea kutofikia malengo waliojipangia ya kujikwamua na tatizo la Umasikini.
Kwa upande wake Mwakilishi wa kuteuliwa na Rais Mh. Ahmada Yahya Abdul-wakil “Shaa” amesema lengo la Serikali kuanzisha vikundi vya Ushirika ni kuwakwamua Wananchi wake kutokana na janga la Umasikini kwani  haina uwezo wa kuajiri mtu watu wote.
“Serikali haina uwezo wa kuajiri mtu mmoja mmoja hivyo Wananchi kuanzisha mambo kama hayo yanatupa moyo na faraja, endeleeni kuhamasishana muwe wengi zaidi,”Alisema Mh.Shaa ambae pia ni Mwanachama wa Meli 4 Sacos.
Nae Katibu wa Meli 4 Saccos Bi.Njuma Ali Juma amempongeza Mh.Shamsi kwa  juhudi kubwa anazozichukuwa za kuhakikisha Ushirika huo wa kukopa na kuweka unaendelea sambamba na kuwaomba kuwaomba Viongozi wengine kuiga mfano wake.
Amesema lengo kuu  la kuanzisha Ushirika huo ni kufikia kuanzisha benki yao wenyewe itakayowasaidia kuwanyanyua kiuchumi na kuepukana na hali ya Umasikini iliodumu kwa muda mrefu miongoni mwao.
Ushirika wa Meli 4 Sacos uliopo Mtaa wa Mbarali meli 4 umeanzishwa mwaka 2005 ukiwa na Wanachama 150 ambapo hadi sasa Una Wanachama 1,500  na kauli mbiu ya Ushirika huo kopa kwa Busara lipa kwa wakati.
Imetolewa na Idara ya Habar Maelezo Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.