Habari za Punde

TRA YATAJA WALENGWA WANAOSTAHILI MSAMAHA WA RIBA NA ADHABU YA MALIMBIKIZO YA KODI

Na Veronica Kazimoto.Tabora                                                         
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewataja walengwa wanaostahili kuomba msamaha maalum wa riba na adhabu ya malimbikizo ya madeni ya kodi kwa asilimia 100 ambapo 
mwisho wa kutuma maombi ya msamaha huo ni tarehe 30 Novemba, 2018.

Akizungumza wakati wa mkutano wa washauri wa walipakodi (Tax consultants) mkoani Tabora, Afisa Elimu Mkuu kwa Mlipakodi wa mamlaka hiyo Rose Mahendeka amesema Walengwa wa msamaha huu ni makampuni, taasisi na watu binafsi ambao wamewasilisha ritani za kodi lakini bado wanadaiwa kodi yote au sehemu ya kodi zitokanazo na ritani hizo.

"Walengwa wengine ni wale wote ambao hawajawasilisha ritani za kodi, hawajasajiliwa na kupatiwa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) au Namba ya Usajili wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na wale walio wasilisha pingamizi au rufaa za kodi ambazo bado zinashughulikiwa katika ofisi za TRA, Bodi ya Rufaa na Mahakama ya Rufani za kodi", alisema Mahendeka.

Aidha, amewataja wasiohusika na msamaha huu kuwa ni pamoja na wale ambaowangestahili kupata msamaha lakini tayari wameshalipa madeni yao, ambao masuala yao ya kikodi yapo katika hatua ya ukaguzi au uchunguzi, wana madeni ya nyuma ya kodi ambayo yanatokana na kesi za jinai za kodi, utakatishaji fedha, usafirishaji wa binadamu au shughuli nyingine haramu kama ilivyothibitika kisheria.

"Wengine ambao hawahusiki na msamaha huu ni taasisi,makampuni na watu binafsi ambao wana madeni ya nyuma ya kodi yanayotokana na adhabu zilizoamuliwa tayari au adhabu za makosa yatokanayo na uzembe wa kukusudia uliobainika kisheria pamoja na wenye riba au faini zilizotokana na kutoa au kutumia risiti za kielektroniki za kughushi," alibainisha Mahendeka.

Kwa upande wake Afisa Elimu kwa Mlipakodi wa TRA Chama Siriwa ametoa wito kwa washauri wa walipakodi mkoani hapa kuendelea kuwaelimisha wafanyabiashara na wale wote wenye taasisi na makampuni mbalimbali yenye malimbikizo ya madeni ya kodi kuwahi kutuma maombi ya msamaha huo kabla muda uliopangwa haujamalizika.

"Mimi napenda tu kusisistiza kuwa mwisho wa kutuma maombi ya msamaha huu ni tarehe 30 Novemba, 2018. Hivyo, natoa wito kwenu washauri wa walipakodi muendelee kuwaelimisha wafanyabiashara na wote wenye taasisi na makampuni kutuma maombi mapema ili waweze kunufaika na msamaha huu," alieleza Siriwa.

Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania ilitangaza msamaha wa riba na adhabu ya malimbikizo ya madeni ya kodi mwezi Julai, 2018 kwa lengo la kutoa unafuu kwa walipakodi wenye malimbikizo ya madeni ya riba na adhabu kwa kusamehe madeni yao na kuwapa fursa ya kulipa malimbikizo ya madeni ya msingi ya kodi - principal tax mara moja au kwa awamu ndani ya mwaka wa fedha wa 2018/19.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.