Habari za Punde

WAZIRI WA BIASHARA NA USHIRIKA-UGANDA AVUTIWA NA UENDESHAJI USHIRIKA NCHINI TANZANIA AOMBA RIDHAA KUJA KUJIFUNZA NCHINI TANZANIA

Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba akisalimiana na Waziri wa biashara na ushirika nchini Uganda Mhe Fredric Ngobi Gume muda mchache kabla ya kuanza kwa mkutano wa mawaziri wa nchi hizo mbili, mkutano uliohudhuriwa pia Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe Charles Mwijage, Jana 11 Julai 2018. (Picha zote Na Mathias Canal, WK)
Kikao kikiendelea eneo la Mtukula Wilayani Misenyi. Jana 11 Julai 2018
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe Charles Mwijage akisalimiana na Waziri wa biashara na ushirika nchini Uganda Mhe Fredric Ngobi Gume muda mchache kabla ya kuanza kwa mkutano wa mawaziri wa nchi hizo mbili, mkutano uliohudhuriwa pia na Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba, Jana 11 julai 2018.

Mathias Canal-WK, Mtukula-Kagera
Serikali ya Uganda imeeleza kuvutiwa na uendeshaji wa ushirika nchini Tanzania hivyo imeomba kupata ridhaa ya kuzuru nchini Tanzania ili kujifunza namna bora ya uendeshaji wa ushirika.

Ombi hilo limetolewa jana 11 Julai 2018 na Waziri wa Biashara na Ushirika nchini Uganda Mhe Fredrick Ngobi Gume wakati akizungumza kwenye mkutano uliohudhuriwa pia na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe Charles Mwijage uliofanyika katika eneo la Mtukula Wilayani Misenyi.

Katika mkutano huo Waziri huyo  anayeshughulikia Ushirika nchini Uganda alimpongeza Waziri wa Kilimo nchini Mhe Dkt Charles Tizeba kwa Nazi kubwa aliyoifanya katika kipindi cha muda mfupi kurejesha imani kubwa na ushirika kwa wakulima ambapo alimpongeza pia kwa tuzo ya heshima aliyokabidhiwa na Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe Kassim M. Majaliwa kwa niaba ya wana ushirika wakati wa sherehe za kilele cha siku ya ushirika Duniani kwenye viwanja vya Furahisha Jijini Mwanza.

Waziri wa biashara na ushirika nchini Uganda Mhe Gume alimuhakikishia mwenyeji wake kuwa biashara ya Kahawa nchini humo ina changamoto sawa katika nchi zote mbili kwa kuwa swala la mikopo isiyo rasmi inayowanyonya wakulima (Butura) nchini Uganda ipo kwa kiwango cha juu.

Alisema kuwa serikali ya Uganda inayoongozwa na Rais wa nchi hiyo Mhe Yoweri Kaguta Museveni itaendeleza ushirikiano na serikali ya Tanzania inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli hivyo panapohitajika ushirikishwaji katika biashara hususani kwenye sekta ya Kilimo watakuwa na msimamo wa pamoja.

Alisema miongoni kwa mambo mengine ya kujifunza nchini Tanzania itakuwa ni pamoja na kujifunza kuhusu namna bora  ya kuendesha ushirika na kuanzisha mfumo wa stakabadhi ghalani.

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba alimueleza Waziri Gume kuwa njia mojawapo ya kusimamia ushirika ni pamoja na mkakati wa usimamizi madhubuti ikiwa ni pamoja na kuwaweka kizuizini wabadhilifu wote katika ushirika.

Mkutano huo ni muendelezo wa utekelezaji wa maagizo ya Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli aliyoyatoa wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali Ikulu Jijini Dar es salaam tarehe 2 Julai 2018 na kuitaka Wizara ya Kilimo kufuatilia kwanini wakulima wa zao la Kahawa wanacheleweshewa malipo yao sambamba na kujua kwanini wakulima wanauza Kahawa yao nchini Uganda.

Naye Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe Charles Mwijage aliongeza kuwa wakulima wa Tanzania na Uganda wanapaswa kuweka msisitizo katika Kilimo kwani kufanya hivyo kutaongeza uimara na uanzishwaji wa viwanda vitakavyoongeza chachu ya ajira kwa wananchi.

MWISHO

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.