Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi Atembelea Ofisi zaTume ya Kitaifa ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kushoto akifanya ziara ya kuikagua Ofisi Kuu ya Tume ta Kitaifa ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya Zanzibar iliyopo Mtaa wa Meya Mjini Zanzibar.Wa Kwanza kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya Zanzibar Bibi Kheriyangu Mgeni Khamis.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya Zanzibar Bibi Kheriyangu Mgeni Khamis akimtembeza Balozi Seif  baadhi ya maeneo ya Ofisi ya Tume yake iliyopo Meya Mjini Zanzibar.Nyuma ya Balozi Seif  ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Mohamed Aboud Mohamed.
Balozi Seif akisalimiana na Mkuu wa Kitengo cha Kinga na Tiba cha Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya Bwana Mahmoud Mussa alipotembelea Vitengo mbali mbali ndani ya Ofisi hiyo.
Balozi Seif Kushoto akizungumza na Wajumbe wa Sekriterieti ya Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya Ofisini kwa Mkurugenzi wa Tume hiyo Meya Mjini Zanzibar baada ya kutembelea maeneo mbali mbali ya Ofisi hiyo.Picha na – OMPR – ZNZ.

Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema dawa za kulevya Nchini zinaweza kuondoka kabisa au kupunguwa kwa kiwango kikubwa endapo Taasisi zinazosimamia udhibiti wa uingiaji na usambazaji wa bidhaa hizo haramu zitajizatiti kushirikiana kwa karibu zaidi katika mapambano hayo.
Alisema Zanzibar haina mahali pengine panapotumiwa kwa uingizaji na utoaji wa Dawa za Kulevya isipokuwa Bandarini na Viwanja vya Ndege maeneo ambayo kama mikakati ya kizalendo itatumiwa na wasimamizi wake uwepo wa Dawa za kulevya itakuwa historia katika Taifa hili.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akizungumza na Kamati ya Sekriterieti ya Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya Zanzibar  baada ya kufanya ziara fupi ya kukagua mazingira ya kazi ya Wafanyakazi wa Tume hiyo kwenye Ofisi yao Kuu iliyopo Mtaa wa Meya Mjini Zanzibar.
Alisema licha ya juhudi kubwa zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali Kuu kwa kushirikiana na Taasisi ya Kitaifa na Kimataifa za kuendesha mapambano dhidi ya Uingizwaji na usambazaji wa Dawa la kulevya lakini bado wapo  baadhi wa Watendaji wanashindwa kuwa waadilifu katika mapambano hayo.
Balozi Seif alieleza kwamba upo ushahidi unaoonyesha kwamba baadhi ya Watendaji wa Taasisi za Umma kama Polisi  na Mahkama sio waaminifu na kulekea kutoa mwanya kwa Wafanyabiashara wa Dawa za Kulevya ili kukwepa Kesi zinazowakabili na hatimae kuendelea kufanya biashara hiyo haramu.
Alitanabahisha kwamba kila sekta ikiamua kutimiza wajibu wake iliyopangiwa na Taifa , wimbi la Dawa za kulevya Nchini linaloikumba Jamii hasa kundi kubwa la Vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa linaweza kuondoka.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji pamoja na kuwashukuru Watendaji wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya Zanzibar kwa kutekeleza majukumu yao ya kazi ya kilaSiku katika mazingira magumu.
Balozi Seif  alisema Serikali Kuu kupitia Uongozi wa Ofisi yake inayoratibu utendaji wa shughuli za Tume hiyo itajitahidi kuwajengea mazingira bora ya Kazi kwa kuwapatia Ofisi itakayolingana na majukumu wanayotekeleza.
“Kazi hii nitamuachia Waziri, Katibu  Mkuu na Watendaji wao kukaa pamoja na Uongozi wenu kufikiria eneo litakalofaa ili tukujengeeni Ofisi inayolingana na kazi zenu nzito za kila siku zinazohitaji utulivu ”. Alisema Balozi Seif.
Alisema ziara yake fupi imempa picha halisi ya kushuhudia Mazingira ya Watendaji wa Tume hiyowanaosimamia jukumu zito la Kitaifa  sio rafiki na hayakubaliani na Kanuni za Utumishi wa Umma zinazoelekeza kufuatwa kwa Usalama wa Afya Kazini.
Mapema  Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya Zanzibar Bibi Kheriyangu Mgeni Khamis alisema Tume hiyo ilianzishwa kwa Mujibu wa Sheria ya Zanzibar  Nambari 9 ya Mwaka 2009 Chini ya iliyokuwa Ofisi ya Waziri Kiongozi.
Alisema mabadiliko ya Kiutendaji Serikalini yalipelekea Tume hiyo baadae kuwa chini ya iliyokuwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Zanzibar  mnamo Mwaka 2000 na baadae Mwaka 2010 ikawa chini ya usimamizi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Bibi Kheriyangu alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba utendaji wa Tume hiyo ulipata ufanisi mkubwa zaidi baada ya kuanzishwa  kwa Idara Tatu zilizofuatiwa na Vitengo Sita ndani ya Tume hiyo.
Alisema hatua hiyo imepelekea kubuniwa kwa Jumuiya za upataji nafuu kwa watumiaji wa Dawa za Kulevya Mitaani hasa kwa Vijana walioamua kuachana na matumizi ya Dawa hizo zilizokwenda sambamba na kuundwa kwa Kanuni za Uangamizaji wa Dawa za Kulevya.
Hata hivyo Mkurugenzi Mtendaji huyo wa   Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya Zanzibar Bibi Kheriyangu Mgeni Khamis alisema zipo changamoto kubwa zinazowakabili Watendaji wa Tume hiyo na kupelekea kuwa katika mazingira magumu ya uwajibikaji wao.
Bibi Kheriyangu alizitaja baadhi ya changamoto hiyo kuwa ni pamoja na wimbi la uingizwaji na usafiriaji wa Dawa za Kulevya Nchini linalotokana na uwepo wa baadhi ya wasimamizi wasiokuwa waaminifu na kupelekea waendesha Biashara hiyo kupata mwanya wa kuendelea na mchezo huo mchafu.
Alisema changamoto nyengine ni uchakavu na ufinyu wa Ofisi ya Tume unaopelekea kuwa na watendaji kidogo licha ya Wizara inayosimamia Utumishi wa Umma   kutoa baraka ya nyongeza ya Wafanyakazi wa Tume hiyo.
Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya Zanzibar inasimamiwa na  Watendaji 35 wenye  uzoefu mkubwa na sifa tofauti za Kielimu katika masuala ya Afya, Utawala, ushauri nasaha pamoja na Ukaguzi wa Dawa za Kulevya.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.