Habari za Punde

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji Aendelea na Ziara Yake Kutembelea Miradi Mbalimbali. Aagiza Uchunguzi Ufanyika Mradi wa Ujenzi wa Vyumba Vya Madarasa Shule ya Msingi Kigoma.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango. Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), (Kulia), akisisitiza jambo wakati akikagua ujenzi wa vyumba vya madarasa vinavyojengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Japan kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 200 katika Shule ya Msingi Kigoma, iliyoko Kigoma Ujiji, mkoani Kigoma.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango. Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), (Mbele), akiwa na maafisa waandamizi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, pamoja na wataalam wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, alipofanya ziara kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa 9 yanayo jengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Japan kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 200 katika Shule ya Msingi Kigoma, iliyoko Kigoma Ujiji, mkoani Kigoma.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kigoma Bw. Sabasi Lugai (kushoto) akisoma taarifa ya mradi wa Ujenzi wa Vyumba tisa vya madarasa na matundu 12 ya vyoo utakaogharimu takribani Sh. milioni 218 wakati Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (kulia) alipotembelea na kukagua miradi katika Mkoa wa Kigoma, wa pili kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Uvinza na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Bi. Mwanamvua Mlindoko.
Sehemu ya msingi wa vyumba vya madarasa mapya yanayojengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Japan, katika Shule ya Msingi Kigoma, Manispaa ya Kigoma Ujiji, Mkoani Kigoma, kwa gharama ya zaidi ya shilingi 200m

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango. Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), (Katikati), akikagua ujenzi wa vyumba vya madarasa vinavyojengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Japan kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 200 katika Shule ya Msingi Kigoma, iliyoko Kigoma Ujiji, mkoani Kigoma. 
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji Dkt. John Shauri Tlatlaa, akitoa ufafanuzi wa idadi ya vyumba vya madarasa katika Shule ya Msingi Kigoma  kwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (wa pili kulia), ambao unatofautiana na maelezo ya Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo  Bw. Sabasi Lugai, aliyetoa taarifa kwamba yako tisa, jambo lililosababisha Naibu Waziri huyo kuagiza kufanyika kwa uchunguzi wa mradi huo.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango)

Na.Benny Mwaipaja, WFM, Kigoma
NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, 
ameiagiza Kamati ya Ulinzi na Usalama wilaya ya Kigoma 
kufanya uchunguzi na kuchukua hatua baada ya kubaini 
harufu ya ufisadi katika ujenzi wa vyumba vya madarasa 9 ya 
shule ya msingi Kigoma yanayojengwa kwa ufadhili wa 
Serikali ya Japan kwa gharama ya shilingi milioni 200.

Dkt. Kijaji ametoa maelekezo hayo baada ya Kaimu 
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Dkt. John Tlatlaa, 
kueleza kwamba  mradi huo unahusisha ujenzi wa vyumba 10 
vya madarasa na vyoo vyenye matundu 12, wakati mkataba 
ulioingiwa kati ya Manispaa na Mkandarasi inayoonesha 
kwamba yatajengwa madarasa tisa na vyoo vyenye matundu 
12.

Baada ya mjadala kati yake na Kaimu Mkurugenzi huyo wa 
Manispaa ya Kigoma, akamwelekeza Kaimu Mkuu wa Wilaya 
hiyo Bi. Mwanamvua Mlindoko kuchukua hatua za 
kiuchunguzi.

"Mradi unaojulikana Mhe. Mkuu wa Wilaya ni wa madarasa 
tisa, mkandarasi akija kudai nyongeza ya malipo kwa darasa 
moja lililoongezeka atakuwa na haki!, ninachokichukua 
mimi ni taarifa hii inayoeleza kujengwa kwa madarasa tisa, 
hilo moja ni la kwake Mkurugenzi kichwani" alisisitiza Dkt. 
Kijaji

Aidha, Dkt. Kijaji alibainisha kutoridhika kwake na gharama 
za ujenzi wa darasa moja kwa shilingi 17m na kwamba kiasi 
cha shilingi milioni 200 kilichotolewa na Japan kutekeleza 
mradi huo kingeweza kujenga madarasa hata 20.

Awali, akitoa maelezo yake kuhusu ujenzi wa mradi huo 
unaojengwa na Kampuni ya Juve Construction and 
General Trading ya Mjini Kigoma, Dkt. John Tlatlaa, 
alisema kuwa mfadhili, Serikali ya Japan ilitoa masharti ya 
majengo hayo kujengwa na mkandarasi badala ya kutumia 
nguvukazi-force account.

"Baada ya Japan kutuma fedha hizo na kuingia kwenye 
akaunti ya Manispaa tulimwita mkandarasi na kumweleza 
kuwa kutokana na wingi wa fedha hizo, atalazimika kuongeza 
darasa moja zaidi" alijitetea Kaimu Mkurgenzi huyo.
Maelezo hayo pamoja na ya nyongezwa kwamba majengo 
mapya yatawekewa nguzo ndio maana gharama zake ziko 
juu, hayakumridhisha Dkt. Kijaji na kuamuru uchuguzi wa 
kina ufanyike.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.