RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ameutaka uongozi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii
Zanzibar (ZSSF) kufanya kazi kwa uadilifu kwa kuyatekeleza maagizo ya Serikali
katika ukodishaji nafasi za kufanyia biashara katika jengo la Jumba la Treni
“Chawl” lililofanyiwa ukarabati mkubwa.
Dk. Shein aliyasema hayo
leo katika hafla ya ufunguzi wa jengo la Jumba la Treni “Chawl building”,
lililopo Darajani Mjini Unguja, ambalo limefanyiwa ukarabati mkubwa na Srikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF).
Katika maelezo yake Rais
Dk. Shein aliutaka uongozi huo wa (ZSSF) kuwa wawazi, wasiwe na muhali na wala
wasimpendelee mtu yeyote katika ukodishwaji wa nafasi za kufanyia biashara
katika jumba hilo la maduka.
Rais Dk. Shein pia,
alisisitiza haja kwa uongozi huo wa (ZSSF) kutofanyabiashra kirafiki wala
kujuana kwani biashara ni heshima, hivyo ni vyema wakafanya biashara kwa lengo
la kupata faida.
Aliongeza kuwa ni vyema
watu wote wakazingatia kuwa nafasi na fursa zilizopo katika jengo hilo ni chache
na kwa hivyo, haitowezekana kila mtu anayehitaji apewe sehemu ya kufanyia
shughuli zake katika jengo hilo.
Alieleza matumaini ya
Serikali kuwa kukamilika kwa mradi wa matengenezo ya nyumba ya treni
kutachochea kasi ya ukuaji wa shughuli za biashara katika mji wa Zanzibar.
Dk. Shein aliwashangaa
wale wote wanaokasirika na kununa wakati Serikali ikifanya mambo mazuri kwani
lazima Serikali itekeleze mambo yake ikiwa ni pamoja na kujenga miundombinu
yake ya kihistoria kwa madhumuni ya kuienzi historia ya Zanzibar.
Aidha, Rais Dk. Shein
alieleza kuwa kuna baadhi ya miji mikubwa ulimwenguni nje ya Afrika, ambayo
inasifika kwa usafi ukiwemo mji wa Singapore, Honolulu, Copenhagen, London,
Geneva, Stockholm na mengineyo, hivyo ni vyema na mji wa Zanzibar ukafuata
mkondo huo.
Alieleza kuwa hivyo, ni
jambo la busara sana na Zanzibar ikaiga tabia ya kuvitunza vitu vyake katika
hali zote ikiwemo usafi ili maeneo yake
nayo yasifike kwa kuwa na mazingira safi yanayovutia.
Alisisitiza suala la
usafi kwa miji yote ya Unguja na Pemba na kueleza haja ya jengo hilo ya
kulitunza na kuliweka katika hali ya usafi ili lizidi kudumu kwa miaka mengine
200 ijayo.
Akitoa historia fupi ya
jumba hilo, Rais Dk. Shein alieleza kuwa Jumba hilo ambalo kwa lugha ya
Kiengereza linaitwa “Chawl Building” ambalo neno Chawl linatokana na moja ya
lugha za Kihidni inayoutwa Marati (Marathi) ambayo inazungumza na takriban watu
68 milioni wa Mashariki ya India.
Alisema kuwa historia
inaeleza kuwa majengo kama hayo yalianza kujengwa mwishoni mwa karne 18 kuingia
19 ambayo ni majengo marefu yanayofikia ghorofa 4 mpaka 5 ambapo wka upande wa
Zanzibar jumba hilo lilijengwa mnamo mwaka 1880.
Kwa mujibu wa Maelezo ya
Dk. Shein aliyejenga Jumba hilo alikuwa ni mtawala wa Kisultani wa Zanzibar
aliyeitwa Barghash bin Said ambalo alijenga kwa dhamira ya kwua chanzo cha
kuzalisha mapato katika kuanzisha na kuendeleza mradi wa maji safi na salama ndani ya mji wa Zanzibar.
Aliongeza kuwa kodi
zilizokusanywa kutokana na jumba hilo ndizo zilizokamilisha miundombinu ya maji
safi na salama katika mji mkuu wa Zanzibar, lakini miundombinu hiyo
haikutosheleza kusambaza maji kwa mahitaji ya sehemu zote za Unguja.
Kuhusu ujenzi wa maduka
ya kisasa katika eneo la Darajani kwenye mradi uliopewa jina la “Darajani
Corridor”, Dk. Shein alieleza kuwa inayochelewesha sio Serikali bali ni Shirika
la UNESCO kutokana na taratibu za Mamlaka ya miji mikongwe duniani lakini
alieleza kuwa hata hivyo wapo baadhi ya watu kutoka Zanzibar ambao walipeleka
fitna juu ya ujenzi wa sehemu hiyo huko UNESCO.
Dk. Shein alieleza kuwa
hata hivyo, ujenzi wake upo pale pale ambapo mradi huo utatekelezwa baada ya
kupokea maoni ya UNESCO ambayo yanategemewa yataletwa baada ya Serikali
kuwasilisha kwao maelekezo waliyoyatoa takriban miaezi sita iliyopita na
kueleza matarajio yake juu ya ujenzi huo kuanza mara tu kukamilika mipango
hiyo, hivyo aliwataka wananchi kuendelea kuwa wavumilivu na lolote litakalokuwa
watajuulishwa.
Kwa upande wa Skuli ya
Darajani, Dk. Shein alisema kuwa skuli hiyo haitovunjwa kama wanavyoeleza watu
wasiojua ukweli na badala yake jengo hilo litatumika kwa ajili ya matumizi
mengine na wanafunzi wake watahamishiwa katika skuli mpya inayojengwa huko
Rahaleo pamoja na wale wa skuli ya Vikokotoni ambao jengo lao hilo la skuli
litavunjwa kwani halimo katika historia na wao pia watahamia Rahaleo.
Akieleza kuhusu ujenzi
wa maduka makubwa “Shopping Malls” katika eneo la Michenzani nao upo pale pale
ambapo Taasisi ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF) ndio utakaojenga maduka hayo
ambapo ujenzi wake hauna muda mrefu utaanza.
Rais Dk. Shein alitumia
fursa hiyo kwa kuwashukuru na kuwapongeza wananchi kwa kustahamili wakati wote
wa ujenzi wakiwemo wale wote waliokuwa wakiishi na kufanya biashara katika
Jumba hilo na kuipongeza Kampuni ya ujenzi ya CRJE East Afrika, wakandarasi wasadidi,
Mshaidizi Ujenzi Kampuni ya CONS Africa na wengineo.
Aliipongeza (ZSSF),Bodi
yake kwa kuyawezesha kwa ufanisi matengenezo ya jengo hilo na kuupongeza
uongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango kwa usimamizi wao mzuri wa kuhakikisha
ujenzi huo unakamilika.
Nae Waziri Fedha na
Mipango Dk. Khalid Salum Mohamed alitumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa Rais
Dk. Shein kwa ushauri wake, maelekezo na usimamizi sambamba na utekelezaji wake
wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM katika kuhakikisha ahadi za ujenzi wa jengo hilo inatekelezwa.
Alisema kuwa dhamira ya
Rais Dk. Shein ni kuhakikisha mji wa Zanzibar unarejea kwenye haiba yake na
unaendelea kuwa kivutio kwa wageni na wenyeji wa Zanzibar.
Katika maelezo yake Dk.
Khalia alieleza miradi mbali mbali ambayo imetekelezwa na mengine inaendelea
kutekelezwa katika uongozi wa Ras Dk. Shein ambayo imeleta faida kuwa kwa ile
ambayo imeshatekelezwa ukiwemo mradi wa ZUSP katika mji wa Unguja na Pemba huku
akieleza azma ya kuutengeza mji mpya katika maeneo ya Chumbuni na Kwahani mjini
Unguja.
Pamoja na hayo, alieleza
hatua za ujenzi wa hoteli ya Bwawani ambao utaanza hivi karibuni pamoja na
ujenzi wa jaa la kisasa katika maeneo ya Kibele, Mkoa wa Kusini Unguja.
Mapema Mkurugenzi
Mwendeshaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) Sabra Issa Machano
alieleza kuwa ujenzi wa Jumba hilo hadi kumalizika kwake umegharimu TZS Bilioni
11.5.
Aliongeza kuwa Jumba
hilo lina milango ya maduka ya biashara 52, sehemu ya IT, eneo la kusalia kwa
wanawake, nyumba 10 za kuishi, mkahawa, sehemu ya mazoezi, duka la mahitaji
mbali mbali ‘supermarket’ ambapo pia, jengo hilo limezingatia watu wenye
mahitaji maalum pamoja na lifti kwa ajili ya kuwafikisha wananchi sehemu walinazokusudia.
Alisisitiza kuwa katika
malengo hayo ni katika kuhakikisha mahitaji yanapatikana kiuchumi, kijamii na
kiuchumi na kueleza kuwa ndani ya miaka 10 fedha za ujenzi huo Serikali
itajilipa huku akitumia fursa hiyo kwa kupongeza Rais Dk. Shein kwa uwamuzi
wake wa kulikarabati jengo hilo.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment