Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt Ali Mohamed Shein na Mkurugenzi Mkaazi wa UN Tanzania Mr. Alvaro Rodriguez wakipiga makofi baada ya kuondoa kipazia katika Bunner ya Uzinduzi wa Programu ya Pamoja na Zanzibar katika Kuwaendeleza Wajasiriamali na Wakulima Wanawake wa Mwani Zanzibar na Vijana, Hafla hiyo ya Uzinduzi imefanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
pamoja na wananchi wake inatambua mchango mkubwa wa Umoja wa Mataifa (UN)
pamoja na Mashirika yake katika kuimarisha maendeleo endelevu ya Zanzibar.
Dk. Shein aliyasema hayo
leo katika uzinduzi wa “Programu ya Pamoja ya Zanzibar” (ZIP), hafla
iliyofanyika huko katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil, Kikwajuni Mjini
Zanzibar ambayo ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Makamo wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd.
Katika hotuba yake, Rais
Dk Shein alisema kuwa program hiyo sio tu itasaidia kuimarisha maendeleo ya
Zanzibar bali itasaidia sana katika kufikia malengo ya maendeleo yaliyowekwa na
Umoja wa Mataifa (UN).
Rais Dk. Shein alisema
kwamba, malengo ya Mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa Zanzibar yako wazi katika kila
sekta na yanafahamika kwa wananchi wote wa Zanzibar jinsi yalivyolenga katika
kuimarisha sekta za maendeleo.
Alisema kuwa UN imekuwa
ikifanya kazi na kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo elimu, afya, upatikanaji
wa maji safi na salama, utawala bora, uimarishaji wa haki za binaadamu, uwezeshaji,
mapambano ya udhalilishaji wa kijinsia pamoja na uhifadhi wa mazingira.
Dk. Shein alitumia fursa
hiyo kutoa shukurani kwa Mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN) kwa mashirikiano
inayotoa katika kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo hapa Zanzibar.
Alisema kuwa programu ya
pamoja inalenga zaidi kushirikiana na Serikali katika kupunguza vifo vya uzazi,
ukatili dhidi ya wanawake na watoto, uwezeshaji wa kiuchumi kwa wanawake
kupitia zao la mwani pamoja na uratibu wa utekelezaji wa malengo ya dunia.
Pamoja na hayo, Rais Dk.
Shein aliongeza kuwa programu hiyo itasaidia zaidi kuimarisha uhusiano uliopo
pamoja na kuiwezesha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kufikia malengo yake ya
maendeleo ya muda mrefu na muda mfupi uliojiwekea.
Dk. Shein aliuhakikishia
Umoja wa Mataifa (UN) kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itahakikisha kuwa
kila sekta inayohusika katika utekelezaji wa mpango huo inatekeleza majukumu
yake ipasavyo.
Aidha, Dk. Shein alieleza
kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itahakikisha kwamba kwa pamoja
inazifanyia kazi changamoto mbali mbali zinazoweza kujitokeza katika programu
hiyo mpya.
Aliongeza kuwa Serikali
kwa kushirikiana na Mashirika ya UN itatumia uzoefu ulionao katika kutekeleza programu na miradi mbali mbali iliyofanywa
hapo siku za nyuma baina ya Serikali na Mashirika hayo ili kutekeleza vyema
progamu hiyo.
Katika hotuba yake hiyo,
Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya wafanyakazi kuleta mabadiliko ya fikra na
mawazo na kuacha kufanya kazi kwa mazoea kama anavyosisitiza mara zote ili
kuweza kuifanikisha progamu hiyo kwa ufanisi mkubwa.
Rais Dk. Shein alitilia
mkazo haja ya kuwa wabunifu katika kubuni na kutekeleza miradi ya maendeleo
yenye tija na inayokwenda sambamba na mazingira pamoja na mahitaji halisi ya
wananchi wa Zanzibar badala ya kusubiri wataalamu kutoka nje waje kubuni miradi
kwa ajili ya Zanzibar.
Alisisitiza kuwa
Zanzibar kwa kuweza kubuni miradi yake wenyewe itakuwa ni rahisi kwa Umoja wa Mataifa
kutoa ushirikiano wake kwa Zanzibar kwa kuzingatia mipango na mahitaji
yaliyopo.
Dk. Shein alisisitiza
umhimu wa ushirikiano baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, sekta binafsi
na asasi za kiraia katika utekelezaji wa miradi mbali mbali inayotekelezwa na
mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa kuzingatia kwamba mashirikiano ya pamoja
yanahitajika.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein alisisitiza umuhimu wa kuwepo suala zima la uwajibikaji, uwazi pamoja
na kujidhatiti katika kufikia malengo yaliyowekwa.
Nae
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment