Habari za Punde

Kampuni ya Samkay Consult Cooperation Limited Kusimamia Ujenzi wa Nyumba za 30 za Maafa Katika Kijiji cha Nungwi Mkoa wa Kuskazini Unguja.

Mkurugenzi Mkuu wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Nd. Makame Haji aliyesismama akitoa Taarifa fupi ya matayarisho ya Mwisho ya Ujenzi wa Nyumba za Makaazi ya Wananchio walioathirika na Mvua za Masika msimu uliopita wakati wa hafla ya kumkaribisha Mshauri Muelekezi wa Ujenzi huo.Kulia ya Nd. Makame ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Shgaaban Seif Mohamed, Mkuu wa Mkoa Kaskazini Unaguja Mh. Vuai Mwinyi Mohamed, Naibu Mkurugenzi wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Nd. Muhidin  Ali Muhidi.
Kushoto ya Ngugu Makame ni Mshauri wa Kampuni ya Samkay  Consult Cooperation  Limited Bwana Amour Hamad Omar.
 Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Shaaban Seif Mohamed akimkaribisha Mshauri wa Kampuni ya Samkay  Consult Cooperation  Limited Bwana Amour Hamad Omar kwa Mkuu wa Mkoa Kaskazini Unguja Mh. Vuai Mwinyi Mohamed.
Mshauri wa Kampuni ya Samkay  Consult Cooperation  Limited Bwana Amour Hamad Omar wa kwanza kulia akiahidi kusimamia vyema ujenzi wa Nyumba za Makaazi ya Wananchi walioathirika na majanga ya mvua za Masika za Msimu uliopita Nungwi na Msuka.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis.OMPR. 
Katibu  Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Shaaban Seif  Mohamed alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hairidhii kuona baadhi ya Wananchi wanakuwa wabishi kuendelea kujenga na hatimae kuishi katika maeneo hatarishi kwa maisha ya Mwanaadam.
Alisema yapo maeneo ambayo Serikali tayari imeshayatolea maamuzi ya kuwataka Wakaazi wa sehemu hizo wahame ili kujiepusha na majanga yanayosababishwa na mafuriko hasa wakati wa msimu wa mvua kubwa za masika.
Nd. Shaaban Seif  Mohamed alisema hayo katika kikao kifupi cha kutambulishwa rasmi kwa Mshauri Muelekezi wa usimamizi wa Ujenzi wa Nyumba  za Wananchi waliokumbwa na Maafa Msimu uliopita kwa Uongozi wa Mkoa Kaskazini zinazotarajiwa kujengwa katika Kijiji cha Nungwi Mkoani humo.
Mshauri huyo Muelekezi wa Kampuni ya Samkay Consult Cooperation  Limited Bwana Amour Hamad Omar ndiye  atakayesimamia Ujenzi wa Nyumba 30 katika Kijiji cha Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja na nyengine Nyumba 30 katika Kijiji cha Tumbe Mkoa Kaskazini Pemba.
Nd. Shaaban alimuomba Mshauri Muelekezi huyo wa usimamizi wa Nyumba hizo kuhakikisha kwamba Ujenzi wa Majengo hayo yanakuwa katika kiwango kinachokubalika Kitaalamu.
 Alisema wapo Washauri  Waelekezi wenye tabia ya kuachilia udhaifu wa Kitaalamu unaofanywa na Baadhi ya Wakandarasi na kusubiri kutoa makosa hatua za mwisho za ujenzi jambo linaloweza kuepukwa mapema ili kuondosha au kupunguza kabisa hasara inayoweza kujitokeza.
Akimpokea Mshauri Muelekezi huyo wa Kampuni ya Samkay Consult Cooperation  Limited Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unaguja Mh. Vuai Mwinyi  Mohamed alisema Ofisi yake iko huru wakati wowote kumpa ushirikiano wa kiutendaji Mtaalamu huyo.
Mh. Vuai alisema hatua hiyo ya ukaribu kati ya Viongozi wa Taasisi zilizopewa jukumu hilo ndio utakaopelekea kukamilika na hatimae kufanikisha kazi hiyo iliyolenga kuwapa faraja wananchi waliopatwa na Maafa ya Mvua za Masika za Msimu uliopita.
Akitoa shukrani zake Mshauri Muelekezi huyo wa Kampuni ya Samkay Consult Bwana Amour  Hamad Omar  aliuahidi Uongozi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na ule wa Mkoa wa Kaskazini Unguja kwamba Taasisi yake itasiamia kwa uadilifu na Uzalendo Mradi huo muhimu kwa maisha ya Jamii.
Bwana Amour alisema yapo mapendekezo iliyotoa Kampuni yake ya kuitaka Serikali kupitia Wizara inayosimamia Ardhi kuliongezea eneo linalotaka kujengwa Nyumba hizo kwa upande wa Nungwi katika Kisiwa cha Unguja  ili lilingane na na lile la Tumbe Kisiwani Pemba.
Alisema hatua hiyo inaweza kutoa ushawishi mkubwa zaidi kwa wafadhili wa Mradi huo kuongeza msaada zaidi kwa vile waathirika wa majanga ya Mvua bado idadi yao ni kubwa ikilinganishwa na wale waliobahatika kupata uteuzi wa mwanzo.
Akitoa Taarifa ya Mradi huo wa Nyumba Mkurugenzi Mkuu wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Nd. Makame Haji Makame alisema ujenzi wa Nyumba hizo Unguja na Pemba unatarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia sasa.
 Nd. Makame alisema ujeni huo utaanza kwa awamu ya kwanza itakayohusisha Nyumba za Makaazi zipatazo 30 kwa kila upande wa Unguja chini ya Ufadhili wa Jumuiya ya Hilali Nyekundu { Red Cresent} ya Falme za Kiarabu {UAE}.
Alisema awamu ya pili itahusisha ujenzi wa Vituo vya Afya, Skuli, Sokona Maduka ikimaanisha kwamba  maeneo hayo ambayo yanatarajiwa kuwa Miji Midogo yatakuwa na huduma zote za msingi zinazopaswa kumfikia  Mwanaadamu.
Mkurugenzi Mkuu huyo wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar alifahamisha kwamba  harakati za maandalizi ya uwezo wa huduma za msingi kama Maji, Umeme na Bara bara zinaendelea kuratibiwa kwa kuhusisha Taasisi zote zinazohusika na masuala hayo.
Ujenzi wa nyumba hizo umekuja kufuatia Jumuiya ya Hilali Nyekundu { Red Cresent} ya Flme za Kiarabu {UAE} kuguswa na maafa yaliyowakumba Wananchi mbali mbali wa Visiwa vya Unguja na Pemba wakati wa Msimu wa Mvua za Masika zilizopita zilizosababisha Wananchi hao kukosa makaazi baada ya Nyumba zao kubomoka kabisa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.