Habari za Punde

BENKI YA STANDARD CHARTED KUIMWAGIA TANZANIA SH. TRILIONI 3.3 KUJENGA RELI YA KISASA-SGR

 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa pili kulia) na Mkurugenzi  Mtendaji wa Benki ya Standard Chartered  Group,   Bw. Bill Winters, wakipeana mikono nje ya jengo la Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam baada ya kumalizika kwa mkutano kati yao ulioangazia ushirikiano wa maendeleo ambapo Benki hiyo itatoa shilingi trilioni 3.3 kujenga Reli ya Kisasa. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Afrika Mashariki Bw. Lamin Manjang na kushoto ni Mkurugenzi wa Benki hiyo nchini Tanzania Bw. Sanjay Rughani.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia) akiagana na mgeni wake Mkurugenzi  Mtendaji wa Benki ya Standard Chartered  Group Duniani kutoka Uingereza   Bw. Bill Winters, baada ya kumalizika mkutano kati yao ambapo Benki hiyo kuipatia Tanzania mkopo nafuu wa Dola Bilioni 1.46  (Trilioni 3.3) ili kutekeleza mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa kutoka Morogoro hadi Dodoma.
Mkurugenzi  Mtendaji wa Benki ya Standard Chartered Group Duniani kutoka  Uingereza   Bw. Bill Winters, akipongeza hatua za ukuaji wa Uchumi wa Ndani wa Tanzania (GDP) kwa kiwango cha asilimia  7 kwa kuwa inaonesha jitihada za kufikia uchumi wa kati, wakati wa mkutano kati yake na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), hayupo pichani. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Afrika Mashariki Bw. Lamin Manjang na kulia ni Mkurugenzi wa Benki hiyo nchini Tanzania Bw. Sanjay Rughani.
Mkutano kati ya Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Standard Chartered Group Duniani kutoka Uingereza   Bw. Bill Winters, na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) ukiendelea katika ukumbi sa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb),  akitoa shukrani za Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa Mkurugenzi  Mtendaji wa Benki ya Standard Chartered Group  Duniani kutoka  Uingereza   Bw. Bill Winters (hayupo pichani), kwa kuisaidia Tanzania kupata Dola Bilioni 1.46 kwa ajili ya Ujenzi wa Reli ya Kisasa kutoka Morogoro hadi Makotopora Jijini Dodoma.
 (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango)

Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
BENKI ya Standard Chartered Group imekubali kuipatia 
Tanzania mkopo nafuu wa dola za Marekani bilioni 1.46 
sawa na zaidi ya shilingi trilioni 3.3 kwa ajili ya kujenga 
kipande cha Reli ya Kiwango cha Kimataifa (SGR) kuanzia 
Morogoro hadi Makutupora, mkoani Dodoma.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. 
Philip Mpango, baada ya kukutana na kufanya mazungumzo 
na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Bw. Bill Winters, 
Jijini Dar es Salaam.

Dkt. Mpango ameishukuru Benki hiyo kwa kukubali 
kugharamia ujenzi wa Reli hiyo ya kisasa ambayo lengo lake 
ni kuimarisha usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo 
kwenda bara na nchi jirani za Maziwa Makuu na zile ambazo 
hazipakani na Bahari.

"Tunajenga Reli hiyo ya Kisasa kutoka Dar es Salaam - 
Morogoro hadi Makutupora ambazo ni awamu mbili lakini 
pia tutajenga reli hiyo kuelekea Isaka mpaka Mwanza na 
baadaye Rusumo ambapo wenzetu wa nchi ya Rwanda, 
tutasaidiana, wao watajenga reli hiyo kutoka Rusumo hadi 
Kigali" Aliongeza Dkt. Mpango
Aidha, Dkt. Mpango amemweleza Kiongozi huyo wa Juu 
kabisa wa Benki ya Standard Chartered Group anayeongoza 
Benki hiyo kwenye nchi zaidi ya 60 duniani, kuhusu 
vipaumbele vikubwa vya nchi ikiwemo kuboresha Shirika la 
Ndege la Taifa-ATCL, na Ujenzi wa Mradi Mkubwa wa Kufua 
Umeme wa Mto Rufiji.

"Tunaimarisha Shirika letu la Ndege ili kuimarisha sekta ya 
utalii kwa sababu tuna vivutio vingi na haipendezi wageni 
wanao kuja nchini wanafikia nchi jirani, sasa ifike wakati 
tuwe na uwezo wa kuwasafirisha moja kwa moja kuja nchini 
kwetu" Alisisitiza Dkt. Mpango.

Alisema Tanzania ni ya pili duniani kwa kuwa na vivutio 
vingi vya utalii ikitanguliwa na Brazil lakini inapokea watalii 
wasiozidi milioni 2 kwa mwaka jambo ambalo linahitaji 
kufanyiwa kazi kwa haraka ili sekta hiyo ichangie uchumi wa 
nchi kwa kiasi kikubwa kupitia fedha za kigeni.

Alisema katika kulifufua Shirika hilo la Ndege, tayari Serikali 
imenunua ndege nne ikiwemo ndege kubwa aina ya Boeing 
787- 8 Dreamliner na kwamba ndege nyingine 3 zitakuwa 
zimewasili nchini ifikapo mwezi Juni, mwakani, na kulifanya 
shirika hilo kuwa na ndege 7.  

Alivitaja vipaumbele vingine kuwa ni kuboresha huduma za 
jamii kama vile elimu, afya, maji na kuendeleza ujuzi kwa 
wananchi ili waweze kufanyakazi kwenye viwanda na 
kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa ujumla kwa kuwa 
maendeleo yanahusu watu.

Akizungumza kwenye mkutano wake na Dkt. Mpango, 
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Standard Chartered 
Group, Bw. Bill Winters, ameipongeza Tanzania kwa kupiga 
hatua kubwa kiuchumi na kwamba Benki yake itatoa mkopo 
huo na kuahidi kuwa balozi wa kuelezea mafanikio makubwa 
ya kiuchumi ya Tanzania kwa wadau wengine.

Aliahidi kuzishawishi taasisi nyingine za fedha ulimwenguni 
kuangalia uwezekano wa kuunga mkono jitihada hizo 
ambazo mwisho wake wanufaika wakubwa watakuwa ni 
wananchi wote wa Tanzania kwa ujumla.

"Tunaimani kubwa na uwezo wa Tanzania pamoja na fursa 
nyingi za kiuchumi ilizonazo na kwamba miradi mingi ya 
kipaumbele iliyoainishwa itafikiwa na tunalo jukumu kama 
Benki kutoa fedha na kuiweka miradi hiyo pia sokoni ili 
iweze kupata fedha" Alisisitiza Bw. Bill Winters.

Katika kikao hicho, Bw. Bill Winters aliambatana na 
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo nchini Kenya na nchi za 
Ukanda wa Afrika Mashariki Bw. Lamin Manjang na 
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo nchini Tanzania Bw. 
Sanjay Rughani, ambapo pia Benki hiyo inafanya shughuli 
zake hapa nchini kwa kipindi cha miaka 101 sasa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.